Ajibu afichua jambo kwa Tshabalala

KIUNGO Mshambuliaji wa KMC, Ibrahim Ajibu amemtabiria makubwa nahodha wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ atafanya vizuri katika timu hiyo kutokana na ubora alionao.

Tshabalala amejiunga na Yanga akitokea Simba mwanzoni mwa msimu huu na tayari ameingia katika mfumo akianza kucheza kikosi cha kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ajibu amesema lilikuwa ni suala la muda kwa Tshabalala kujiunga na Yanga kutokana na ubora aliokuwa nao huku akiweka wazi ushawishi wa fedha na kiwango bora ndiyo siri ya wachezaji wengi kutoka timu hizo kongwe kuhama.

TSHA 01

“Sikushangazwa na Tshabalala kuhama kutoka Simba kwenda Yanga, hii haijaanza sasa, tangu miaka ya nyuma wachezaji walihama kutoka timu moja kwenda nyingine kutokana na ubora, pia ushawishi wa fedha,” amesema Ajibu aliyewahi kuzitumimia Simba, Yanga, Azam FC na Singida Fountain Gate na Coastal Union.

“Beki huyo ni bora ukiondoa fedha ambazo amevuna akijiunga na Yanga nina imani kubwa atafanya mambo makubwa kwani sio mchezaji wa kuridhika ni mpambanaji hajawahi kukubali kushindwa kirahisi atakuwa bora pia ndani ya Yanga,” aliongeza Ajibu.

Akizungumzia KMC timu ambayo amekuwa akiitumikia kwa sasa amesema wabnapitia wakati mgumu kutokana na matokeo lakini anaamini watakuwa bora kwenye mechi zijazo.

TSHA 02

“Tumeanza vibaya matokeo hayatufurahishi lakini huu hauwezi kuwa mwisho wetu tunaendelea kujifua na kujiweka tayari kwa ajili ya kujiweka tayari kwa ushindani kwa mechi zinazofuata,” amesema Ajibu na kuongeza;

“Wachezaji wote, benchi la ufundi na uongozi tunatambua umuhimu wa kuwa na timu bora shindani tunatarajia kurudi tukiwa imara ili kuipambania nembo ya timu iweze kucheza msimu ujao na kumaliza kwenye nafasi nzuri.”