TANZANIA YAWASILISHA MPANGO WA GRIDI YA TAIFA YA MAJI COP30

………………

Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha Mpango wa Gridi ya Taifa ya
Maji katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaofanyika jijini Belem nchini Brazil.
 

Gridi
ya Taifa ya Maji ni Mkakati wa Taifa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
katika kuhakikisha kunakuwa na huduma endelevu ya maji kwa jamii, viwanda,
kilimo, mifugo na mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 

Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa wasilisho hilo, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya
Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema 

mpango
huo wa gridi ya taifa ya maji utasaidia kutatua changamoto kwa kuwa na vyanzo
vya uhakika vya Maji kutoka Maziwa Makuu na mito mikubwa.
 

Amebainisha
kuwa Tanzania ni kinara wa ajenda ya maji Afrika kupitia uwekezaji wa miradi
mikubwa ya maji ambayo inatekelezwa na Serikali ili kukabiliana na uhaba wa
huduma hiyo muhimu kwa binadamu.
 

Akiendelea
kuzungumza, Bw. Mitawi alisema kuwa pamoja na mambo mbalimbali gridi ya taifa
ya maji itasaidia katika kuwezesha ukuaji wa uchumi na huduma za maji kuwa
endelevu na uhakika.
 

Aidha,
Naibu Katibu Mkuu Mitawi alisema kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha
washirika wa maendeleo kutoka sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha
maandalizi ya gridi ya taifa ya maji yanachukua nafasi yake na kukamilisha
mpango huo muhimu.

Kwa
mantiki hiyo alisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja ni kulinda vyanzo vya maji
yakiwemo maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyka pamoja na mito ili kuhakikisha
usalama wa maji unakuwa endelevu kwa wakati wote.
 

Alitumia
nafasi hiyo kuwashukuru washirika wa maendeleo kama Shirika la kimataifa la
WaterAid, NDC Partners na Shrika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) kwa
kushiriki katika jitihada za Serikali za kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa
upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania Bi. Manka Mushi
alisema shirika hilo gridi ya taifa ya maji inaakisi mikakati ya Serikali ya
kutatua changamoto ya upungufu wa maji.
 

Hivyo,
alibainisha kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika si tu unatatua changamoto ya
upatikanaji wa huduma hiyo wa uhakika bali sekta mbalimbali zikiwemo kilimo,
uvuvi, nishati, viwanda, afya na elimu.
 

Bi.
Manka alipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kuja
na mpango wa kuamzisha gridi ya taifa ya maji ambayo itatatua changamoto ya
uhaba wa upatikanaji wa huduma hiyo.
 

Itakumbukwa
kuwa Machi 22, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza ianzishwe Gridi ya Taifa Maji ili maji
yaweze kufika katika maeneo yote nchini.Aidha, wakati akifungua Bunge la 13
amesisitiza utekelezaji wa Gridi ya Maji ya Taifa kukamilika ifikapo Mwaka
2030.