KIKOSI cha Azam FC kimeondoka jana Jumatano kwenda DR Congo kuwahi mechi ya kwanza ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Maniema Union, huku mshambuliaji raia wa Congo anayekipiga timu hiyo ya Chamazi akivujisha faili la wenyeji mapema.
Jephte Kitambala, aliyewahi kuitumikia Maniema amefichua mbinu na ubora na udhaifu wa timu hiyo kwa waajiri wake wa sasa wakijiandaa kuvaana Jumapili kwenye Uwanja wa Martyrs, uliopo jijini Kinshasa kwa mechi ya kwanza ya Kundi B.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Azam msimu huu akitokea, Maniema, ndiye aliyetumiwa na kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge ambaye pia kiasili anatokea DR Congo katika video mbalimbali za kuwasoma wapinzani hao, kabla ya kikosi hicho kuianza safari hiyo jana.
Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, aliliambia Mwanaspoti, Kitambala ndiye aliyekuwa anatumiwa zaidi na benchi la ufundi ili kuvujisha siri za wapinzani, kabla ya kukutana Jumapili.
“Ni mchezaji anayeifahamu vyema Maniema ndio maana anatumiwa kwa kutoa baadhi ya udhaifu na ubora wao na hata aina pia ya uchezaji licha ya kuzitazama mechi zao, ni mbinu muhimu kwetu ya kujua namna ya kupambana nao,” alisema mchezaji huyo.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na Mwanaspoti, kocha wa Azam, Florent Ibenge alisema licha ya yeye binafsi kuwajua pia wapinzani wao vizuri, sio mechi nyepesi kutokana na ushindani wa kundi hilo, hivyo ni lazima wacheze kwa tahadhari.
Azam iliyokuwa Kundi B katika Kombe la Shirikishoi Afrika sambamba na AS Maniema, Wydad Casablanca ya Morocco na Nairobi United ya Kenya, inamtegemea zaidi Kitambala kwenye eneo la ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo anayechezea kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kusajiliwa Agosti 10, 2025, akitokea Maniema, ameifungia mabao manne katika mechi za kufuzu hatua ya makundi Shirikisho msimu huu.
Azam iliyofika hatua ya makundi ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia yake, ilianza kwa kuitoa El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, kisha raundi ya pili kuwatoa mabaharia wa KMKM ya visiwani Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0.
Kwa upande wa Maniema, iliitoa Pamplemousses ya Mauritius kwa jumla ya mabao 4-3, kisha hatua iliyofuata ikaitoa Royal Leopards ya Eswatini kwa penalti 4-3, baada ya mechi baina ya miamba hiyo kuisha kwa sare ya kufungana jumla ya mabao 2-2.