Dar es Salaam. Dereva wa bodaboda, Dominic Ezekiel na wenzake watano, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 29 yakiwemo ya kutakatisha Sh100 milioni, mali ya ubalozi wa China.
Mbali na Ezekiel, washtakiwa wengine ni Hassan Abdallah, James Nehemiah, Thomas Stiven, Guster Peter na Method Emanuel.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Novemba 19, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala amedai, washtakiwa walitenda makosa hayo tarehe tofauti kati ya Julai 2024 hadi Oktoba 15, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Kati ya mashtaka 29 yanayowakabili washtakiwa hao, mashtaka 22 ni ya kughushi risiti za mashine ya EFD, wakionesha kwamba ubalozi wa China umepokea viwango tofauti vya fedha, wakati wakijua si kweli.
Pia, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ya kuwasilisha risiti hizo za kughushi ubalozi wa China, wakati wakijua ni za uongo.
Washtakiwa pia wanakabiliwa na shtaka moja la utakatishaji fedha wanalodaiwa kutenda kati ya Julai 2024 hadi Oktoba, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Makakala amedai washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh100 milioni kutoka ubalozi wa China huku wakijua zilitokana na makosa tangulizi ya kughushi.
Baada ya kusomwa mashtaka, upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Nyaki ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
