Wakati Watanzania wakiendelea kutafakari yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito wa kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa ili amani iendelee kutawala hapa nchini.
Siku hiyo, yaliibuka maandamano yaliyotawaliwa na vurugu ambapo waandamanaji hao walikabiliana na vikosi vya ulinzi na usalama, jambo lililosababisha vifo vya vijana katika maeneo mbalimbali nchini.
Maandamano hayo yaliyozua vurugu, yalianzia Dar es Salaam na baadaye kuenea katika mikoa kama Arusha, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma na Songwe, yalisababisha taharuki na madhara katika miji mikubwa na kuzua hofu na usumbufu wa shughuli za kila siku.
Tukio hilo ni la kwanza kushuhudiwa nchini hasa Tanzania Bara kwa sababu nyakati za uchaguzi zimekuwa zikipita salama tangu mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa.
Mwaka huu, ukiwa ni uchaguzi wa sababu, hali imekuwa tofauti ambapo zilizuka vurugu na kusababisha mgawanyiko wa watu katika taifa, jambo linalosababisha hofu miongoni mwa wananchi hao.
Kutokana na sintofahamu hiyo, makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwamo viongozi wa dini, wamejitokeza kulaani kilichotokea huku wakihimiza uwajibikaji kwa waliohusika pamoja na kuunda na kuhimiza maridhiano ya kitaifa.
Novemba 14, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa mshindi wa uchaguzi huo, alilihutubia Bunge la 13 ambapo alisisitiza umuhimu wa kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa.
“Watanzania kwa mamilioni walijitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi waliowataka. Kazi iliyo mbele yetu sasa ni kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, ili sote kwa pamoja tuijenge, tuitunze na tuilinde nchi yetu, na kuzidi kunyanyua hadhi ya Taifa letu,” alisema Rais Samia.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisisitiza kwamba wanapozungumzia umoja wa Kitaifa wanaongozwa na uwepo wa Tunu ya Muungano.
“Hivyo basi, kuudumisha kuimarisha na kuuenzi Muungano wetu kutaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali tunayoiunda. Tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha tunatatua changamoto za Muungano kila zinapojitokeza,” alisema Rais Samia.
Wito huo wa mkuu wa nchi, siyo tu unaonyesha kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwa wananchi, bali pia unaonyesha haja ya kujenga nchi kwa pamoja na kumaliza tofauti zilizopo ikiwamo za kiitikati, tofauti za kiuchumi na ukosefu wa ajira kwa vijana wengi.
Kutokana na wito wa kiongozi huyo, wachambuzi wa siasa nchini wamejadili namna ya kujenga umoja na mshikamano wa Watanzania katikati ya mgawanyiko uliopo sasa huku wakishauri mambo ya kufanya ili kufanikisha hilo.
Vilevile, wanaonya kwamba umoja wa kitaifa utaimarika kama kutakuwa na haki katika uendeshaji wa siasa za hapa nchini na kujenga usawa miongoni mwa wanajamii ili kila mmoja ajihisi ni sehemu ya raia wa taifa hili.
Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame anasema ili kufikia hatua hiyo, Serikali inatakiwa kuweka mkazo katika kukemea na kuondoa migawanyiko ya kikabila, kidini na kikanda.
Anasema wananchi wapaswa kuelimishwa kuhusu madhara ya ubaguzi na kuchochea mshikamano ili kufikia lengo hilo.
“Itawezekana kufikiwa hatua hiyo ikiwa yatawekwa mbele maslahi ya taifa kuliko ya mtu binafsi au kikundi kwani umoja wa kitaifa hujengwa pale watu wanakubaliana juu ya mambo yenye faida kwa nchi nzima,” anaongeza.
Profesa Makame anasisitiza kuwa ili kuwa na jamii yenye mshikamano na utulivu viongozi wa kisiasa na kijamii wanapaswa kuonyesha mfano wa kuweka mbele maslahi ya taifa ikiwamo kukuza elimu ya uraia na historia ya taifa kwa kuimarisha utambulisho wa kitaifa na kuondoa uhasama wa kihistoria.
“Kukuza mawasiliano ya heshima na maridhiano katika mijadala ya kitaifa, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, na majukwaa ya mijadala vinapaswa kuhimiza lugha ya staha, kusikilizana, na kutafuta suluhu badala ya kuchochea migogoro,” anasema.
Anaongeza kuwa kila raia ana nafasi ya kuchangia mafanikio haya kwa kutenda haki na kuonyesha heshima kwa wengine, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kitaifa na kukataa lugha na vitendo vya chuki au ubaguzi.
Nguvu ya vijana itambuliwe
Kwa upande wake, Mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Abel Kinyondo anasema ili Taifa lifikie mafanikio hayo lazima nguvu ya vijana itambuliwe na kutumika kwa maslahi ya Taifa.
Anasema idadi kubwa ya Watanzaia ni vijana, hivyo ili Taifa liungane na lipige hatua pamoja, lazima kundi la vijana lipatiwe misingi ya kiuchumi na kijamii.
“Ni bahati mbaya kuwa kundi kubwa la Watanzania ni vijana lakini viongozi kwa idadi kubwa huwa watu wazima na wazee. Ili Taifa liungane na kusonga mbele pamoja, lazima kundi hili litambuliwe na kushirikiishwa ipasavyo katika nafasi za uongozi ili lishiriki kutoa uamuzi yanayowahusu,” anasema.
Anabainisha kuwa Tanzania yenye amani, umoja na utulivu itafikiwa ikiwa kundi hilo litawezeshwa kiuchumi ikiwemo fursa za ajira na elimu ya kujitegemea.
Watu wazungumze, wasikilizwe
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Paul Loisulie anasema ili kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, jitihada za makusudi zinahitajika ikiwamo kutoa fursa kwa watu kuzungumza na kusikilizwa.
“Kwa maoni yangu, watu wapate nafasi ya kupumua ili watoe sumu iliyopo ndani mwao ikiwa msongo wa mawazo, chuki zilizojengeka na mengine yafananayo,” anasema, akiongeza kuwa hiyo itawezekana kwa kuruhusu taasisi za kiraia na hata za serikali.
Anasema: “Kama alivyofanya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kukaa na watu na kuwapa nafasi ya kujieleza, watu wakipumua hivyo watatoa sumu waliyoibeba na ikifanyika vizuri watarejea katika maisha ya kawaida,” anaongeza.
Pili, anasema kuwa uwajibikaji uonekane hasa kwenye vyombo ambavyo havikuweza kutumia taarifa za kiintelijensia kukadiria na kushauri kwa usahihi mamlaka za juu kuhusu maandamano yaliyotokea na kusababisha madhara makubwa yaliyoshihudiwa.
“Kuruhusu taasisi na asasi za kiraia ikiwamo vyama vya siasa ziwe imara ili iwe rahisi kuzitumia kufikia wananchi badala ya serikali kwenda moja kwa moja kwa wananchi,” anasema.
Anaona changamoto kubwa kuwa kwa sasa hivi suala hili limeenda mpaka ngazi ya chini kabisa (kwa wananchi wenyewe).
“Maridhiano ya Zanzibar ya mwaka 2010 na hata Kenya mwaka 2008 iliwezekana kwa urahisi kwa sababu ajenda ilikuwa imeshikiliwa na vyama vya siasa hasa viongozi,” anasema.
Serikali, wazazi wawajibike
Mwanadiplomasia mwandamizi, Balozi Benson Bana anasema Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua madhubuti kumaliza tatizo lililojitokeza na kufungua ukurasa mpya.
“Ili tuweze kufika huko, viongozi wetu wasiyatazame kisiasa haya yaliyotokea, bali wawasikilize vijana na kujibu madai yao.
“Hata hivyo, historia yetu kama Taifa inatubeba sana Tanzania, hakuna jambo linaloshindikana kupitia mazungumzo,” anasema.
Dk Bana anaonyesha kuwa ili Tanzania ya umoja, mshikamano inayosonga mbele pamoja ifikiwe, Serikali inatakiwa kuanza na hali iliyopo ili kuchora ramani ya kesho iliyo bora.
Balozi huyo mstaafu anawatwisha mzigo wazazi na walezi kuwa wanalo jukumu la kuhakikisha malezi wanayoyatoa kwa watoto wao yanazalisha vijana wenye uzalendo na maadili mema ili kuwa na Taifa la umoja, utu, uzalendo na mshikamano.
Kwake yeye, Taifa linaanza na malezi, bila malezi bora hata serikali ikiweka mkazo katika maeneo ya kiutendaji Taifa halitakuwa na jamii iliyostaarabika.
“Malezi ya vijana wetu, wazazi walee kwa kufuata misingi ya mila na desturi zetu ili vijana wakue katika maadili hayo. Pia, taasisi za kijamii na vyama vya siasa navyo vijikite katika kuandaa vijana wenye mapenzi mema na nchi yao,” anaongeza.
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Dk Ananilea Nkya anasisitiza uandikaji wa Katiba mpya itakayoweka misingi bora kwa jamii.
Anasema Serikali ikiwekeza kwenye Katiba bora ikaainisha yale yanayotakiwa kufanyika yakawekwa kisheria Tanzania yenye umoja na mshikamano itafikiwa.
“Jambo la msingi hapa ni moja tu, Katiba mpya. Bila Katiba mpya hakuna huo umoja na mshikamano hautawezekana,” anasema.
Yeye anaona kuwa Katiba mpya ndiyo itakayojenga msingi wa kufikiwa na kutekelezwa kwa mikakati na sera zitakazoweza kuifikisha nchi katika maono hayo ya Rais Samia.
“Yote yaliyotokea na kutufikisha hapa ni matokeo ya Katiba mbovu, hatuwezi kutoka hapa na kupiga hatua nyingine bila kupata Katiba mpya,” anasema.
Kwa mujibu wake, mikakati yote itakayochukuliwa ikiwamo maridhiano, haitaweza kulivusha Taifa kama haitapelekea kuandikwa kwa Katiba mpya ndani ya muda mfupi iwezekanavyo.
