Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika ufunguzi wa Bunge la 13, imebeba ujumbe mpana wa faraja, busara na dira ya kujenga taifa jipya linalosimama juu ya maridhiano na umoja.
Ni hotuba ambayo bila shaka imegusa mioyo ya Watanzania wengi, kwa sababu ya namna ilivyoanza kwa upole, ukimya wa kutafakari maumivu ya waliopoteza maisha na kauli za mama mwenye kutaka kuponya vidonda vilivyoachwa na uchaguzi.
Rais Samia alianza kwa kutoa pole kwa wote waliopoteza ndugu katika vurugu zilizoambatana na uchaguzi, akiwatakia pia majeruhi uponyaji wa haraka.
Dakika moja ya ukimya aliyoiomba kabla ya kuanza kuhutubia Bunge, ilikuwa ishara ya heshima kwa maisha ya kila Mtanzania.
Ni kitendo kilichoonyesha kwamba licha ya nafasi yake kama Mkuu wa Nchi, bado anachukua jukumu la kuwa mfariji na mleta matumaini kwa taifa lililopitia majanga.
Sehemu iliyoacha alama kubwa katika hotuba hiyo ni pale alipotangaza msamaha wa jumla kwa vijana waliokumbwa na mashtaka ya uhaini kwa kushiriki maandamano ya kupinga uchaguzi. Aliwaita ‘wanangu,’ neno linalobeba upendo, huruma na sauti ya mzazi anayejua uchungu wa kuzaa, lakini bado anaona haja ya kumpa mwana nafasi ya kujirekebisha.
Kwa mtazamo wake, vijana wengi waliingia kwenye maandamano wakifuata mkumbo bila kutambua madhara, hivyo adhabu pekee haiwezi kuwa suluhisho la kudumu.
Kwa kuizingatia hali hiyo, Rais Samia alimuelekeza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuchunguza kiwango cha makosa ya kila kijana na kuwaondolea mashtaka wale waliokutwa hawakudhamiria kufanya uhalifu.
Huu ni msingi muhimu wa kujenga upya imani kati ya wananchi na dola na hatua ya kuweka mbele haki pamoja na huruma. Kauli yake aliyoitoa kwa kunukuu Biblia Takatifu alisema: “Bwana uwasamehe kwa maana hawajui watendalo,” imefanya msamaha huu uwe na uzito wa kiroho na kimaadili.
Hotuba hii pia imeweka mwelekeo wa taifa kwa kipindi cha 2025/2030. Miongoni mwa mambo yaliyogusiwa ni mchakato wa katiba mpya, ambao Rais ameahidi kuuanza ndani ya siku 100 kwa kuunda tume ya usuluhishi na maelewano. Hii ni hatua mahsusi kwa taifa lililotengana kifikra na kihisia, kwani tume hiyo itajadili chanzo cha maandamano, matumizi ya nguvu yaliyopitiliza, na namna ya kuepusha migogoro ya aina hiyo siku zijazo.
Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa kudumisha Muungano na kuujenga kwa misingi ya haki na ushirikishwaji.
Ametoa mwito kwa wadau wote kushiriki katika safari ya maridhiano na kutafuta suluhu za kudumu kwa misingi ya mazungumzo, ukweli na uwajibikaji.
Aidha, amekiri kuwa demokrasia ni dhana pana inayotafsiriwa kwa mitazamo tofauti, hivyo Tanzania inapaswa kuijenga demokrasia yake kwa kuzingatia mila, desturi na tunu za taifa.
Kwa kutambua nafasi adhimu ya vijana, Rais ametangaza kuanzisha Wizara Maalumu ya Vijana pamoja na mshauri wa vijana Ikulu. Hatua hii inayo onyesha dhamira ya kuiweka nguvu kazi ya taifa katikati ya uamuzi wa nchi na kuifanya ifaidike moja kwa moja na sera za serikali.
Kwa ujumla, hotuba hii imekuwa jibu la wazi kwa mwito wa kutafuta kwanza uponyaji wa taifa kabla ya kutafuta chanzo cha mgogoro. Ni hotuba iliyosheheni busara, upendo na uongozi wa kutaka kuona Watanzania wanatembea pamoja katika misingi ya amani na umoja.
