Dar es Salaam. Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 na 30 mwaka huu, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa na mjadala huku wengine wakiipinga na wengine wakiunga mkono.
Vyama vya siasa vya ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeipinga na kukosoa uteuzi wa tume hiyo huku Ada Tadea na National League for Democracy (NLD) na mwanadiplomasia mwandamizi Balozi Benson Bana, wakiiunga mkono.
Pia, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume hiyo ya uchunguzi, huku kikiwataka walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
“Tunawaomba makamishna wa Tume waifanye kazi hiyo kwa masilahi mapana ya Taifa, uzalendo na uadilifu. Watoe majawabu yatakayaowezesha safari ya kuijenga Tanzania njema yenye maelewano, utulivu na usalama kwa wote,” amesema Kenani Kihongosi, katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.
Juzi, Rais Samia aliteua tume hiyo yenye wajumbe wanane, ikiongozwa na Jaji mstaafu Mohamed Othman Chande.
Wajumbe wengine wanaounda tume hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue pamoja na Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.
Pia, yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Hatua hiyo ya mkuu huyo wa nchi ni utekelezaji wa kile alichoahidi Novemba 14, mwaka huu, alipohutubia Bunge la 13, akisema aliuzunishwa na matukio hayo ya Oktoba 29 na 30 na kwamba ataunda tume kuchunguza.
Katika matukio hayo, baadhi ya watu walipoteza maisha, mali na miundombinu ya umma na binafsi ziliharibiwa na kuchomwa moto.
Vyama hivyo vya upinzani vimepinga tume hiyo vikishauri iundwe itakayojumuisha wajumbe kutoka nje ya Tanzania, wakiwamo wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika, Taasisi za Kimataifa za Haki za Binadamu, ili haki itendeke vikisema Serikali pamoja na vyombo vyake ni sehemu ya watuhumiwa.
Akizungumza Dar es Salaam, jana Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche alisema tume hiyo haiwezi kutenda haki katika mazingira ambayo Serikali inadaiwa kutuhumiwa.
“Haiwezekani mtuhumiwa akajichunguza mwenyewe halafu tutarajie haki kupatikana.Tunatoa wito kwa taasisi za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa kuishinikiza Serikali kuruhusu uchunguzi huru wa kimataifa,” amesema Heche.
Kwa mujibu wa Heche, wote walioteuliwa katika Tume hiyo waliwahi kuwa au ni watumishi wa Serikali kwa nyakati tofauti, lakini pia ni wanachama wa chama cha siasa kilichoshika dola.
“Tume huru haipaswi kuwa na uhusiano wowote na Serikali wala chama tawala. Kwa jinsi ilivyo Tume hiyo ni njama ya kuficha ukweli, kufuta ushahidi na kuendelea kuwaumiza waathirika.”
Kwa upande wake, CUF kimetoa wito kwa Jumuiya za kimataifa na kikanda kuishinikiza Serikali kufanyika kwa uchunguzi huru wa mauaji, uvunjaji wa haki za binadamu na uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mohamed Ngulangwa, matarajio yao ni kuundwa kwa chombo huru kitakachojumuisha wawakilishi kutoka taasisi za kimataifa.
“Tunataka chombo huru kitakachojumuisha wawakilishi kutoka taasisi za nje zinazohusika na haki za binadamu na utawala bora, asasi za kiraia zilizo huru na majaji wenye rekodi ya kuaminika watakaoweza kusimamia haki bila kujichagulia upande,” amesema.
Ngulangwa amesema Tume iliyoundwa inakosa sifa ya kuaminika kufanya uchunguzi huru wenye matokeo ya yatakayoaminika na makundi yote yaliyoathirika kwa namna tofauti.
“Tume inayopaswa kuchunguza matukio haya inapaswa kuwa huru na ya kuaminika ndani na nje ya nchi, kama kweli tuna lengo la kuliponya Taifa. Tume huru ya uchunguzi isichukuliwe kwa uzito mwepesi na wala mzaha usipewe nafasi,” amesema Ngulangwa.
Jana Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alidai Tume hiyo si ya haki bali ni jaribio la kuficha makosa na kuwalinda waliohusika katika unyanyasaji huo.
Ado ameweka wazi kuwa chama hicho hakitashiriki kwa namna yote ile katika uchunguzi utakaofanywa na Tume hiyo.
Walichosema Ada Tadea, NLD
Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatibu amesema anaunga mkono uamuzi wa Rais Samia kuunda Tume hiyo.
“Tanzania tunajuana wenyewe, haiwezekani kila jambo tukaita watu wa nje, Tanzania ni nchi huru inayojitawala haiwezekani matatizo yetu tukaita watu wa nje waje kuyatatua,” amesema Khatibu ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa.
“Ada Tadea tuna imani na wajumbe walioteuliwa, tunamuunga mkono Rais, nawaomba viongozi wa siasa waache ubepari na ubeberu, tupende vya kwetu na kuwatukuza wataalamu wetu,” amesema.
Katibu Mkuu wa NLD, Hassan Doyo amesema haiwezekani jambo lifanyike ndani ya nchi, kisha kuwaita wa nje ya nchi kuchunguza watu
“Kwanza, nani mwenye mamlaka ya kuunda Tume kwenye nchi ya watu? Pili, naamini hawa walioteuliwa wanaweza kutekeleza wajibu wao kwa haki,” amesema.
Katika hatua nyingine, mwanadiplomasia mwandamizi Balozi Benson Bana amesema ni wakati mwafaka kumuachia Rais Samia kutumia vyombo vyake vyote vya kikatiba kutafuta ukweli na taarifa sahihi zitakazomwezesha kufanya uamuzi ulio bora kwa masilahi ya umma.
Amesema vyama vya upinzani na raia wa kawaida wanayo haki ya kutoa maoni kuhusu Tume mpya ya uchunguzi kwa kuwa ni chombo kilichowekwa hadharani, lakini akasisitiza umuhimu wa kuheshimu mipaka ya mamlaka ya kikatiba ya Rais.
“Tuiache hii Tume ifanye kazi, hatujui hadidu za rejea, muda wake wa kazi, wala mamlaka yake kamili. Hayo yote ni Rais atakayeyaelekeza ili Tume itekeleze wajibu wake kwa misingi ya ukweli na haki.
“Rais ameapa kwa mujibu wa Katiba yetu, si vizuri kumfundisha jinsi ya kufanya kazi,” amesema Balozi Bana.
Amefafanua kuwa kuna sheria inayompa Rais mamlaka ya kuunda kamisheni za uchunguzi ili kubaini kilichotokea, kutathmini maeneo yaliyokwama na kumpatia mapendekezo sahihi ya hatua za kuchukua kwa manufaa ya Taifa.
