Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema Wizara ya Fedha imebeba matumaini ya Serikali na wananchi katika kuhakikisha inatafuta fedha za kuendeleza ujenzi wa miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
Balozi Omar amesema hayo katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Wizara ya Fedha (Treasury Square), jijini Dodoma leo Jumatano Novemba 19, 2025 alipokuwa akizungumza na menejimenti na wafanyakazi wa wizara.
Balozi Omar aliyekuwa ameambatana na Naibu Mawaziri wake wawili, Mshamu Munde na Laurent Luswetula katika ofisi hizo, amesema wizara inatakiwa kuweka mikakati na mipango madhubuti ya kutafuta rasilimali za ndani kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha miradi mbalimbali pamoja na kuweka sera bora za fedha zitakazosaidia kuyawezesha makundi ya vijana kupata ajira.
Amesema kuwa Wizara ya Fedha ndio moyo wa Serikali kwa maendeleo ya nchi, hivyo menejimenti na wafanyakazi wote, wanapashwa kujipanga kikamilifu kuhakikisha fedha zinapatikana lakini pia kwa kuyasikiliza makundi yenye changamoto zinazokwaza ustawi wao wakati nchi ikianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hata hivyo, wachambuzi wanapendekeza Serikali igeukie mbinu za kubana matumizi ili kuwezesha nchi kujiendesha kwa rasilimali zake za ndani, bila kutegemea mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa.
Pendekezo hilo la wadau wa uchumi, linakuja ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan aoneshe shaka kwa Tanzania kupata mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa, kutokana na doa la vurugu wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.
Tukio la maandamano yaliyozaa vurugu hizo lilisababisha vifo vya baadhi ya wananchi, majeruhi, uharibifu wa mali na biashara za watu binafsi, huku baadhi ya miundombinu ya umma ikichomwa moto.
Kutokana na tukio hilo, taasisi za kimataifa ukiwamo Umoja wa Mataifa (UN), zimetoa wito wa kurejeshwa hali ya amani nchini, huku Jumuiya ya Madola ikituma ujumbe maalumu wa kufanya majadiliano ya maridhiano.
Akizungumzia hilo, Mtaalamu mwandamizi wa fedha na uchumi, Dk Victoria Mjema amesema bila kubadili mfumo wa usimamizi wa matumizi ya umma, hata mapato ya ndani yakiimarika bado yatapotea katika matumizi ambayo hayachochei ukuaji wa uchumi.
Amependekeza hatua nne ili kupunguza matumizi, ambazo ni kukagua upya bajeti za wizara, kupunguza safari za nje zisizo za lazima, kuweka ukomo wa matumizi ya vikao na kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma ili kuondoa gharama zisizo halisi.
Mtaalamu huyo, amesema nchi nyingi zilizoingia kwenye mifumo ya kujitegemea zilipunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa wastani wa asilimia 15 hadi 20 katika miaka ya kwanza, hatua ambayo hupunguza shinikizo la kukopa.
“Kubana matumizi si hatua ya kukata matumizi kiholela, bali ni kuchagua yale yenye athari ya moja kwa moja kwa ustawi wa watu. Serikali ipime thamani ya kila shilingi inayotumika, kabla fedha haijatoka,” amesema Dk Mjema.
Pia, amesema taasisi nyingi huingia kwenye matumizi makubwa kwa sababu hazifanyi tathmini ya gharama na faida na mara nyingi bajeti za mwaka hutengenezwa bila uhalisia wa mapato.
Amesema ni wakati wa Serikali kuanzisha utaratibu thabiti wa kuoanisha matumizi na matokeo. Mathalan, fedha zinazopelekwa kwenye miradi ya maji zipimwe kwa kiwango cha upatikanaji wa maji, sio kwa kiasi tu kilichotolewa.
“Kama matumizi hayabadilishi maisha ya watu, basi hayastahili kuwa kwenye bajeti ya kipindi kigumu kama hiki,” amesema Dk Mjema.
Mchumi mwandamizi kutoka moja ya taasisi za umma aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema kubana matumizi ya Serikali kunahitaji pia kukomesha marudio ya majukumu ndani ya taasisi za umma.
Amesema kwa miaka mingi, kumekuwa na tabia ya kuanzisha vitengo, taasisi au mashirika mapya bila kufanya tathmini kama kazi hizo tayari zinafanywa na taasisi zilizopo.
“Hatua hiyo inasababisha kupanuka kwa bajeti ya mishahara na uendeshaji huku tija ikiwa ndogo,” amesema mchumi huyo.
Mchumi huyo ameshauri Serikali kupunguza ukubwa wa mashirika yasiyo na tija, kuyaunganisha mengine na kupunguza safari za ndani zinazoweza kushughulikiwa kwa njia ya Tehama.
Amesema matumizi ya Tehama kwenye mawasiliano, uchanganuzi wa taarifa na ufuatiliaji wa miradi, yanaweza kupunguza gharama kwa hadi asilimia 30 katika baadhi ya maeneo ya uendeshaji.
Ameambatanisha pendekezo hilo na kile alichoeleza, kwa kuwa kuna wizara zenye mawaziri 27 na naibu mawaziri zaidi ya 30, ni vema zingepunguzwa na kubaki angalau 15.
“Sio zipunguzwe kwa maana ya kuondolewa, hapana. Ziunganishwe ili kupunguza bajeti za mawaziri, badala yake waziri mmoja awe na jukumu la kusimamia wizara yenye idara kadhaa,” amesema.
Mtaalamu wa Uchumi na Maendeleo, Profesa Michael Mlambiti amesema kubana matumizi yasiyo ya lazima kutakuwa na maana ikiwa Serikali itaendeleza nidhamu kwenye mikataba ya ujenzi na miradi mikubwa.
Ameeleza moja ya sababu zinazofanya baadhi ya nchi kuingia kwenye madeni makubwa si wingi wa miradi, bali gharama zake ambazo mara nyingi hupanda kutokana na ucheleweshaji, marekebisho ya mikataba au uchaguzi wa makandarasi wasiokuwa na uwezo.
Profesa Mlambiti amependekeza kila mradi uwe na mfumo wa kudhibiti gharama, ukaguzi wa mara kwa mara na adhabu kali kwa makandarasi wanaoleta hasara.
“Naamini kama Serikali itasimamia nidhamu ya gharama kikamilifu, inaweza kuokoa mabilioni ambayo kwa sasa hupotea katika mianya ya utekelezaji,” amesema Profesa Mlambiti.
Vyanzo vya mapato viongezwe
Mchumi mwandamizi, Dk Jessemiah Mvungi amesema changamoto hiyo, inaipa Serikali nafasi ya kuimarisha udhibiti wa mapato ya ndani na kuzifanya rasilimali zilizopo kuwa msingi wa kutengeneza fedha nyingi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Amesema mfumo bora wa mapato ya ndani ni uti wa mgongo wa kujitegemea.
Dk Mvungi amesema miaka ya karibuni kumeibuka hoja kwamba uwezo wa kukusanya kodi unaongezeka, lakini bado uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa uko chini ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika Mashariki.
Ameshauri Serikali kuongeza ubunifu katika vyanzo vya mapato bila kupandisha kodi kiholela.
Dk Mvungi ametaka Serikali iongeze wigo wa walipa kodi, irahisishe ulipaji, iongeze matumizi ya Tehama na ipunguze mianya ya ukwepaji kodi inayoikosesha Serikali mabilioni kila mwaka.
Hata hivyo, Dk Mvungi ameonya kukusanya kodi bila kuzingatia hali ya biashara ndogo, wafanyabiashara wadogo na uzalishaji wa ndani kunaweza kuathiri mzunguko wa uchumi.
Kulidhibiti hilo, amesema sera za kodi lazima zizingatie uwezo halisi wa walipa kodi ili uchumi uendelee kupumua.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Baraka Loy amesema tatizo la utegemezi wa mikopo ya nje si tu ukosefu wa fedha, bali ni uamuzi wa kipaumbele cha mwelekeo wa uwekezaji.
Loy amesema Serikali ikitekeleza miradi yenye matokeo ya haraka hasa kwenye kilimo, viwanda vidogo, uzalishaji wa umeme, usafirishaji na uchumi wa dijitali, itaongeza pato kwa kipindi kifupi na kutoa nafasi ya kufadhili miradi ya muda mrefu.
Loy amesema miradi mikubwa kama reli, bandari na nishati ni muhimu kwa uchumi wa muda mrefu, lakini inahitaji fedha nyingi na matokeo yake huchelewa kuonekana.
Katika mazingira ambayo mikopo ya nje inaweza kupungua, alishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye miradi inayozalisha mapato ndani ya miezi 12 hadi 36.
Amefafanua kuwa, ikiwa Serikali itaongeza uzalishaji wa kilimo cha biashara, kupanua skimu za umwagiliaji, kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa maliasili kama gesi na madini, itatengeneza mapato ya mara kwa mara yatakayosaidia kukamilisha miradi mikubwa bila kushindwa kulipa gharama za kila siku.
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dickson Mwanga amesema Serikali inapaswa kutengeneza mazingira rafiki zaidi kupunguza urasimu, kuboresha mikataba na kutoa motisha kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Amesema sekta binafsi inaweza kugharimia hadi asilimia 40 ya miradi ambayo kwa sasa Serikali inabeba peke yake.
Mwanga amesema nchi nyingi zenye uchumi unaokua kwa kasi, kama Rwanda na Ethiopia, zimetumia sekta binafsi kupunguza mzigo wa Serikali katika miundombinu, nishati, teknolojia na huduma za jamii.
Mwanga amesema ukopaji wa ndani si tatizo kama ukifanyika kwa nidhamu na kwa kiasi kinachoweza kustahimiliwa na soko.
Amefafanua kuwa, kukopa kupita kiasi ndani kunaweza kushindana na sekta binafsi katika kupata fedha benki, hivyo kupunguza mikopo kwa wafanyabiashara na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Pia, amesema ukopaji uliopimwa vizuri, wenye riba nafuu na unaolenga miradi mahsusi yenye mapato unaweza kuwa chanzo kizuri cha fedha wakati mkopo wa nje ni mgumu kupatikana.
Ameshauri Serikali kuendelea kupanua soko la dhamana za muda mrefu ili kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara kutoka nje ambayo mara nyingi ina riba kubwa na masharti magumu.
Ameshauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye maeneo yanayozalisha ajira kwa wingi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii na biashara ndogondogo.
“Hii inamaanisha kutekeleza zaidi miradi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja sokoni, miundombinu ya minada, viwanda vya kusindika mazao ya wakulima, barabara za vijijini na mifumo ya masoko ambayo itawafanya wananchi kuona tija ya moja kwa moja ya uwekezaji wa Serikali,” amesema.
Pia, amesema taswira ya nchi hutengenezwa zaidi na namna inavyoshughulikia tofauti za kisiasa, uhuru wa maoni na ushiriki wa wananchi katika utoaji wa maoni kuhusu mustakabali wa nchi.
Amesema maridhiano ya kweli kati ya wadau wa siasa, Serikali, vyama vya upinzani na jamii ni msingi wa uthabiti wa uchumi.
“Bila utulivu wa kisiasa, nchi yoyote hupoteza uaminifu wa wawekezaji, kupuuziwa na taasisi za fedha na kuingia kwenye mzunguko wa ukosefu wa fedha kwa ajili ya maendeleo,” amesema.
