Taifa la Tanzania linamomonyolewa. Mmomonyoko ni mkubwa. Nchi inagawika pande mbili. Wanaoshutumu, wanaolalamika, wanaotukana na wanaochukizwa na uongozi uliopo madarakani, dhidi ya wanaotetea, wanaosifu na wanaoona kila kitu kinakwenda vizuri.
Nani wa kuwaweka Watanzania pamoja? Tanzania imekuwa sawa na ile nyumba, wazazi hawapo, wamebaki watoto wasiosikilizana. La mwenzake, liwe jema au baya, hataki kusikia, kuelewa wala kukubali. Nyumba ya aina hiyo ni mbaya na hatari kupita kiasi.
Viongozi wa dini wamechagua kuwa sehemu ya mgawanyiko. Jamii moja ya kidini ipo upande mmoja wa shilingi, nyingine inatetea.
Dhahiri, majaribu ya kuligawa taifa ni makubwa. Hatari inaonekana waziwazi, watu wamefumba macho na masikio wameweka nta.
Mayowe ya kuiomba Tanganyika yamekuwa mengi. Ajabu, wanaoomba Tanganyika, wote wamezaliwa nchi ikiwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hiyo Tanganyika wanaijulia wapi? Bila shaka, ni hadithi ya kufuata mkumbo. Katika somo la saikolojia, inaitwa “The Bandwagon Effect.”
Kuweka sawia muktadha, bandwagon effect ni ile hali ambayo watu wanafanya jambo fulani kwa sababu wengine wanafanya. Unakuta watu wanavamia tabia fulani, mitindo, au hulka, kwa sababu wanaona kila mtu yupo hivyo.
Kwa ufasaha, bandwagon effect ni mwenendo wa watu kufanya yale ambayo wengine wanafanya ili waonekane wanakwenda na wakati.
Yaani kuendana na upepo wa mambo. Shauku ya kuwa sehemu ya kundi kubwa na kupata umaarufu, husababisha watu kuiga kwa kufuata mkumbo.
Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alikuwa na busara kubwa kutambua madhara ya mkumbo. Lincoln alimwandikia barua mwalimu wa mtoto wake. Alimweleza mwalimu kumfundisha mtoto wake namna ya kuwa mwanaume bora, mwenye kujiamini, mkweli, mwaminifu, msikivu na anayetambua fedha nzuri ile unavyoitafuta.
Miongoni mwa mengi ambayo Lincoln alimwandikia mwalimu wa mtoto wake, ni hili: “Try to give my son the strength not to follow the crowd when everyone getting on the bandwagon.” Tafasiri yake ni kuwa, jitahidi umpe mtoto wangu nguvu za kutofuata umati, pale kila mtu anapofuata mkumbo.”
Hatari ni hii; mkumbo unaweza kukufanya uuone uzuri wa nchi kuwa ubaya. Utamchukia mtu, kisa unaona watu wote wanamchukia.
Unaweza kumpenda asiyestahili kwa kuwa umeona ndiyo fasheni. Inatakiwa kujiamini na kuchanganua mambo, ndipo uamue.
Bandwagon effect, pia huitwa bandwagon fallacy. Huundwa kwa namna ya kuegemea imani za watu wa kawaida kabisa, au kuuangukia umma ili kila mtu aone kufanya kitu fulani ndiyo mwendo sahihi. Babdwagon fallacy husababisha watu kuona kitu fulani ni sahihi kwa kuwa kinaungwa mkono na kila mtu, na kina umaarufu mkubwa.
Kijana ambaye amezaliwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anapoamka na kudai Tanganyika, unajua bila shaka ni matokeo ya bandwagon fallacy. Kisa kila mtu anapaza sauti hiyo, inaonekana ndiyo sahihi kwa wote. Hii ni hatari kupita kiasi.
Tanzania hivi sasa ipo njiapanda. Muungano ni moja ya njia hatari. Pande nyingine za njiapanda ni udini, siasa chafu na ukabila. Hatari ya Muungano ni kuwa watu hawauheshimu. Wanajadili kama kitu ambacho unaweza kuamka asubuhi na kugawana mbao na fito, kila upande ujitegemee.
Muungano haujadiliwi kama tunu. Kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dola imara kwa sababu ni ushirikiano wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, zilizoamua kuwa taifa moja.
Muungano hauzungumzwi kwa namna kwamba Watanganyika na Wazanzibari ni imara kwa sababu ni Watanzania.
Mafundisho ya mitaala ya kijamaa shuleni, kwamba “umoja ni ngivu utengano ni udhaifu”, “kidole kimoja hakivunji chawa”, inaonekana yamegeuka maandiko ya kale.
Kelele za mkumbo wa mgawanyiko, ni kwa sababu vijana wa kizazi kipya hawajaelekezwa na kuelewa kuwa Tanganyika na Zanzibar ni imara kwa kuwa zimeunda Tanzania. Udini ni saratani inayoitafuna Tanzania. Vuguvugu za kudai Tanganyika, zilishakuwepo kipindi Rais wa Tanzania akiwa Ali Hassan Mwinyi.
Wakati huo, lilibuka kundi la wabunge waliojiita “G55”. Wabunge hao walitaka Tanganyika ndani ya Tanzania. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwakabili na kuwasambaratisha.
Mwalimu Nyerere alisema, ndani ya hoja za G55, kulikuwa harufu ya udini. Tanzania, Serikali haina dini, lakini Watanzania wana dini.
Ni mwiko kujadili mambo ya nchi kwa mgawanyo wa kidini. Mitandaoni hali ni mbaya. Watu wanasemana waziwazi kwa udini.
Makanisa yanatoa matamko hatari. Wapo wanatoa ubashiri mgumu, wanasema wameoteshwa kiongozi fulani anakufa na hafi. Ni maono ya uongo. Mashehe nao wanajibu mapigo.
Kwa nini viongozi wa dini hawakutani kwenye kamati ya kitaifa ya maridhiano ya kidini, na
kushauriana, ili kama kuna jambo la kushari nchi litolewe bila kutazamana dini ya anayekosoa na anayekosolewa?
Hatari zaidi ni kuwa nyakati hizi ambazo zinahitaji zaidi upatanisho. Viongozi wa dini wanatakiwa kutoa matamko ya kuleta watu pamoja.
Badala yake, wanachochea moto. Mpasuko unaongezeka. Mwafaka unakuwa mgumu kupatikana. Viongozi wa dini nao wanatekwa na bandwagon fallacy.
Siasa chafu ni njia ya tatu katika njiapanda hatari kwa nchi. Mchezo wa kupakana matope. Matokeo yake, wale ambao wangeweza kuwa wakombozi kipindi nchi ikiwa kwenye mgawanyiko, ndiyo ambao wananyimwa uhalali kwa sababu ya majina yao kupakwa masizi ya kisiasa. Uongo unaizingira siasa. Wasafi wanachafuliwa, wachafu wanatakaswa mithili ya malaika. Hatari kubwa zaidi, msako wa madaraka, unasababisha silaha iwe kuchafuana.
Kisha, watu bora wanaonekana hatari, halafu wasio na uwezo wanapata mwanya wa kupenya.
Ukabila ni janga la nne. Siku hizi kiongozi wa Tanzania anatazamwa kulingana na jamii anayotoka. Kabila lake wanamkumbatia na kuona uongozi ni wao.
Kiongozi akikosolewa, jamii nzima inaamka kana limekolewa kabila lao. Uongozi ukienda kwa jamii nyingine, kabila fulani linakuwa kama vile limepoteza madaraka, na lingine limepokea.
Zimeanza fununu kwamba inabidi uteuzi wa viongozi utazame namna ya kuziangukia jamii za makabila makubwa.
Hii siyo Tanzania ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Nchi imeingia njiapanda hatari. Inahitaji Mungu na jitihada za dhati kuinasua. Vinginevyo, wajukuu watarithi nchi iliyoharibika kabisa.
