Morogoro. Maandalizi ya maonyesho ya biashara, viwanda na kilimo ya mwaka 2025 yanayotarajiwa kuanza kesho hadi Novemba 30, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri, Manispaa ya Morogoro, yamefikia asilimia 90.
Jumla ya washiriki 201 wamethibitisha kushiriki, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kadri siku zinavyozidi kusogea.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano, Novemba 18, 2025, Meneja wa Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Mkoa wa Morogoro, Dustan Mziwanda amesema maonyesho hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha wajasiriamali kutoka sekta mbalimbali zikiwamo za biashara, kilimo, viwanda na huduma.
Amesema washiriki waliothibitisha mpaka sasa, ni wale wanaotoka katika kampuni za sekta binafsi, taasisi za Serikali pamoja na mashirika mengine.
“Washiriki 201 wamesajiliwa hadi leo (jana), na tunatarajia idadi inaweza kuongezeka ifikapo siku ya ufunguzi wa maonyesho yenyewe,” amesema Mziwanda.
Ameeleza kuwa maonyesho hayo yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya TCCIA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yakilenga pia kuwaonyesha wananchi maendeleo ya teknolojia katika kilimo na viwanda.
Hivyo, ametoa wito kwa wakazi wa Morogoro na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kuona bidhaa na huduma mbalimbali kama za uzalishaji wa viazi mviringo kutoka Nongwe wilayani Gairo, vinavyolimwa katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.
Aidha, Mziwanda amesema mkoa huo unazidi kuwekeza katika kilimo cha matunda kupitia mafunzo kwa vijana kuhusu uandaaji wa miche ya matunda ya muda mfupi, yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Ameeleza kuwa wanahamasisha kilimo cha karafuu, kokoa na bustani za matunda kama njia ya kuongeza kipato na kupanua wigo wa uzalishaji, badala ya kuendelea kutegemea kilimo cha maua pekee.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji katika sekta za kilimo, madini, mifugo na utalii.
Ametaja hifadhi za Mikumi, Udzungwa, Nyerere na Wami–Mbiki, kama maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuvutia wawekezaji.
“Maonyesho haya yatatoa nafasi kwa taasisi na mashirika kuonyesha shughuli zao na kwa wawekezaji kubaini fursa zilizopo Morogoro,” amesema Malima, akisisitiza kuwa mkoa huo umejipanga kikamilifu kuendelea kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa wananchi wake.