Vurugu za uchaguzi zilivyotikisa kalenda, mipango ya vyuo vikuu

Dar es Salaam. Vurugu zilizotokea wakati wa  Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, zinaelezwa kuvuruga kwa kiasi kikubwa ratiba za masomo na mipango ya vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Hatua ya vurugu hizo zilizosababisha vyuo kusimama kwa muda zinaelezwa na viongozi wa taasisi hizo kuwa imeathiri mikakati ya muda mrefu ya vyuo, bajeti za uendeshaji na kuvuruga shughuli muhimu za kimasomo.

Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara (STeMMUCo), Gosso Mkubwa amesema jana kuwa  sintofahamu  iliyotokea iliwalazimu kufanya mabadiliko ya dharura katika ratiba ya taasisi.

“Tumejikuta tukiahirisha au kusogeza mbele matukio muhimu kama mahafali na pia tumelazimika kukutana upya ndani ili kurekebisha mikakati yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa hata mipangilio ya kawaida ya kitaaluma imeathirika, ikiwamo kupunguza mapumziko ya Aprili na kuwahisha mitihani ya memorandum, uamuzi aliosema ulikuwa wa lazima kutokana na mazingira ya wakati huo.

Kwa upande wake, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), kimeeleza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa huku mshauri wa wanafunzi, Dk Hassan Mohamed Issa akisema kilichotokea kimevunja utaratibu wa kitaaluma ambao wameuzoea kwa miaka mingi.

Kwa mfano, amesema hawakutarajia kuwapokea wanafunzi wa ngazi zote yaani stashahada, shahada na uzamili kwa wakati mmoja, jambo ambalo limeongeza mzigo wa kiutawala.

‘’Shughuli kubwa kama MUM Marathon, makongamano na mahafali ama yameahirishwa au yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa,’’ amesema.

Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo,  Hassan Yuda amesema baadhi ya shughuli zilizopangwa zimesitishwa kabisa.

“Kulikuwa na semina tulizopanga, lakini hazikuweza kufanyika kwa sababu wawezeshaji wameshapanga muda wao kulingana na ratiba ya awali,” amesema.

Athari hizo hazijaishia kwa taasisi pekee, kwani wanafunzi nao wamejikuta wakikabiliana na mazingira ya ukosefu wa utulivu wa kitaaluma.

Warda Salmini, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa udaktari wa mifugo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), amesema kukaa nyumbani kwa muda mrefu,  kumeathiri uwezo wa wanafunzi kujipanga.

“Siku za kusoma zitakuwa chache, hivyo kuna changamoto kukamilisha masomo yote,” amesema.

Kwa mujibu wa kalenda mpya iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Novemba 8, 2025 wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatakiwa kuripoti Novemba 17 kwa ajili ya utaratibu wa utangulizi, huku wanaoendelea wakirejea Novemba 24.

Maofisa wa wizara wanasema mabadiliko hayo yamesababishwa na ucheleweshaji uliotokana na vurugu za uchaguzi.

Waonya athari kuchukua muda mrefu

Wataalamu wa elimu wanatabiri kuwa athari hizo zinaweza kuendelea kwa muda mrefu, endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kurejesha mwenendo wa kitaaluma.

Dk Joyce Mwingira, mchambuzi wa elimu ya juu na mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema vyuo vinapaswa kuchukua hatua za haraka kufidia upungufu wa muda wa mawasiliano darasani.

“Mitikisiko kama hii huathiri maendeleo ya kozi na inaweza kusababisha upungufu wa kiuelewa kwa wanafunzi,” amesema na kushauri vyuo kuongeza vipindi vya  masomo, kuongeza muda wa matumizi ya maktaba na kuweka ratiba nyumbulifu za  mitihani.

Dk Mwingira ameonya pia kuwa athari za kihisia kwa wanafunzi hasa wale waliokuwa wakijiandaa kwa mitihani, hazipaswi kupuuzwa, kwani sintofahamu inaweza kuongeza msongo wa mawazo na kuathiri uwezo wao wa kurejea katika hali ya kusoma.

Athari za kifedha pia zimeibuka, hasa kwa vyuo binafsi vinavyoegemea zaidi mapato kwa  uendeshaji.

Mtaalamu wa mipango ya elimu, Dk Kelvin Mhando amesema mabadiliko ya kalenda husababisha gharama za ziada zisizopangwa, ikiwamo kupanga upya taratibu za lojistiki, kubadili mikataba ya huduma na kupanga upya majukumu ya watumishi.

“Kwa taasisi binafsi, hata mtikisiko mdogo unaweza kuyumbisha makadirio ya fedha ya mwaka mzima,” amesema.

Dk Mhando ametoa wito kwa Serikali na vyuo kuandaa mifumo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya muda mrefu, ili kulinda uthabiti wa kalenda za kitaaluma katika siku zijazo.