Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema upungufu mkubwa wa ufadhili unalifanya kushindwa kuwafikia hata theluthi moja ya watu milioni 318 wanaotazamiwa kukabiliwa na njaa kali ifikapo mwaka 2026.
Kwa mujibu wa WFP, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kali imeongezeka kwa zaidi ya mara mbili tangu 2019, kutokana na mchanganyiko wa migogoro, athari za mabadiliko ya tabianchi na misukosuko ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa WFP watu 318 wanakabiliwa na njaa duniani huku zaidi ya watu milioni 124 walilishwa na shirika hilo kwa mwaka 2024.
Katika taarifa iliyotolewa na tovuti za DW na Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la WFP limeeleza kuwa limelazimika kujikita kwa watu milioni 110 walio hatarini zaidi, huku ikikadiria kuwa hatua hiyo inahitaji zaidi ya dola bilioni 13. Hata hivyo, shirika hilo limeonya linaweza kupata nusu tu ya fedha hizo kutokana na kupungua kwa misaada ya kimataifa.
Taifa la Marekani ambalo ndilo mfadhili mkubwa wa WFP limepunguza misaada yake chini ya utawala wa Rais Donald Trump, huku baadhi ya nchi za Ulaya pia zikibana bajeti za kibinadamu, hali inayoathiri moja kwa moja uwezo wa mashirika ya misaada kutoa huduma.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametangaza njaa katika Ukanda wa Gaza na baadhi ya maeneo ya Sudan mwaka huu, hatua ambayo Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain, ameieleza kuwa ni ‘fedheha katika karne ya 21’.
Katika utangulizi wa Ripoti ya Mtazamo wa 2026, McCain amesema majibu ya dunia bado yamegawanyika, yanachelewa na hayatoshi, ambapo karibu operesheni zote zimepunguza mgao wa chakula na pesa.
Amesema pia mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada yameongezeka, ishara ya kuzorota kwa uzingatiaji wa sheria za kibinadamu kimataifa.
Watu milioni 41 katika hatari ya dharura
Wakati huohuo WFP imeeleza kati ya watu milioni 318 wanaokabiliwa na njaa kali, takribani milioni 41 wapo katika kundi la dharura au chini yake. Wiki iliyopita, WFP kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) yalitaja maeneo 16 duniani ikiwamo Haiti hadi Sudan Kusini kuwa katika hatari ya njaa.
Mashirika hayo yamepokea dola bilioni 10.5 pekee kati ya dola bilioni 29 zinazohitajika kukabiliana na hali hiyo mwaka huu, pengo linaloelezwa kuongeza mateso kwa mamilioni ya watu.
