Mbeya. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Mbeya, imebariki kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya Sh1 milioni alichohukumiwa Itika Ulimboka Mwakasura kwa kosa la kumbaka na kumlawiti bibi mwenye umri wa miaka 90.
Hukumu hiyo imetolewa Novemba 17, 2025 na Jaji Joachim Tiganga, na nakala ya hukumu hiyo kupatikana katika tovuti ya mahakama (TanzLII) leo Alhamisi, Novemba 20, 2025, wakati akitoa uamuzi wa rufaa iliyokuwa imekatwa na Mwakasura.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Januari 24, 2025 katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, na ilidaiwa Mwakasura aliingia katika nyumba ya bibi huyo na kumwingilia bila ridhaa yake, ambapo alimbaka na kisha kumlawiti.
Kulingana na kumbukumbu za mahakama, mrufani katika rufaa hiyo alikutwa na mtoto wa bibi kizee huyo akiwa uchi ndani ya chumba alichokuwa amelala mama yake, ambapo alijaribu kutoroka lakini alikamatwa akiwa uchi.
Upande wa Jamhuri katika shauri hilo lililosikilizwa na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe uliita mashahidi saba na kuwasilisha ripoti ya daktari kama kielelezo, lakini bibi huyo hakuweza kutoa ushahidi kutokana na umri wake na hali ya kiafya.
Katika utetezi wake, mrufani alikanusha mashtaka dhidi yake na kudai aliingia ndani ya chumba cha bibi huyo kwa lengo la kuiba maharagwe, utetezi ambao ulikataliwa na mahakama na kuhukumiwa miaka 30 jela.
Mwakasura alikata rufaa akiegemea sababu sita kwamba hakimu alikosea kisheria na kimantiki pale alipoamini mashahidi wa Jamhuri ambao ushahidi wao ulikuwa hautoshi kumtia hatiani kwa kuwa hakuna aliyemuona akibaka na kulawiti.
Akijenga hoja za sababu za rufaa, mrufani huyo alieleza ametiwa hatiani kwa kosa la kubaka kinyume cha kifungu 130(1)(2)(e) na 131(1) na kosa la kulawiti kinyume na kifungu 154(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyorejewa 2023.
Alieleza katika ushahidi wao, shahidi wa pili na watatu walikuwa wa kutiliwa mashaka na walishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake kwa kuwa ushahidi wao uliegemea katika mashaka na haukuwa unathibitisha kosa.
Aliendelea kudai mahakama ilikosea pale iliposhindwa kutafuta ripoti ya mtaalamu ili kupima kama mwathirika alikuwa hawezi kutoa ushahidi, na kwamba mahakama iliukataa ushahidi wake bila uhalali wowote kinyume cha sheria.
Mrufani aliendelea kueleza kuwa shahidi wa kwanza, ambaye ni mtoto wa bibi kizee huyo, hakushuhudia kwa macho yake akimbaka na kumlawiti mama yake.
Alieleza ushahidi wa shahidi huyo na ule wa mke wa shahidi huyo ulikuwa wa mashaka kwa kuwa yeye (mrufani) alikiri tu kuingia katika nyumba hiyo kama mwizi wa maharagwe na sio kama mbakaji au mlawiti kama ilivyodaiwa.
Mwakasura alisema kitendo cha bibi kizee huyo kushindwa kutoa ushahidi wake mahakamani kilimnyima haki na kuhoji kwa nini kama hakuwa anaweza kutoa ushahidi, aliweza kupiga yowe siku ya tukio kama shahidi wa kwanza anavyodai.
Alilalamika kuwa mahakama ilimtia hatiani kimakosa kwa mhemuko na kutozingatia utetezi wake, huku akipinga ushahidi wa daktari kwamba ulikuwa wa mashaka kwa vile alishindwa kueleza mashine aliyotumia kufanya uchunguzi.
Jamhuri alivyopangua rufaa
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali George Mgwembe alisema sababu za rufaa hazina maana kwa vile ili kuthibitisha shitaka la ubakaji ni lazima kumwingilia kuthibitishwe pamoja na umri wa mwathirika na utambulisho wa mshukiwa.
Kuhusu kosa la ulawiti, wakili huyo alisema upande wa mashtaka ulitakiwa tu kuthibitisha mshtakiwa alimwingilia mwathirika kinyume cha maumbile kama inavyoelezwa na kifungu 154(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu.
Katika kesi hiyo, alisema ushahidi wa shahidi wa kwanza, pili na tatu uliungwa mkono na ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni daktari, na hivyo kuweza kuthibitisha pasipo kuacha mashaka yoyote kuwa bibi kizee huyo alibakwa na kulawitiwa.
Akirejea ushahidi wa shahidi wa kwanza, wakili huyo alisema alitoa ushahidi kuwa alimkuta mrufani ndani ya chumba cha mama yake, huku mama yake akiwa amelala kitandani bila nguo za ndani na kukiwa na kinyesi kitandani.
Kwa upande wa mrufani, shahidi huyo alieleza kuwa alimkuta akiwa uchi kuanzia kiunoni hadi miguuni, na kwamba alijaribu kutoroka eneo la tukio lakini alikamatwa baadaye akiwa uchi kama alivyotoka ndani ya chumba hicho.
Pia alirejea ushahidi wa daktari aliyemchunguza bibi kizee huyo na kubaini uke wake ulikuwa umeingiliwa, alikuwa na michubuko na wekundu, na pia sehemu ya haja kubwa ilikuwa na michubuko na misuli yake ilikuwa imelegea.
Wakili huyo alisema kitendo cha daktari kushindwa kutaja vifaa vya kisasa alivyovitumia kufanya uchunguzi hakikuathiri kesi ya Jamhuri, na kwamba mrufani alikuwa na nafasi ya kumdodosa shahidi juu ya hilo na hakufanya.
Alieleza bibi kizee huyo alipiga yowe la kuomba msaada usiku huo, ambalo ndilo lilimfanya mtoto wake kuingilia, na ile kukutwa na michubuko sehemu za siri na kinyesi kitandani kunathibitisha alitumia nguvu kumwingilia bibi huyo.
Wakili Mgwembe alieleza kuwa wakati ushahidi bora katika kesi za ubakaji unapaswa kutoka kwa mwathirika mwenyewe, yapo mazingira kama umri mdogo, uzee na hali ya kiafya yanayoweza kufanya ashindwe kutoa ushahidi kortini.
Hata hivyo alisema ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri kwa ujumla wake ulikuwa wa kuaminika, uliounganika na ulithibitisha vigezo vyote muhimu vinavyotakiwa kisheria kuthibitisha kosa la ubakaji na ulawiti kama ilivyo katika kesi hiyo.
Jaji Tiganga katika hukumu yake alisema ili kuthibitisha kosa la jinai pasipo kuacha mashaka yoyote, sheria iko wazi katika kuthibitisha kosa la kubaka kwamba upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha vipengele vitatu.
Moja ni mwathirika kuingiliwa (penetration) hata kama ni kidogo, mwathirika kuingiliwa bila ridhaa yake, na utambulisho wa mshtakiwa aliyetenda tendo hilo.
Katika kesi hiyo, Jaji Tiganga alisema ushahidi wa daktari unaonyesha sehemu za siri za bibi kizee huyo kulikuwa na michubuko, wekundu na mishipa ilikuwa imelegea, na pia uwepo wa damu kwenye kinyesi kilichopatikana kitandani.
“Daktari alihitimisha kuwa kitu butu kilimwingilia mwathirika. Huu ushahidi wa kisayansi unathibitisha kipengele cha kuingiliwa. Umri wa miaka 90 wa mwathirika na kelele za kuomba msaada alizotoa zinathibitisha hakuridhia,” alisema Jaji.
Jaji alisema katika hoja zake, mrufani alidai hakuna shahidi aliyemuona akifanya kitendo hicho, lakini hata hivyo ni kanuni iliyo wazi kuwa kosa la kubaka hufanyika kwa siri na mara chache kwa uwazi, hivyo ushahidi wa mazingira hutumika.
“Kwenye shauri hili, ushahidi unaomuunganisha mrufani na kosa sio tu unamuunganisha bali ni balaa. Mrufani alikutwa na shahidi wa kwanza ndani ya chumba cha mwathirika usiku wa manane tena akiwa uchi.
“Lakini mwathirika naye, akiwa na msongo, alikutwa hana nguo za ndani na kukiwa na kinyesi kitandani, mrufani akatoroka eneo la tukio lakini akakamatwa baadaye akiwa uchi. Nguo zake zilipatikana eneo la tukio na kuchukuliwa na polisi,” alisema.
Jaji alisema mtiririko wa matukio ambao unaungwa mkono na ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri unamnyooshea kidole mrufani na si mtu mwingine, hasa ikizingatiwa kuwa alikutwa ndani ya chumba cha mwathirika akiwa uchi.
Kulingana na Jaji, utetezi wake kuwa aliingia ndani ya chumba hicho kwa lengo la kuiba maharagwe ni ushahidi wa baadaye (afterthought) kama njia ya kujinasua, kwani kama alikuwa ni mwizi ilikuwaje akavua nguo zake ndani ya chumba.
“Hoja ya mrufani kuwa mahakama ilihitaji kuwa na taarifa ya mtaalamu kuthibitisha mwathirika hawezi kutoa ushahidi haina mashiko. Sheria ya ushahidi inatoa nguvu kwa mahakama kupima uwezo wa shahidi kutoa ushahidi,” alisema.
Jaji Tiganga alisema amepitia hukumu ya hakimu aliyemtia hatiani mrufani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela na kulipa faini ya Sh1 milioni kwa familia ya mwathirika, na kuridhika kuwa alichambua kwa kina ushahidi wa pande mbili.
Ni kutokana na hilo, alisema upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha shitaka hilo bila kuacha mashaka yoyote kwamba ni mrufani ndiye aliyembaka na kumlawiti bibi kizee huyo na anastahili adhabu aliyopewa na mahakama ya chini.
