Dar es Salaam. Kesi tatu za uhaini zinazowakabili washtakiwa 227 zimetajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, bila washtakiwa kuwepo mahakamani, huku Jamhuri ikibainisha bado inaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kula njama na kutenda kosa la uhaini, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 katika Jiji la Dar es Salaam.
Wakati kesi hizo zinasikilizwa kwa njia ya mtandano, ndugu, jamaa na marafiki walimiminika kwa wingi mahakamani hapo kwa kile walichodai wapendwa wao wangeweza kuachiwa huru leo Jumatano, Novemba 19, 2025.
Wengine wakidai wamefika mahakamani hapo ili kujiridhisha iwapo wapendwa wao wameshtakiwa kwa kesi ya uhaini kwa kuwa walipofikishwa kwa mara ya kwanza, baadhi ya ndugu hawakupata taarifa mapema, hivyo walishindwa kufika.
Baadhi ya ndugu wa washtakiwa hao akiwamo Asha Seleman ambaye ndugu zake wawili wameshtaki kwa uhaini na Neema Samuel, walidai wamefika mahakamani hapo baada ya kusikia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa wale ambao walifuata mkumbo kwenye maandamano na hawakudhamiria kufanya makosa, wafutiwe makosa yao na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Rais Samia alitoa kauli hiyo Ijumaa Novemba 14, 2025 Dodoma, wakati akilihutubia na kulizindua Bunge la 13 jijini Dodoma ambapo alitoa msamaha kwa washtakiwa hao na kuagiza vyombo vya dola hususan DPP kuwachuja na kuwaachia huru wale waliofuata mkumbo na kushiriki vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu, uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kesi ya kwanza ni kesi ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26392 ya mwaka 2025 yenye jumla ya washtakiwa 38, Jamhuri imedai upelelezi wake bado unaendelea.
Hata hivyo, kabla ya kesi hiyo kutajwa, hakimu Beda amehoji baadhi ya washtakiwa wa kesi hiyo hawaonekani kwenye video iliyounganishwa kutoka katika ukumbi wa usikilizwaji wa kesi kwa njia ya mtandao uliopo katika Mahakama ya Kisutu, na washtakiwa waliopo Segerea.
Akijibu swali hilo, ofisa wa Magereza kutoka gereza la mahabusu la Segerea, Sajenti Hosea John ameieleza Mahakama baadhi ya washtakiwa wamepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Baada ya majibu hayo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi, amedai upelelezi bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Moshi ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Novemba 19, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kutajwa kwa njia ya video.
Moshi baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi Paul Kisabo aliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo kwa muda ili washtakiwa wapelekwe mahakamani hapo, badala ya kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya video.
Kisabo amedai kama kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa njia ya video, basi walipaswa kupewa notisi ya siku saba kabla ya kesi hiyo kutajwa, lakini upande wa mashtaka hawakufanya hivyo.
“Mheshimiwa hakimu, naomba Mahakama yako itoe amri ya washtakiwa kuletwa mahakamani hapo na mawakili wa pande zote tuwepo mahakamani ana kwa ana ili kesi hii isikilizwe,” amesema Wakili Kisabo.
Kwa upande wake, Wakili Maduhu William na Sisti Masawe wamedai kesi hiyo ni kubwa na inahitaji umakini hivyo Jamhuri walitakiwa kukamilisha upelelezi kwa wakati na sio kuiahirisha.
Maduhu amedai kuwa taarifa ya ofisa Magereza kuna washtakiwa wameenda kutibiwa, haijulikani ni washtakiwa wangapi? lakini hawajui wameenda kutibiwa wapi?
“Tunaomba Mheshimiwa hakimu uende kutembelea Gereza la Mahabusu Segerea ili iwaone washtakiwa hawa na ujue hali zao, na utoe amri kwa mkuu wa gereza hilo litimize wajibu wake wa kufahamu washtakiwa waliopelekwa kutibiwa ni wangapi” amesema.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, hakimu Beda aliuliza upande wa mashtaka, upelelezi umefikia hatua gani? Nao walijibu kuwa bado upo katika hatua ya upelelezi.
Kuhusu washtakiwa kwenda kutibiwa na kushindwa kutokea katika mtandao wa Mahakama, hakimu Beda alielekeza ofisa huyo wa Magereza Sajenti Hosea John afuatilie na kujua idadi ya washtakiwa waliopelekwa hospitali na kisha ampe majibu.
Kuhusu kesi hiyo kufutwa, hakimu Nyaki amesema hana Mamlaka yoyote kikatiba wala kisheria kufanya chochote katika kesi hiyo kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza isipokuwa katika hatua ya ukabidhi, yaani usikilizwaji wa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings).
Baada ya kueleza hayo, hakimu Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wanaweza kuletwa mahakamani au kesi hiyo ikasikilizwa kwa njia ya mtandao.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Omary Salimu, Tulizan Said, Haji Mlacha, Mgaya Athuman, Wilbaad Kivuyo na wenzao 33 ambao wanakabiliwa na mashtaka mawili kula njama na uhaini.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 ndani ya Jamhuri ya Tanzania walikula njama ya kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la uhaini, washtakiwa walidai kuwa washtakiwa hao Oktoba 29, wakiwa katika maeneo mbalimbali Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Wakati huohuo, kesi ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26387 ya mwaka 2025 yenye jumla ya washtakiwa 94 imetajwa mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato alidai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo ameomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 25, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wanaendelea kusalia rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Paulina Palangyo (28) mfanyabiashara, Mkazi wa Mbezi na wenzake 93.
Awali kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 76 lakini wiki iliyopitwa Jamhuri ilifanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na kuongeza washtakiwa 18 na kufanya idadi ya washtakiwa 94.
Katika hatua nyingine, kesi ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26540 inayowakabili washtakiwa 95 imetajwa mbele ya Hakimu Mushi na upande wa mashtaka umedai kuwa bado unaendelea na uchunguzi.
Kutokana na hali hiyo, hakimu Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wanaendelea kusalia rumande kutokana kesi inayowakabili haina dhamana.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Haruna Mwaisumbe, Abbas Mfinanga, Abdallah Kashinje, Frank Kinduka, Kulwa Nguma na wenzake 90.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Novemba 7, 2025 na kusomewa kesi ya kula njama na uhaini.
