Simba Queens yaendeleza ubabe WPL

SIMBA Queens imeendeleza ubabe katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya kuitandika Bunda Queens mabao 3-0, mechi iliyopigwa leo Novemba 19, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.

Huo ni muendelezo baaada ya mechi ya raundi ya kwanza Simba Queens kupata ushindi kama huo uwanjani hapo dhidi ya Bilo Queens iliyopanda daraja msimu huu.

Simba Queens chini ya kocha msaidizi, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ilianza kupata bao dakika ya 37 kupitia Aisha Mnunka aliyemalizia pasi ya Fasila Adhiambo.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Bunda Queens ilijitahidi kuzuia mashambulizi ya Simba Queens na hadi dakika 45 zinakamilika, matokeo yalibaki bao 1-0.

Kipindi cha pili, Bunda Queens ilishindwa kuvumilia presha ya Wanamsimbazi hao wa kike na kujikuta inaruhusu bao la pili dakika ya 51 kupitia mshambuliaji Jentrix Shikangwa ambaye mechi iliyopita alifunga hat-trick.

Dakika 14 baadaye, Simba Queens ikaongeza bao la tatu kupitia kiungo kinda Elizabeth Mwiti aliyemalizia kwa kichwa kona iliyochongwa na Shikangwa.

Matokeo hayo yameifanya Simba Queens iendelee kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi sita na mabao sita.

Mechi nyingine iliyochezwa leo, Alliance Girls ya Mwanza ikiwa nyumbani Uwanja wa Nyamagana, imebakiza pointi tatu kwa kuichapa Ceasiaa Queens bao 1-0.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kutamatika, kocha mkuu wa Bunda Queens, Alley Ibrahim amesema walijaribu kuzuia kipindi cha kwanza lakini wachezaji walikosa kustahimili kipindi cha pili wakaruhusu mabao mawili.

“Tulifungwa kwa makosa binafsi na Simba Queens walikuwa bora kwa mabao ya setpieces (kutengwa), kipindi cha kwanza tulizuia vizuri lakini tulishindwa kustahimili, kipindi cha pili wakaja vingine tukaruhusu mabao mengine. Sababu nyingine wachezaji wanne wanafanya mitihani ya kidato cha nne na wengine saba hawana vibali,” amesema Ibrahim.

Kwa upande wa Mgosi, amesema Bunda Queens ilionyesha ushindani mkubwa lakini ilipambana hadi dakika 90 na kuondoka na pointi tatu.

“Bunda Queens inajua kufanya making (kujilinda) na ushindani ulikuwa mzuri, haikuwa mechi rahisi kwa sababu walikuwa wanahitaji pointi tatu na sisi tulikuwa tunazihitaji zaidi, tuliangalia kipindi cha kwanza kilikuwa na shida gani na kipindi cha pili tulibadilika tulishambulia sana tukapata mabao,” amesema Mgosi.