MZUMBE YAJIPANGA KUJITANUA KIMATAIFA – MICHUZI BLOG

FARIDA MANGUBE , MOROGORO

Chuo Kikuu Mzumbe kimejipanga kujitanua kimataifa kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa, kuboresha mitaala na kupokea wanafunzi kutoka nje ya nchi, ikiwa ni mkakati wa kukuza ubora wa elimu na kuongeza mapato.

Akizungumza katika Baraza la 25  la wahitimu chuo kikuu Mzumbe, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, amesema mpango huo unalenga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi na wale kutoka mataifa mengine kuja kusoma Mzumbe, hatua itakayokifanya chuo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuongeza ushindani katika soko la elimu ya juu.

Katika hafla hiyo, Melina Baradyana mwanafunzi Shahada ya awali ya Usimamizi wa Mazingira ameibuka mwanafunzi bora wa mwaka na kujinyakulia zawadi kedekede kutoka kwa menejimenti ya pamoja na wadau wakiwemo BRELA ambao wamemzawadia Shilingi 500,000 huku Beki ya CRDB wakimzawadia  Shilingi milioni 1.5

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Melina amesema zawadi hizo ni motisha kubwa kwake na kwa wanafunzi wengine, na kwamba kupitia taaluma yake atachangia jitihada za serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kufanya tafiti.

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Philemon Luhanjo, amewataka wanafunzi kuwa na imani na Chuo Kikuu Mzumbe akisema kimeendelea kuzalisha viongozi wa ngazi za juu nchini, akitoa mfano wa Rais wa Awamu ya Sita pamoja na Makamu wa Rais ambao ni miongoni mwa wahitimu wa chuo hicho.

Amesema amevutiwa na maendeleo ya chuo hicho likiwemo ongezeko la idadi ya wanafunzi na programu nyingi zinazotolewa sasa, akitoa wito kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka nje ya Tanzania ili kukuza mapato na kuimarisha hadhi ya kimataifa.