Ceassia kushusha mashine tatu WPL

KOCHA Mkuu wa Ceassia Queens ya Iringa, Ezekiel Chobanka amekiri kikosi cha timu hiyo kipo katika wakati mgumu baada ya kuanza vibaya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), huku akianza hesabu za mapema za usajili wa dirisha dogo akilenga kushusha mashine tatu za maana.

Ceassia imeanza vibaya ligi hiyo baada ya kupoteza mechi mbili za awali za WPL, ikifungwa na Geita Queens na Alliance Girls kila moja kwa 1-0, jambo lililomfanya Chobanka akune kichwa.

Akizungumza jijini Mwanza baada ya kupoteza 1-0 mbele ya Alliance Girls, Chobanka amesema wameanza vibaya kutokana na upya wa kikosi chake ambacho asilimia 90 wachezaji ni wapya wamesajiliwa dirisha kubwa.

“Lakini sishangai matokeo haya kwa sababu tuna timu mpya ndiyo naanza kusuka timu kwani tumeleta wachezaji wengi wapya na katika kikosi kilichopo ni wanne tu tuliokuwa nao mwaka jana,” amesema Chobanka.

Amesema tayari ameanza mikakati ya kuimarisha timu yake katika dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba, mwaka huu, ambapo atasajili wachezaji watatu.

“Nafikiria dirisha dogo nitaongeza wachezaji watatu wa kigeni ambao tayari wapo na walikuwa jukwaani leo. Nitaleta washambuliaji wawili na beki wa kati mmoja,” amesema Chobanka.

Kocha huyo wa zamani wa Alliance Girls na The Tigers Queens, amesema bado kikosi chake hakitumii vyema nafasi zilizotengenezwa katika michezo miwili waliyocheza mpaka sasa.

“Ilikuwa mechi ya ushindani kwa sababu wachezaji wengi wa Alliance nimewakuza, leo wametunyima utulivu na walitawala eneo la katikati lakini pia tumepata nafasi hatujazitumia,” amesema kocha huyo.