Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amefanya uteuzi na kubadilisha makatibu wa wizara nane, manaibu katibu wakuu wizara tano wakiwemo waliokuwa wakuu wa mikoa wawili.
Katika uteuzi huo, wizara tisa makatibu wake wakuu wameendelea kuwa walewale waliokuwapo awali na wateule wataapishwa Jumamosi Novemba 22, 2025 Ikulu Zanzibar.
Kutokana na taarifa kwa umma iliyotolewa usiku huu Novemba 20, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mattar Zahor Masoud ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Salama Mbarouk Khatib aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara wa Vijana Ajira na Uwekezaji.
Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Rahma Salim Mahfoudh ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango huku Saleh Mohamed Juma ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo akitokea kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo.
“Ali Said Bakari ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kabla ya hapo alikuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe.
Waliobadilishwa wizara ni Fatma Mabrouk Khamis ambaye amehamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu akitokea Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Khamis Suleiman Mwalimu amehamishiwa Wizara ya Kazi na Uwekezaji akitokea Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji huku Dk Habiba Hassan Omar akihamishiwa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Katika taarifa hiyo Mohamed Dhamir Kombo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Idara ya Kilimo na Uhakiki wa Chakula.
Amos John Enock ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rashid Ali Salum amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Uwekezaji kabla uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Makame Machano Haji ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
“Khalid Masoud Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji akitokea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
