Dar/Dodoma. Baraza jipya la mawaziri lililoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan limeibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi, wakiwa na maoni tofauti kuhusu ufanisi, uwajibikaji na kasi ya utendaji katika mhula wa pili wa Serikali ya wamu ya sita.
Mitazamo na matarajio ya wananchi hayo, inatokana na mabadiliko yaliyopo kwenye baraza hilo lenye wizara 27.
Mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri ni pamoja na kuhamishwa kwa baadhi ya wizara katika Ofisi ya Rais, ya Waziri Mkuu na kubadilishwa kwa baadhi ya mawaziri.
Katika baraza hilo, Rais Samia amefanya mabadiliko kadhaa, wakati sura mpya zikiingia barazani wamo pia waliowekwa kando akiwamo Dk Doto Biteko, aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu.
Katikati ya hoja hizo za wananchi, Chama cha Mapindizi (CCM) kimetoa onya kwa mawaziri na naibu mawaziri watakaoshindwa kwenda na kasi ya utendaji wa Rais Samia kuwa, watawashughulikia.
Novemba 17, 2025, Rais Samia alitangaza baraza la mawaziri lenye mawaziri 27 na naibu mawaziri 29, huku akisema mabadiliko hayo yanalenga kuongeza weledi, kurekebisha mianya ya utendaji na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kauli hiyo imeongeza kiu ya Watanzania kuona tofauti katika utendaji na nidhamu ya uwajibikaji ndani ya Serikali.
Katika mabadiliko hayo, sura mpya zimepewa nafasi muhimu serikalini, baadhi ya vigogo wamebaki na wengine kubadilishwa wizara.
Mabadiliko mengine ni uteuzi wa Dk Rhimo Nyansaho ambaye sasa anaongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Joel Nanauka, waziri mpya wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana.
Katika maoni, vijana wengi wamekuwa na matumaini juu ya uteuzi huo wakisema ni ishara ya Serikali kuanza kusikiliza changamoto zao kuhusu ajira, ubunifu na fursa za kiuchumi.
Pia, baadhi ya wananchi wameonesha matumaini yao kwa kurejea kwa mawaziri wenye uzoefu akiwamo Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Jumaa Aweso (Maji), Profesa Makame Mbarawa (Uchukuzi) na Profesa Palamagamba Kabudi wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Wengi wanasema wanaamini uzoefu wao unaweza kuongeza uthabiti katika sekta zinazohitaji uimara wa kisera na usimamizi thabiti.
Wanasema kuwa, kutorejea kwa waliokuwa mawaziri waandamizi kutoka baraza lililopita, kumefungua mjadala mpana kuhusu mwelekeo mpya wa Serikali.
Hata hivyo, Rais Samia alisema hataona shida kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri, iwapo kutakuwepo na wateule watakaozitumia nafasi walizopewa kama fahari badala ya dhamana ya kuwatumikia wananchi.
“Mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua na kipindi fulani mlinisema kuwa nabadilisha sana. Na nilisema nabadilisha mpaka nipate yule atakayefanya kazi na mimi kwa moyo mmoja,” alisema.
Rais Samia alisema nafasi za uteuzi ni kupishana, ndiyo maana baadhi ya waliokuwepo hawapo sasa na kuna sura mpya zilizochanganyika na chache za zamani.
Walioachwa ambao walikuwapo kwenye baraza lililopita ni aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani), Jenista Mhagama (Afya), Dk Seleman Jafo (Viwanda na Biashara), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Dk Damas Ndumbaro wa Katiba na Sheria.
Pia, wapo wanaosema baraza jipya halitaweza kuleta mageuzi makubwa ya kijamii huku hofu yao ikijengwa na mambo tofauti yakiwamo ya utata uliojitokeza katika uchaguzi uliowaweka madarakani na hofu ya kukosa mikopo kutoka nje.
Mbali na maoni wanayotoa kupitia mijadala mbalimbali ikiwamo mitadao ya kijamii, Mwananchi imezungumza na baadhi ya wananchi akiwamo Janeth Mwambije, mkazi wa Kivule Dar es Salaam, aliyesema imani yake kwa baraza hilo ni kwamba, litajibu matamanio ya Watanzania.
“Matarajio yangu ni kuwa, baraza hilo watapambana kutimiza yale aliyoahidi Rais Samia kwenye kampeni zake maana ndiyo walioteuliwa kuyafanya,” amesema.
Amesema kutokana na wingi wa wabunge wa CCM, inaashiria walioteuliwa wamepatikana kwa vigezo vingi, hivyo watapigania vyema matamanio ya Watanzania.
“Naamini wamechunguzwa na kuonekana wanakidhi vigezo hivyo, ninatarajia kuwa watafanya kazi waliyoaminiwa kuifanya,” amesema.
Katika baraza hilo pia yapo mageuzi ya kimuundo ikiwamo kuanzishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana hatua inayotafsiriwa na wengi kama mbinu ya Serikali kuweka nguvu mpya kwenye kundi kubwa la vijana linalobeba kesho ya nchi.
Pius Lukanula kutoka Kishapu Shinyanga, amesema kwakuwa baraza limebeba vijana wengi, anatarajia kuona likiibua vipaji na fursa kwa vijana zaidi ya lile lililopita.
“Baraza jipya limebeba vijana kwa kiwango kikubwa, pia wizara mpya ya vijana, imeanzishwa, kama kijana ninaona ni baraza litakalojali vijana,” amesema.
Pia, amesema uteuzi wa wanasiasa wakongwe waliokuwa nje ya baraza lilipita akiwamo Dk Bashiru Kakurwa ni mkakati mzuri kwa kuwa, ukongwe wake na taaluma yake ya siasa unaonesha nia ya Rais kuwa na baraza la weledi na sifa za kitaaluma.
“Uwepo wa vijana wengi kwenye baraza inaonesha litakuwa baraza la kuchochea ubunifu na fikra mpya za vijana. Ukitazama baraza hili unaona mchanganyiko mzuri wa wakongwe na wapya pia vijana na wanawake hali inayoashiria baraza litagusa makundi yote,” amesema Lukanula.
Katika hatua nyingine, baraza hilo pia limekuja na mabadiliko, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iliyokuwa chini ya Ofisi ya Rais, sasa imerejeshwa tena kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayotajwa kuibua matarajio mapya ya uwajibikaji katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Wakati anatangaza mabadiliko hayo, Rais Samia alisema: “Tawala za mikoa ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, lakini kwa kuwa Waziri Mkuu ndiyo msimamizi wa shughuli zote za Serikali, tumeirudisha kwa Waziri Mkuu.”
Baadhi ya wananchi wameonesha imani yao kuwa, mabadiliko hayo yatasaidia kurahisisha uratibu wa Serikali, kupunguza urasimu na kusimamia kwa karibu watendaji wa chini wanaogusa maisha ya watu moja kwa moja.
Hata hivyo, wapo pia wanaoonesha shaka kuwa baraza hilo jipya halitaweza kujibu matamanio ya Watanzania.
Hofu yao inajengwa na shaka ya Serikali kukosa kuaminiwa na baadhi ya mataifa na taasisi za kimataifa na kunyimwa misaada na mikopo kutokana na sura mbaya ya nchi, kimataifa iliyotokana na machafuko yaliyosababishwa na ghasia za uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa uzoefu wa kuishi muda mrefu Tanzania, baraza lililoundwa ninaliona likienda kupitia wakati mgumu na halitaweza kusaidia wananchi ipasavyo kutokana na mambo kadhaa.
“Kwanza yaliyotokea kipindi cha uchaguzi kugubikwa na vurugu, pili Rais Samia alisema kutokana na vurugu hizo tunaweza kukosa uwezo wa kukopesheka, hivyo kukosa mikopo,” amesema Emmanuel Kasembo, mkazi wa Bagamoyo, mkoani Pwani.
Kasembo amesema hatua hiyo inaweza kuathiri uwezo wa baraza hilo kuhudumia wananchi ikiwa Serikali itakabiliwa na uhaba wa fedha za kutekeleza mipango mbalimbali ya Serikali.
“Uhaba wa fedha unaweza kusababisha Serikali kuanza kubuni kodi na tozo kwa wananchi ili kupata fedha za kuendeshea miradi, hali inayoweza kuongeza mzigo kwa wananchi, hivyo mimi sioni kama baraza hili litaweza kutimiza vyema matarajio ya Watanzania,” amesema.
Mbali na matarajio hayo ya wananchi wanaoonesha matumaini na shaka kwa baraza hilo, Duma Mgange kutoka Kondoa, mkoani Dodoma aliibua jambo jipya.
Licha ya kupongeza na kuonesha matumaini yake kwa baraza hilo jipya, Mgange aliibua hoja ya uwakilishi wa wazee bungeni, akitaja kuwa, kundi hilo halipewi kipaumbele sawa na makundi mengine.
“Wizara ya wazee ipo wapi, hata huko bungeni hatuoni mzee mwenye upaa akisimamia masuala ya wazee moja kwa moja,” amesema.
Mgange amesema wazee wanahitaji kuwa na wizara inayogusa kundi hilo moja kwa moja kama ilivyoanzishwa wizara maalumu ya vijana.
“Wanawake wanatetewa sana na tumeona vijana nao wakipiganiwa sana. Mfano wameahidiwa ajira milioni 8.5 na kuundiwa wizara maalumu lakini sisi wazee hatuoni anayetutetea,” amesema.
Maoni na matarajio hayo ya Watanzania yanayojaa imani na hofu yanaonesha uzito wa majukumu yaliyopo mbele ya mawaziri na manaibu mawaziri walioaminiwa na kuteuliwa katika baraza hilo.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi leo Jumatano Nobemba 19,2025 alikutana na waandishi wa habari katika Makao makuu ya CCM, ‘White House’ jijini Dodoma na kuwatahadharisha wateule wa Rais Samia kwamba, wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na viwango, vinginevyo wategemee kuchukuliwa hatua.
Kihongosi amesema waziri au naibu waziri ambaye hatatimiza wajibu wake kwa viwango na akasababisha kumuangusha Rais Samia, hawatavumiliwa.
Kihongosi amesema chama kinatarajia utendaji wa kiwango cha juu kutoka kwa viongozi walioteuliwa, akibainisha wengi wao ni wapya na wanapaswa kufahamu Rais hana mchezo katika kushughulikia masuala ya utendaji serikalini.
“Chama hakitasita kuchukua hatua kali kwa kiongozi yeyote atakayekuwa mzembe, wajue wana wajibu wa kuwatumikia Watanzania ili kutimiza ndoto za mkuu wa nchi,” amesema Kihongosi.
Pia, amesema hatua ya Rais Samia kuomba mamlaka husika kuwaachilia huru baadhi ya vijana waliokuwa wakishikiliwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, hivyo chama kinatarajia Serikali kusimamia ipasavyo ahadi hizo.
Amewataka wateuliwa wote wakafanye kazi na watendaji wa Serikali ili wahakikishe utekelezaji wa ahadi ya siku 100 uje na matokeo.
Pia, ameonya chama kitawachukulia hatua watendaji wote watakaoshindwa kutimiza wajibu wao au kuendeleza vitendo vya rushwa, akisema upimaji wa utendaji utafanyika na watakaobainika watawajibishwa mara moja.
Katika hatua nyingine, Kihongosi amempongeza Rais Samia kwa kuunda tume ya uchunguzi kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika matukio hayo, vurugu zilitokea mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita, Arusha, Mara na Ruvuma na kusababisha raia kuuawa, wengine kujeruhiwa huku mali za watu binafsi na miundombinu ya umma vikiharibiwa.
Tume hiyo yenye wajumbe saba inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Wajumbe walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.
Katika tume hiyo, pia yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Pia, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kurejesha amani inapopotea ni kazi kubwa na yenye gharama kwa Taifa.
