KIPA namba moja wa Simba, Moussa Camara amefanyiwa upasuaji salama huko Morocoo, huku mwenyewe akivunja ukimya kwa kukiri haikuwa rahisi kwake kukubali uamuzi huo kwa hofu aliyokuwa nayo awali, lakini akituma salamu kwa nyota wa Simba kuelekea mechi za CAF.
Camara aliyeongeza mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika mwishoni mwa msimu huu, jana Novemba 18, 2025 amefanyiwa upasuaji wa goti la kulia na sasa atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki 10 na kumfanya akose mechi kama sita, japo ataiwahi Yanga baada ya Dabi ya Kariakoo kusogezwa hadi Machi 2026.
Awali, dabi hiyo ilipangwa kupigwa Desemba 13, 2025 na kipa huyo angeikosa, lakini sasa itapigwa akiwa ameshapona na kurejea uwanjani, kitu kinachomfurahisha Camara.
Akizungumza mara baada ya kufanyiwa upasuaji huo, Camara amesema haikuwa rahisi kukubali upasuaji huo ambao ni wa kwanza katika maisha yake, jambo ambalo awali lilimtisha.
Camara amesema hata hivyo, baada ushauri wa kina kutoka kwa madaktari wa Simba, viongozi, wasimamizi binafsi alikubaliana na hatua hiyo na anashukuru jambo hilo limepita salama na sasa anajiuguza ili apone na kurejea tena uwanjani baada ya miezi miwili na ushei ijayo.
“Haikuwa rahisi kukubali hii hatua, nilikuwa na wasiwasi sana, lakini madaktari wa klabu yangu Simba, viongozi, wasimamizi na familia wamenisaidia sana kubadili akili yangu, ni kweli nilikuwa sikubaliani na uamuzi huo kabisa,” amesema Camara na kuongeza;
“Madaktari walionifanyia upasuaji wameniambia hakukuwa na njia nyingine ya kupona bila kufanya hiki kilichofanyika, taarifa iliyonivutia wamenionyesha mastaa wakubwa tu waliopitia tatizo kama hili na wakapona na sasa nawaona wanacheza kama kawaida, wameniambia nitapona ndani ya wakati.”
Pia kipa huyo raia wa Guinea, amewatumia salamu wachezaji wenzake wa Simba akiwataka kuendelea kuipigania klabu hiyo na kuhakikisha furaha ya mashabiki inaendelea hata kwenye mechi ngumu ambazo wanakwenda kuzicheza.
“Nawaombea sana wenzangu na timu kwa ujumla waendelee kuipigania klabu,” amesema kinara huyo wa cleansheet katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita alipomaliza na 19 akicheza mechi 28 kati ya 30.
Camara wakati anaanza hatua ya uponaji, atazikosa mechi sita za mashindano yote zikiwemo tatu za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Petro Atletico, Stade Malien na Esperance, wakati zile za Ligi Kuu Bara ni dhidi ya TRA United, Azam FC na Tanzania Prisons.
