Mzize ang’ara tuzo za CAF 2025

Mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars, Clement Mzize ameshinda Tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025 katika hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mzize ameshinda tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga msimu wa 2024-2025 hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikishinda 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Januari 4, 2025.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mzize alikuwa anashindana na wenzake 12 lakini kura zilizopigwa na mashabiki, zimempa ushindi huo.

Katika mchakato wa kulisaka bao bora, CAF lilitangaza wachezaji 13 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ambapo mashabiki wakapewa nafasi ya kuchagua mshindi.

Orodha hiyo iliandaliwa na Kamati Maalum ya Ufundi ya CAF ambapo kura zilianza kupigwa Alhamisi, Novemba 6, 2025 na kufungwa Jumatano, Novemba 12, 2025.

CAF liliweka kituo maalum cha kupigia kura kupitia CAFOnline.com na kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa CAF, kura za mashabiki zinachangia asilimia 100 ya matokeo ya mwisho, jambo linaloifanya tuzo hii kuwa ya kipekee kwani ndiyo pekee inayotegemea maoni ya moja kwa moja ya umma.

Mzize ameibuka mshindi mbele ya Abdellah Ouazane (Morocco vs Tanzania-AFCONU17), Anas Roshdy (Misri vs Afrika Kusini -AFCONU17), Asharaf Tapsoba (Burkina Faso vs Cameroon-AFCONU17), Barbra Banda (Zambia vs Morocco-WAFCON2024).

Wengine ni Calvin Fely (Madagascar vs Morocco-CHAN2024), Ghizlane Chebbak (Morocco vs Nigeria-WAFCON2024), Ibrahim Adel (Pyramids vs ES Tunis-Ligi ya Mabingwa), Jean-Claude Girumugisha (Al Hilal SC vs MC Alger-Ligi ya Mabingwa).

Pia kuna Ndabayithethwa Ndlondlo (Afrika Kusini vs Uganda-CHAN2024), Oussama Lamlioui (Morocco vs Madagascar-CHAN2024), Refiloe Jane (Afrika Kusini vs Mali-WAFCON2024) na Soufiane Bayazid (Algeria vs Uganda-CHAN2024).