Wadau wataja ilikojificha tabasamu ya Watanzania

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali nchini wameeleza matarajio yao kwa Serikali kuhusu hatua wanazotamani kuona ikizichukua ili kujenga Taifa lenye furaha na kuwaletea wananchi tabasamu la kudumu.

Maoni hayo yanakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa kauli inayosisitiza dhamira yake “ya kuona Serikali anayoiongoza inakumbukwa kwa tabasamu litakalokuwepo kwenye nyuso za Watanzania.”

Kwa mujibu wa ripoti ya furaha duniani ya mwaka 2024, Tanzania ipo kwenye kundi la nchi 20 za mwisho, ikiwa namba 385. Imepata pointi 3.78 ikilinganishwa na Finland ambayo inashika usukani ikiwa na pointi 7.4 huku Afganistan ikishika mkia kwa pointi 1.72.

Ripoti hiyo ambayo hutolewa na taasisi Wellbeing Research Centre ya chuo Kikuu cha Oxford kwa kushirikiana na taasisi nyingine maarufu, huandaliwa kwa hutumia vigezo vya pato la taifa, huduma za jamii na muda wa kuishi kwa afya njema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia alisema anatamani Serikali yake ikumbukwe si tu kwa utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali, bali pia kwa kuleta faraja na furaha kwa Watanzania.

“Namwomba Mungu, Serikali nitakayoiongoza ikumbukwe si tu kwa mambo yatakayokuwa yamefanyika, lakini pia kwa tabasamu litakalokuwepo kwenye nyuso za Watanzania,” alisema Rais Samia.

Baada ya kauli hiyo, wadau kutoka makundi mbalimbali wameeleza mambo wanayoona ni muhimu kutekelezwa ili kufanikisha dhamira hiyo ya kuleta furaha.

Miongoni mwayo, wametaja ajira kwa vijana, utatuzi wa changamoto za jamii, usimamizi wa haki pamoja na uwajibikaji wa watendaji wa Serikali.

Mwananchiimezungumza na wadau kutoka taasisi za dini, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wachambuzi wa masuala ya kijamii, kila mmoja ametoa mtazamo unaoshabihiana kuhusu suala hilo.

Miongoni mwao, ni Askofu William Mwamalanga, mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Maaskofu na Mashehe ya Amani, Haki na Maadili, ambaye amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau, inapaswa kushughulikia malalamiko ya wananchi na kuimarisha utendaji unaozingatia haki na utu.

Mathalan, amesema kero zilizochangia vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi, zinapaswa kutatuliwa ili kurejesha utulivu wa fikra na kuondoa mgawanyiko uliopo miongoni mwa wananchi hivi sasa.

“Ili Watanzania waweze kupata tabasamu, ni lazima Serikali ishughulikie malalamiko yao. Kwanza imalize mgawanyiko uliotokana na yale yaliyojitokeza kwenye uchaguzi, kisha viongozi waongoze kwa uadilifu. Bila kufanya hivyo, hilo tabasamu halitapatikana,” amesema Askofu Mwamalanga.

Mtazamo wake unaungwa mkono na mdau wa haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya ambaye amesema makovu yaliyosababishwa na uchaguzi hayawezi kufubaa hadi pale yatakaposhughulikiwa kwa kina.

Amesema Watanzania wanatamani kupata Katiba mpya, hivyo hawataweza kupata furaha wanayoihitaji iwapo suala hilo halitashughulikiwa mapema ipasavyo.

“Ili jamii ipate furaha, ni lazima mahitaji yao ya msingi yatimizwe,” amesema Dk Nkya.

Viongozi wa kisiasa nao wameungana na mtazamo huo, kuwa uhitaji wa Katiba mpya ni msingi muhimu wa kuijenga furaha ya Taifa. Wamesema Watanzania hawawezi kupata tabasamu la kweli bila kupewa fursa ya kuandika Katiba itakayowawezesha kuamua namna wanavyotaka nchi yao iongozwe.

Kwa msingi huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), Rashid Rai amesema kauli ya Rais Samia kuhusu kuacha tabasamu kwa Watanzania inahitaji hatua za msingi, ikiwemo wananchi kuandika Katiba mpya itakayojengwa juu ya haki, utu na utawala bora.

Amesema Katiba yenye misingi hiyo ndiyo itakayozalisha amani, furaha na tabasamu linalotarajiwa.

“Watanzania hawawezi kupata tabasamu kama kunakuwa na malalamiko dhidi ya uchaguzi kila mara, lazima hali hii iondolewa kwa kutengeneza Katiba mpya ambayo wananchi wanaihitaji,” amesema.

Rai ameongeza kuwa tabasamu la wananchi litatimia piwa iwapo Serikali itaimarisha utendaji kazi wake, kuboresha huduma katika taasisi za umma, kudhibiti rushwa na kukomesha vitendo vya utekaji ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa nchini.

“Watu wanataka vyombo vya dola vitende haki kwa mujibu wa sheria, Bunge lisimame upande wa wananchi badala ya kuegemea serikalini na huduma za afya, maji na elimu viboreshwe. Haya ndiyo yatakayozalisha tabasamu hilo,” amesema.

Si hayo tu, uwajibikaji wa watendaji wa Serikali ni suala linaloibuliwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii kuwa ni la muhimu, wakisisitiza ukomeshaji wa uonevu, kusimamia haki na kusikiliza kero za wananchi, kama njia ya kufanikisha lengo la Rais Samia la kuacha tabasamu kwa Watanzania.

Chief Waihojo Mwambipile, mmoja wa wachambuzi hao, amesema kauli ya Rais ni yenye matumaini, lakini utekelezaji wake utakuwa mgumu kuamini ikiwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, rushwa, ufisadi na huduma duni za jamii vitaendelea.

Amesema Serikali inapaswa kuchukua hatua za vitendo zinazolenga kuboresha maisha ya watu badala ya kutoa ahadi pekee, ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kuwaongezea furaha.

“Kutoa tabasamu kwa Watanzania kunahitaji kutatua changamoto ya ajira kwa vijana ili waweze kujipatia kipato badala ya kuwaambia wajiajiri bila kuwa na mtaji. Pia Serikali isimamie ipasavyo fedha za umma ili kuondoa hofu kuwa zinapotea,” amesema.

Mwambipile amessisitiza kuwa tabasamu la Watanzania litatokana na kuwa na imani kwa mamlaka kuhusu usimamizi wa fedha za umma, fursa za ajira na utatuzi wa tuhuma za ufisadi zinapobainishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Serikali ikiwa mstari wa mbele katika kusikiliza na kutatua matatizo ya jamii, kushughulikia taarifa za ufisadi zinazoibuliwa, kuvutia uwekezaji utakaoongeza ajira na kusimamia haki na uhuru wa watu, tabasamu hilo litapatikana,” amesisitiza Mwambipile.

Mbali na makundi hayo, waendesha bodaboda, bajaji pamoja na wasanii nao wanayo mambo wanayotarajia kuyaona yakitekelezwa ili kuondoa msongo, kuleta amani na kuongeza furaha yao ndani ya jamii.

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji, Said Kagomba amesema kundi hilo litapata tabasamu endapo litapewa kipaumbele katika upatikanaji wa mikopo, hasa ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Amesema vijana wengi wanaojiajiri katika sekta ya usafirishaji wanahitaji mikopo ili kununua vifaa vya kazi na kujikimu kimaisha. “Tunashukuru kwa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana. Tunaomba tupatiwe mikopo yetu ya asilimia 10 mapema ili vijana wanunue vifaa vya kazi na waendelee kufanya shughuli zao,” amesema.

Ameongeza kuwa sekta ya bodaboda na bajaji imekuwa mkombozi mkubwa kwa vijana, kwa kuwa imewaajiri wengi, likiwamo kundi la wasomi wanaosubiri ajira za taaluma zao.

“Tunapongeza hatua zilizochukuliwa, lakini tunaomba Serikali ituunge mkono zaidi kwa kutupa mikopo kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba ameitaka Serikali kuangalia upya mitalaa ya elimu kwa kuongeza masomo ya uraia na ujuzi, ili kuwajengea vijana misingi ya uzalendo, umahiri na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa kwa ufanisi zaidi.