Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha kesi tatu zinazowakabili washtakiwa 79 wanaokabiliwa na makosa ya kula njama ya kutenda kosa na uhaini, kutokana na upelelezi wake kutokukamilika.
Aidha upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa unaendelea na upelelezi ili waweze kufanya uchambuzi kwa washtakiwa ambao watakutwa hawahusiki na tuhuma hizo waweze kuachiwa kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Leo Jumatano Novemba 19,2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Erasto Philly, kesi hizo zilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili watatu huku washtakiwa wote 79 wakiwakilishwa na jopo la Mawakili wanne wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Arusha, Khamisi Mkindi.
Kesi ya kwanza ilikuwa na washtakiwa 53 katika kesi namba 26512/2025 ambao wanakabiliwa na makosa mawili ambayo ni kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29,2025 walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.
Kosa la pili linalowakabili washtakiwa hao ni uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Katika kesi ya pili namba 26514/2025 ilikuwa na washtakiwa 21 ambao wameshtakiwa makosa mawili ikiwemo kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29,2025 walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.
Wakili wa Jamhuri aliieleza Mahakama kuwa kesi hizo zilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuiomba Mahakama hiyo kuzipangia tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kutokana na upelelezi wake kutokamilika.
Wakili Mkindi aliiomba Mahakama wapatiwe hati za mashtaka pamoja na kuomba kufahamu kuhusu uchambuzi ulioagizwa na mamlaka kufanywa ili wasiohusika na kesi hizo waachiwe na kurejea katika majukumu yao.
“Tunafahamu kwamba ofisi ya mashtaka iliyopo chini ya DPP ambayo ilipewa maelekezo na Rais wafanye uchambuzi wa watuhumiwa, tungependa kusikia uchambuzi huo umefikia hatua gani ili ambao hawahusiki kwa namna yoyote watoke mapema waendelee na shughuli zao,”alisema Wakili wa utetezi
Wakili wa Jamhuri aliieleza Mahakama kuwa wanaendelea kufanyia kazi maelekezo hayo kwa kuendelea na upelelezi ambao bado haujakamilika.
“Maelekezo ya Rais tumeyapata tunayafanyia kazi,upelelezi unaendelea haujakamilika hilo hata sisi tunaendelea nalo na tutakamilisha siku za karibuni ili ambao hawahusiki waachiwe,”amesema wakili wa Serikali
Kesi zote tatu zimeahirishwa hadi Desemba 3,2025 ambapo kesho Novemba 20,2025 washtakiwa wengine 112 akiwemo mwandishi wa habari wa mkoani Arusha, Godfrey Ng’omba watafikishwa mahakamani kwa ajili ya kesi zao kutajwa.
