Dar es Salaam. Katika historia ya Tanzania, viongozi wa dini wamekuwa sehemu muhimu katika maamuzi ya mambo yanayoibua mjadala wa kitaifa, lakini nafasi yao mara kadhaa imekuwa ikikumbwa na mitazamo tofauti, hasa wanapokemea masuala yahusuyo siasa.
Wakati mwingine wanapotoa maoni juu ya mwenendo wa Serikali au mwelekeo wa nchi, hukosolewa na kutakiwa kubaki kwenye kulea waumini wao kiroho, lakini pindi Taifa linapotikiswa na sintofahamu za kisiasa, wao ndio hutazamwa kama daraja muhimu la kuunganisha pande hasimu.
Mvutano huu wa mitazamo tofauti juu ya nafasi ya viongozi hawa wa kiroho unaibua mjadala mpana kuhusu mipaka halisi kati ya dini na siasa katika jamii ya Kitanzania, kwa kuzingatia nafasi na wajibu wa kijamii wa viongozi hawa.
Kwa miongo mingi, viongozi wa dini zote, wa Kiislamu na Kikristo, wamekuwa sehemu ya kijamii inayoheshimika kwa makundi yote kutokana na msimamo wao wa maadili, uadilifu karama ya kipatanishi katika jamii bila kuwa na upande.
Hata hivyo, mchango wao unapogusa masuala ya utawala, uchaguzi au ukosoaji wa baadhi ya mamlaka, mijadala tofauti huibuka.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi huamini kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuzungumzia imani na maadili pekee, wakionya kwamba kuhusika kwao kwenye siasa kunaweza kuchochea mgawanyiko au kutumiwa kisiasa kuchochea udini
Mifano kadhaa inaonyesha baadhi ya viongozi wa kiroho walipozungumzia mivutano ya kisiasa wakikemea na kushauri kuhusu haki na uhuru wa kidemokrasia, kauli zao zilichochea ukosoaji mkali, baadhi wakisema hazipaswi kutoka kwa watumishi wa Mungu.
Hali kama hiyo imekuwa ikijirudia mara kadhaa, hususan pale viongozi wa dini wanapohoji mambo yanayogusa uhuru, utawala bora au haki za binadamu. Wengi hukosolewa na kutakiwa kukaa kimya huku wengine wakiadhibiwa kwa namna mbalimbali, ikiwemo kufungiwa nyumba zao za ibada au kwa misukosuko mingine.
Katika mtazamo mwingine, taswira juu ya nafasi ya viongozi hawa hubadilika pindi dalili za tishio la amani zinapoonekana kutokana na mtikisiko wa kisiasa. Wadau wote wakiwemo wanasiasa wenyewe hujikuta wakihitaji zaidi sauti za viongozi wa dini zitawale majukwaa ya mijadala, ili kuponya Taifa.
Hivi karibuni, mifano ya hali hii ni mingi, ambapo kutokana na sintofahamu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 ambao uliambatana na maandamano yaliyopelekea vurugu, kumekuwa na matamko mbalimbali ya taasisi mbalimbali zikiwemo za dini huku jamii, Serikali na wanasiasa wakihitaji zaidi sauti za viongozi wa dini zaidi katika kulirejesha Taifa kwenye njia kuu.
Hali hii inakoleza mjadala wa kimaadili na kiuelewa kuhusu nini jamii inataka viongozi wa dini wazungumze kuhusu matatizo yanayoikabili jamii, ambayo nao ni sehemu ya jamii hiyo inayoathiriwa na mambo husika.
Hii ni kutokana na hali kuwa kauli yao inapoonekana kukosoa na kukemea basi upande wanaoukosoa huwatuhumu kuwa viongozi wa dini wanafanya siasa, lakini wakitoa wito wa amani baada ya sintofahamu, hupongezwa na kuitwa nguzo ya taifa. Kwa maneno mengine, tathmini ya kauli zao hutegemea upepo wa kisiasa uliopo na si wajibu wao kwa jamii.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kijamii na baadhi ya viongozi wa dini wanasema kundi hili lina nafasi ya kipekee ya katika jamii.
Wanasema, hata katika historia ya enzi na enzi viongozi wa dini historia imewaonyesha wakiwa mstari wa mbele katika kutetea na kukemea mambo ya kijamii na kisiasa ikiwemo kuwezesha mataifa yao kupigania uhuru enzi za harakati za kudai uhuru dhidi ya ukoloni.
Wanasema kuwa watumishi wa Mungu nao ni binadamu na sehemu ya jamii husika, hivyo wana haki na wajibu wa kushauri na kukemea mambo yanayogusa jamii zao.
Mdau wa masuala ya Haki za Binadamu nchini, Dk Ananilea Nkya anasema siasa ni mhimili mkuu unaogusa nyanja zote za maisha ya binadamu hivyo viongozi wa dini kama sehemu ya jamii wana wajibu wa kutoa maoni, kushauri na kukemea yale wanayoona yafaa.
“Wanasiasa wanapaswa kutambua kuwa viongozi wa dini wana wajibu vilevile katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kufanya hivyo si kosa.
“Kiongozi wa dini anaongoza watu, sasa kukemea mambo ya haki, uhuru na uwajibikaji ukisema ni kosa, unataka aongelee yapi?” anahoji Dk Nkya ambaye pia ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania.
Kwa upande wake katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, anasema viongozi wa dini wanapozungumzia masuala ya kijamii na kisiasa ni sehemu ya kutimiza wajibu wao wa kijamii kwa jamii na kwamba wanaingilia masuala yasiyowahusu.
“Viongozi wa dini mbali na kutoa huduma ya kiimani pia tuna wajibu wa kijamii katika kusimamia haki na utu,” anasema.
Kwa mujibu wa Shekh Ponda, Shura ya maimamu ambayo ni moja ya taasisi kubwa za Kiislamu, inayo kamati maalumu ambayo inahusika na masuala ya siasa moja kwa moja, hivyo si sahihi kuwapa mipaka viongozi hao kwenye mambo ya jamii yakiwemo ya kisiasa.
Mwenyekiti wa Kamati maalum ya Maaskofu na Masheikh ya Haki, Amani na Maadili Tanzania, Askofu William Mwamalanga anasema viongozi wa dini wanao wajibu wa moja kwa moja kwa jamii yao na mazingira yanayoizunguka jamii hiyo yakiwemo ya kisiasa.
Askofu huyo anasema watumishi wa Mungu wanapaswa kutazamwa kama nuru ya ulimwengu na kauli zao na matendo yao kuchukuliwa kama mfano mwema wa kuponya na kuelekeza jamii yaliyo mema.
“Neno la Mungu linamzungumzia mwanadamu na mazingira yanayomzunguka na jamii yake kwa ujumla, hivyo watumishi wa Mungu tunaagizwa kuwa nuru ya ulimwengu kwa maneno na matendo yetu kwa jamii inayotuzunguka,” amesema askofu huyo.
Anasema ni bahati mbaya kuwa baadhi ya watu katika jamii hawatambui kuwa viongozi wa dini wanao wajibu kwa ulimwengu na si ndani ya nyumba zao za ibada pekee, akibainisha kuwa kukemea na kushauri kuhusu mambo yanayogusa jamii yakiwemo yale ya kisiasa, ni wajibu wao wa kijamii.
“Tatizo wapo watu wasioelewa kuwa sisi watumishi wa Mungu kazi yetu ni kutengeneza palipoharibika na kuleta nuru palipo na giza,” amesema Askofu huyo akipongeza Shura ya Maimamu kwa kusimamia vyema wajibu huo kwa jamii.
“Tunawapongeza sana Shura ya Maimamu tumeona tamko lao la hivi karibuni kuhusu mwenendo wa uchaguzi, wameongea mambo ya msingi sana kwa jamii yetu hasa katika kipindi hiki nchi yetu ikiwa gizani. Viongozi wa dini lazima tukemee kama sehemu ya wajibu wetu wa kuwa nuru kwa ulimwengu palipo na giza.
Ili kuondoa giza kwenye jamii, viongozi wa dini zote ni vyema tukaungana kwa masilahi ya nchi, na wadau wote watuelewe kuwa sisi kuongelea mambo ya siasa na kijamii ni jambo la kutimiza wajibu wetu tunaloagizwa kwa mujibu wa utumishi wetu,” amesema.
