UCHAMBUZI WA MALOTO: Maswali 10 tata muundo Baraza jipya la Mawaziri

Rais Samia Suluhu Hassan anaanza uongozi wa muhula mpya, bila yeyote miongoni mwa wasaidizi wake watatu wa juu, aliofanya nao kazi kipindi chake cha kwanza kilichofikia tamati Novemba 3, 2025.

Dk Philip Mpango, Kassim Majaliwa na Dk Doto Biteko, walikuwa wasaidizi wakuu wa Rais Samia katika muhula wake wa kwanza. Dk Mpango (Makamu wa Rais), Majaliwa (Waziri Mkuu), Biteko (Naibu Waziri Mkuu). Wote hao hawamo ndani ya muundo wa Serikali mpya inayoendelea kuundwa na Rais Samia.

Alianza Mpango, kwa kutotajwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia, Januari 19, 2025. Akafuata Majaliwa, aliyetangaza kutogombea ubunge.

Kiufupi, kwa mujibu wa Katiba, ibara ya 51 (2), Majaliwa kutogombea ubunge tafsiri yake ilikuwa kutoutaka uwaziri mkuu katika muhula mpya wa Rais Samia.

Dk Biteko, kiongozi kijana, aliyetabiriwa na wengi kwa nafasi ya kwanza kwamba angekuwa Waziri Mkuu, baada ya Majaliwa, inawezekana ndiye ametengeneza mshangao mkubwa zaidi, na kujenga viulizo, kwamba nini kimetokea hadi asijumuishwe kabisa kwenye Baraza la Mawaziri?

Swali kuhusu Dk Biteko linatokana na unyeti wa nafasi aliyoshika. Aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa tatu kushika cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Hii ni baada ya Dk Salim Ahmed Salim na Augustino Mrema, ndiyo pekee waliowahi kuwa manaibu waziri mkuu kabla ya Biteko, na wote hao ilikuwa wakati wa Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Mwaka 1994, ilikuwa mara ya mwisho Tanzania kuwa na Naibu Waziri Mkuu, Mrema alipovuliwa cheo hicho na Rais Mwinyi. Miaka 29 baadaye, Septemba Mosi, 2023, Dk Biteko alikalia kiti hicho. Dhahiri, ilionekana Rais Samia alikuwa na imani kubwa na Biteko. Swali tata ni je, kipi kimetokea hadi imani yote ya Rais Samia kwa Biteko ikayeyuka?

Maswali kuhusu Biteko, yanakaribisha pia viulizo kuhusu namna Rais Samia alivyomaliza muhula wake wa kwanza na anavyouanza mpya. Alifanyaje nao kazi mpaka asitamani kumbakisha yeyote miongoni mwa hao watatu? Yupo mtu anaamini kwamba kama Rais Samia angemtaka Mpango au Majaliwa, asingeshindwa kumshawishi abaki.

Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, aliwaachia zawadi Watanzania, na ulimwengu wa wasoma vitabu, aliposimulia maisha yake ndani ya kitabu chake, My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu.) Katika kitabu hicho, Mkapa ameandika kuwa mara alipokula kiapo kuwa Rais wa Tanzania, Novemba 1995, alimfuata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ampe mapendekezo ya majina ili awateue kwenye Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa Mkapa, Mwalimu Nyerere alimjibu: “Ben, mawaziri watafanya kazi na wewe, kwa hiyo wewe ndiye unapaswa kuteua unaowaona watakufaa.”

Kutoka kwa Mkapa hadi Samia, mwongozo wa Mwalimu Nyerere ni hai, Rais aliye madarakani anapaswa kuteua mawaziri ambao yeye anaona watamfaa kutimiza malengo yake ndani ya muhula wa miaka mitano.

Kwa mantiki hiyo, Rais Samia ndiye mwenye dhima ya uteuzi wa mawaziri, maana wanakwenda kufanya kazi chini yake.

Rais hapaswi kuteua mtu ambaye haendani naye kiutendaji. Maana, mwisho kabisa, tathmini itakapofanywa na kuonekana Rais Samia kipindi chake matokeo chanya yalikuwa kidogo, hataeleweka akisingizia kukwamishwa na mawaziri. Rais hapaswi kupangiwa mawaziri.

Kingine, Mkapa ameandika kwenye kitabu chake kuwa licha ya Mwalimu Nyerere kukataa kumpa majina ya kuwateua kuwa mawaziri, lakini alimuusia katika uteuzi wake azingatie mzani wa kiimani, kwamba Serikali haina dini lakini Watanzania wana dini.

Alishauri uwepo mzani kwenye Baraza la Mawaziri baina ya Waislam na Wakristo, vilevile kutambua Tanzania ni dola ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Uteuzi wa Rais Samia, umekidhi mwongozo wa Mwalimu Nyerere. Katika Baraza jipya lenye wizara 27, mwaziri 27 na naibu mawaziri 30, Rais Samia amejitahidi kuweka uwiano wa dini, vilevile Muungano umezingatiwa kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na uwiano huo, bado maswali yanaendelea kuhusu aina ya mawaziri aliowaacha nje ya Baraza la Mawaziri. Innocent Bashungwa, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Jenista Mhagama, Waziri wa Afya, Selemani Jafo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Pindi Chana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Damas Ndumbaro, Waziri wa Sheria na Katiba, vilevile Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo. Kila mmoja miongoni mwa mawaziri hao wa Baraza la Mawaziri lililopita, anatengeneza swali la peke yake. Je, nini kimemsibu? Muunganiko gani umekosekana baina yake na Rais Samia? Alifanya nini mpaka aonekane hatoshi katika Baraza jipya?

Mawaziri hao wa zamani sita, ni maswali zaidi ya sita. Dk Biteko ni swali la saba. Ukiongeza kwamba Dk Biteko hakuwa tu Naibu Waziri Mkuu, bali pia Waziri wa Nishati.

Hapo Biteko anatengeneza swali la nane, je, hakutosha unaibu waziri mkuu au uwaziri mkuu, hata uwaziri wa kawaida hafai? Kuna nini nyuma yake? Kuanza muhula mpya na wasaidizi wakuu wapya, akiwa amewaweka kando watatu aliofanya nao kazi kwa ukaribu kipindi kilichopita ni swali la tisa.

Swali la 10 ni Rais Samia kuanzisha wizara mpya ya vijana, waziri akiwa mtu mpya, siyo tu kwenye Baraza la Mawaziri, bali pia bungeni na kisiasa.

Joel Nanauka, ndiye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana. Nanauka ambaye ni mwanasiasa mpya, anahitaji kujifunza uendeshaji wa serikali. Kitendo cha kumpa wizara mpya, naye akiwa mpya, inaweza kusababisha muundo wa wizara peke uchukue muda mrefu.

Katika muhula uliopita wa Rais Samia, alionekana kupata wakati mgumu kwenye wizara mbili, Wizara ya Viwanda na Biashara, vilevile Wizara ya Uwekezaji. Mawaziri wa wizara hizo walikuwa Geofrey Mwambi na Profesa Kitila Mkumbo, ambao wote walikuwa wapya kwenye Baraza la Mawaziri.

Baadaye, ilimlazimu Rais Samia kuwapumzisha wote wawili na kuifuta Wizara ya Uwekezaji. Hata hivyo, baadaye, Rais Samia aliiunda upya Wizara Uwekezaji kuwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, kisha akamteua Profesa Kitila kuiongoza.

Uteuzi mpya wa Baraza la Mawaziri, unafanya kikao chake cha kwanza, Rais Samia atakuwa mwenyekiti, sura nyingi zikiwa mpya.

Sura 10 alizomaliza nazo Baraza la Mawaziri lililopita, hatakutana nazo; Dk Mpango, Majaliwa, Biteko, Mhagama, Bashungwa, Bashe, Chana, Ndumaro, Jafo na Stegomena Tax, ambaye hakugombea ubunge, wala hakuteuliwa katika nafasi 10 za Rais.

Pamoja na ukweli kuwa mawaziri wanakwenda kufanya kazi na anayewateua, kwa hiyo lazima wakidhi matakwa ya mteuaji, jambo la msingi kuzingatia ni kwamba uteuzi wa Baraza la Mawaziri ni hesabu ambayo huhitaji vikokotoo vya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Nyakati za misuguano ya kisiasa, Rais hupaswa kuteua mawaziri ambao watakuwa na nguvu ya kuwezesha kumaliza misuguano.