Dar es Salaam, Novemba 20, 2024 — Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ongezeko la wahitimu wanawake
katika elimu ya juu ni ishara muhimu ya hatua ambayo Tanzania inapiga katika
kufikia usawa wa kijinsia.
Amesema hayo leo wakati wa duru ya tatu ya mahafali ya 55 ya
UDSM, yaliyowatunuku wahitimu 2,452 wa shahada na astashahada. Kati ya hao:
Wanawake ni 1,386 (56.6%)
Wanaume ni 1,066
Takwimu hizo zinaendeleza mwelekeo wa duru ya pili ya
mahafali iliyofanyika Novemba 18, 2025, ambapo wahitimu walikuwa 2,742,
wakiwemo:
Wanawake 1,510 (55.4%)
Wanaume 1,232
Kikwete, ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, alisema
awali idadi kubwa ya wanafunzi wa kike ilikuwa ikionekana zaidi kwenye elimu ya
msingi na sekondari, lakini sasa ongezeko hilo limepanuka hadi ngazi ya vyuo
vikuu.
“Ni jambo la kutia moyo kuona wanawake wakiongoza
katika elimu ya juu. Haya ni mafanikio makubwa kwa taifa letu,” alisema.
Kwa mujibu wa wadau wa elimu, ongezeko la wahitimu wanawake
linatarajiwa kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi, taaluma za
kitaalamu na sekta za kiuchumi ambazo kwa muda mrefu zimetawaliwa na wanaume.
Mahafali ya mwaka huu yametajwa kuwa miongoni mwa yenye
uwiano mkubwa zaidi wa kijinsia kuwahi kurekodiwa katika historia ya UDSM.


.jpg)