Dar es Salaam. Mzigo wa makaratasi, kusahau fomu muhimu, pamoja na ucheleweshaji wa taratibu za usajili wa mpango wa bima ni miongoni mwa changamoto zilizowalazimu mawakala wa bima kubadili mfumo wao wa utendaji, hatua iliyosababisha kuzinduliwa kwa mfumo wa kidijitali wa J-Force.
Mfumo wa zamani uliathiriwa pia na kupotea kwa baadhi ya nyaraka, makosa ya kibinadamu katika kujaza taarifa, pamoja na kukosekana kwa nakala ya kumbukumbu kwa mteja ambaye mara nyingi alisaini mkataba bila kupata maelezo ya mpango wake kwa undani.
Akizungumza leo, Novemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Mkufunzi wa Kampuni ya Jubilee Life Insurance, Constantine Ouma, amesema kwa miaka mingi mawakala wamekuwa wakilazimika kubeba mzigo mkubwa wa makaratasi wanapokwenda kwa wateja, ikiwa ni pamoja na bahasha, karatasi za ziada na fomu mbalimbali zinazotumika katika mchakato wa usajili.
“Mara nyingi wakala anaenda kwa mteja, lakini anagundua kuwa amesahau fomu ya lazima ofisini. Huo mzigo wa makaratasi umekuwa ukichelewesha taratibu na wakati mwingine kurudisha mchakato nyuma,” amesema Ouma.
Amesema kupitia mfumo wa J-Force, wakala hatalazimika tena kubeba makaratasi, badala yake ataweza kumtumia mteja fomu na maelezo yote kwa njia ya mtandao, ambapo mteja ataweza kuyasoma, kuyaangalia na kuthibitisha usahihi wake kupitia barua pepe kabla ya kuendelea na hatua nyingine.
“Kwa sasa mteja anapokea ‘quotation’, maelezo ya mpango wake na masharti kupitia baruapepe yake. Anayapitia mwenyewe na akithibitisha, taratibu nyingine zinaendelea bila kusafirisha makaratasi,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance, Helena Mzena amesema mfumo huo ni hatua kubwa ya mageuzi ya kiteknolojia ndani ya kampuni hiyo na sekta ya bima kwa ujumla.
Amesema programu hiyo imebuniwa kwa lengo la kurahisisha usajili wa wateja na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, huku ikiwapa mawakala uwezo wa kufanya kazi popote walipo bila kwenda ofisini.
“Kupitia application hii, mawakala wetu wataweza kusajili wateja kwa urahisi, kutoa mikataba kwa haraka, kupata taarifa zote muhimu, kuona michango ya wateja wao pamoja na kuona kamisheni zao bila usumbufu,” amesema Helena.
Amesema teknolojia hiyo itasaidia kufikia malengo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 50 ya Watanzania wanakuwa na bima ya maisha.
“Kwa hivyo ili kufikia mamilioni ya Watanzania unaohitajika kuwafikia, haiwezekani kubaki kwenye makaratasi. Teknolojia kama hii ndiyo suluhisho, kwa sababu inawafikia watu hadi vijiji vya mbali,” amesema.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Bima Tanzania, Vedasto Rwegoshora amesema ujio wa mfumo mpya wa kidigitali wa J-Force utasaidia kuondoa changamoto ambazo mawakala wamekuwa wakikutana nazo kwa muda mrefu, hasa kubeba mizigo ya makaratasi na kuchelewa kwa taarifa kutoka makao makuu.
Rwegoshora amesema mawakala hapo awali walilazimika kubeba nyaraka nyingi wanapokwenda kufanya kazi, hali iliyosababisha usumbufu na kupunguza ufanisi.
“Ulikuwa unaweza kukutana na wakala ana sanduku au briefcase, ukadhani anaenda likizo kumbe ni makaratasi yote ya kazi. Kwa hivyo J-Force imekuja kutatua hili tatizo kikamilifu,” amesema Rwegoshora.
