Zigo la Mchengerwa Wizara ya Afya hili hapa

Dar es Salaam. Uteuzi wa Omary Mchengerwa kuwa Waziri wa Afya, umeibua maoni mapya kutoka kwa wadau wa sekta hiyo, wakibainisha maeneo muhimu yanayohitaji msukumo wake wa haraka.

Miongoni mwa mambo yanayomsubiri Mchengerwa aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 17, 2025 ni usimamizi makini wa utoaji wa huduma za afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote.

Baadhi ya wadau wamesema uteuzi wa Mchengerwa umekuja katika kipindi ambacho sekta ya afya inahitaji mwelekeo mpya, ushirikiano mpana na uwekezaji wa kimkakati, huku matumaini yakiwa juu ya uwezo wake kuweka mageuzi yatakayoinua huduma za afya nchini.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti juu ya hilo, wadau hao wamesisitiza kuwa, katika utekelezaji wa bima hiyo, sekta binafsi isionekane mpinzani wa Serikali bali mshirika katika kutoa huduma.

Baadhi ya wadau wamemtaka waziri huyo mpya kushawishi ongezeko la bajeti ya afya kufikia angalau asilimia 15 ya Bajeti ya Taifa, kama ilivyokubaliwa kwenye Mkataba wa Abuja.

Mwelekeo wa bajeti ya afya

Maoni ya wadau hao yanakuja kufuatia tathimini ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa miaka ya hivi karibuni, ambayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Bajeti hiyo ilipanda kutoka Sh2.019 trilioni mwaka 2021/22 hadi Sh2.149 trilioni mwaka 2022/23.

Mwaka 2023/24 ilifikia Sh2.464 trilioni na kwa mwaka 2024/25 imefikia Sh2.540 trilioni.

Julai mwaka jana Rais Samia alipokuwa akifunga Kongamano la Kumbukizi ya Hayati Benjamin Mkapa, alisisitiza kuwa, mafanikio ya sekta ya afya yanahitaji nguvu ya pamoja ikihusisha Serikali, sekta binafsi, wadau na taasisi za dini.

Alisema wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi yatakayovutia uwekezaji katika huduma za afya.

Rais wa Chama cha Wafamasia, Fadhili Ezekiah amesema pamoja na mabadiliko ya viongozi ndani ya wizara, suala muhimu linalopaswa kuangaliwa ni ubora wa elimu kwa vyuo vya kada za kati, hasa kutokana na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi katika maeneo ya mafunzo ya afya.

Ezekiah amesema lazima kuwepo usimamizi madhubuti ili wahitimu wanaozalishwa wawe na ubora unaolingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

“Tumefungua milango sana, kwa sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta ya afya hasa elimu. Ni muhimu kuweka usimamizi madhubuti wa wadau hao ili wataalamu watakaozalishwa wawe na ubora na kuendana na takwa la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050,” amesema Ezekiah.

Pia, amesema Mchengerwa itabidi atupie jicho kwenye utekelezwaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaopaswa kuwa shirikishi ili kuhakikisha sekta binafsi inatumika kama nyenzo ya kuongeza upatikanaji wa huduma, badala ya kuonekana mshindani wa Serikali.

Ezekiah ameshauri Waziri Mchengerwa kusimamia utekelezaji wa utoaji wa huduma ya afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote, akisema wagonjwa wa kulazwa pekee ndio wahudumiwe hospitali za Serikali.

“Ni muhimu wagonjwa wa kulazwa wakahudumiwa hospitali za Serikali, huku wagonjwa wa nje waruhusiwe kupata dawa katika maduka binafsi yaliyosajiliwa,” ameshauri Ezekiah.

Hata hivyo, ametahadharisha kuiona sekta ya afya kuwa ya madaktari na wauguzi pekee, akisisitiza kuwa, kada nyingine kama wafamasia, wanasaikolojia, wataalamu wa mazoezi na mazingira pia ni muhimu katika mfumo wa huduma, jambo alilosema waziri pia anapaswa kuliona hilo kwa kina.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema moja ya majukumu ya haraka ya Waziri Mchengerwa ni kutoa tathmini ya namna hospitali zilivyohudumia majeruhi wa maandamano ya Oktoba 29, mwaka huu ili kubaini maeneo ya kuboresha.

“Majeruhi wengi walifika hospitalini na kupewa huduma. Sasa tunataka tuangalie ni mambo gani tumejifunza kwenye jambo hilo ili yasijirudie kamwe,” amesema Dk Nkoronko.

Dk Nkoronko amesema mzigo mwingine unaomsubiri Mchengerwa ni wa kuunda sera mpya ya afya.

Amesema wizara hiyo inahitaji sera mpya ya afya kwa kuwa iliyopo ni ya mwaka 2007 na haitoshelezi mahitaji ya sasa ya maendeleo ya sekta.

Pia, amependekeza kuwepo kwa sheria moja ya afya itakayojumuisha maeneo yote muhimu, badala ya kuwa na sheria tofauti zinazohusiana na bima na usajili wa madaktari.

Dk Nkoronko amesema uwekezaji katika vifaatiba na miundombinu, unahitaji kuimarishwa, sambamba na kuongeza bajeti ya sekta kufikia malengo ya Abuja.

Ameongeza kuwa, wizara inapaswa kuwekeza katika mifumo ya udhibiti wa magonjwa, uzalishaji wa dawa na vifaatiba nchini, pamoja na kuchochea tafiti za ndani ili ziwe msingi wa uamuzi wa kitabibu.

Dk Nkoronko amesema ni muhimu Tanzania kunufaika na soko la usambazaji dawa katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), sambamba na kuhakikisha kila Mtanzania anamudu kugharamia matibabu, jambo alilosema waziri anapaswa kulisimamia na kuhakikisha dhamira hiyo inatimia.

Kwa upande mwingine, Dk Nkoronko amesema tiba za Tanzania zinategemea matokeo ya tafiti, hivyo Waziri Mchengerwa anapaswa kujenga ushawishi ndani ya Serikali ili kuwe na bajeti kubwa ya utafiti, kwa sababu asilimia 80 ya tafiti zinazotumika sasa, zinatoka nje ya nchi.

Dk Nkoronko amesema kutokana na mabadiliko haya, wataalamu wanatamani kuona tafiti zilizofanyika Tanzania zinatumika kuleta majibu ya changamoto za afya zilizopo nchini.

“Jambo lingine tunataka tuone ubunifu wake utakaochochea uwezo wa kila Mtanzania kumudu kugharamia huduma za matibabu,” amesema Dk Nkoronko.

Mtaalamu wa Afya, Ernest Winchislaus amesema masilahi duni ya watumishi wa afya ni mzigo mwingine kwa waziri huyo.

Winchislaus amesema suala hilo limeimbwa kwa muda mrefu, sasa linapaswa kushughulikiwa kwa haraka, kwa sababu wahudumu hao wanafanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya wanavyolipwa.

Amesisitiza pia umuhimu wa kusimamia kikamilifu Bima ya Afya kwa Wote ili kuwafikia Watanzania wote.

Winchislaus amesema pamoja na hatua zilizochukuliwa kuboresha sekta hiyo, bado kunahitajika uwekezaji mkubwa katika vifaatiba vya kisasa.

Historia ya uteuzi wa Mchengerwa

Kabla ya kuteuliwa kuongoza Wizara ya Afya, Mchengerwa alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Nafasi hiyo ameichukua kutoka kwa Jenista Mhagama, aliyeongoza wizara hiyo kuanzia Agosti 14, 2024, baada ya kutokea mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Kabla ya Jenista, wizara hiyo iliongozwa na Ummy Mwalimu aliyeanza kuitumikia tangu Novemba, 2015.