Kuenea kwa 4G, 5G na mustakabali wa ujumuishi wa kidijitali Tanzania

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua na kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi, hasa kupitia mitandao ya 4G na 5G.

Hatua hii imekuwa chachu muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali unaowezesha wananchi, taasisi na biashara kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha ongezeko kubwa la watumiaji wa intaneti, huku asilimia kubwa wakitumia huduma za 4G.

Aidha, kuanzishwa kwa huduma za 5G katika baadhi ya miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Mwanza kumefungua ukurasa mpya katika mapinduzi ya kidijitali nchini.

Kwa mujibu wa TCRA hadi Septemba 2025 kulikuwa na mitambo 14,104 ya kukurushia mawimbi ya simu ya 4G huku ile ya 5G ikifikia 1059. Kiwango cha mitambo ya 4G hivi sasa ni kikubwa kuliko ile ya 3G ambayo ipo 13,845 lakini ni kidogo kuliko 2G ambayo ina mitambo 15,050.

Kwa upande wa ueneaji wa mtandao wa 2G ndiyo umeenea zaidi ukifikia asilimia 98.6 ya watu wote nchini ukifuatiwa na 4G kwa asilimia 94.2, 3G kwa asilimia 93.8 kisha 5G kwa asilimia 28.9.

Hata hivyo eneo zima la nchi limefikiwa kwa asilimia 78.2 ya mtandao wa 2G, 3G kwa asilimia 75.9, 4G kwa asilimia 76.9 na 5G kwa asilimia 8.6.

Kwa upande wa matumizi kiwango cha utumiaji wa intaneti kwa kutumia teknolojia mbalimbali kilifikia watu milioni 56.3 huku wastani wa kusambaa kwa mtandao huo ukiwa ni asilimia 82.6 ya idadi ya watu nchini.

Kwa upande wa watoa huduma za intaneti kupitia simu kampuni ya Vodacom inaongoza soko kwa asilimia 32.7 ikifuatiwa na kampuni ya Yas kwa asilimia 28.5, Airtel kwa asilimia 20.7, Halotel kwa asilimia 15.4 na TTCL kwa asilimia 2.7.

Serikali kupitia mkakati wa Tanzania Digital Economy Framework imeweka kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano ya kisasa. Kupitia mradi wa National ICT Broadband Backbone (NICTBB).

Maelfu ya kilomita za mkongo wa taifa yamejengwa, mamilioni ya watanzania wameunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti katika maeneo ya mjini na vijijini.

Kampuni za simu nazo zimeongeza uwekezaji katika teknolojia za 4G na 5G huku maeneo mengine zikifanya ushirikiano na serikali ili kutimiza malengo. Ushirikiano huu wa sekta binafsi na serikali umechochea mapinduzi makubwa ya kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma.

Katika ripoti ya robo mwaka iliyoishia Septemba mwaka huu Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Philip Besiimire anasema wamefanikiwa kujenga vituo vipya 229 vya 4G, kati ya hivyo 41 vikiwa katika maeneo yenye upungufu wa huduma kupitia ushirikiano wetu na Serikali chini ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).

Anasema uboreshaji huo ulianza katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, ambapo walikuwa akitekeleza mpango mkakati wa miaka miwili katika kuboresha miundombinu ya kiteknolojia, ambao unahusisha uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani milioni 100 (Sh250 bilioni). “Maboresho hayo yanajumuisha kuboresha mtandao wetu wa radio (radio access network) katika maelfu ya maeneo ya mtandao wetu, pamoja na kuboresha zaidi miundombinu yetu ya TEHAMA, ikiwamo jukwaa la M-Pesa,” alisema Besiimire.

Anasema mpango huu unaboresha uzoefu wa wateja kwa kuongeza ubora wa huduma za mawasiliano na M-Pesa, sambamba na kupanua wigo wa teknolojia za 4G na 5G katika mtandao wetu.

“Kuboresha mtandao wetu kutasaidia kuharakisha utekelezaji wa malengo yetu ya kuondoa pengo la kidigitali katika maeneo ya mijini na vijijini, huku tukiboresha ujumuishaji wa kifedha kupitia uimara wa huduma za M-Pesa,” alisema bosi huyo wa kampuni namba moja ya simu kwa idadi ya wateja.

Uwekezaji uliofanyika hadi sasa umechangia pakubwa katika kusaidia ukuaji wa asilimia 56 wa matumizi ya 4G. Sehemu kubwa ya matumizi ya data sasa inapitishwa kupitia mtandao wa 4G, huku teknolojia ya 5G ikiongezeka kwa kasi kubwa zaidi.

Aidha Besiimire alidokeza kuwa Agosti mwaka huu kampuni anayoiongoza ilisherehekea miaka 25 tangu ianze kuwaunganisha Watanzania na mustakabali bora.

Faida za ongezeko la huduma intaneti ya kasi

Ongezeko la matumizi ya intaneti ya kasi limechochea ubunifu miongoni mwa vijana, kuibua ajira mpya katika sekta ya teknolojia, uandishi wa dijitali, maudhui ya mtandaoni na ushauri wa kidijitali.

Aidha, sekta ya afya imeanza kutumia teknolojia ya telemedicine kurahisisha uchunguzi na matibabu kwa njia ya video, hasa vijijini.

“Mambo mengi hivi sasa namaliza kiganjani mwangu ninachohitaji ni intaneti tu yenye utulivu nafanya vikao mtandao, nanunua kulipa na kuuza nikiwa popote pale, kwa ujumla mtandao umeongeza hata ufanisi wa kazi umeongezeka,” alisema John Japhet mfanyabiashara wa Dar es Salaam.

Hata hivyo pamoja na mafanikio haya, bado zipo changamoto kama gharama kubwa za vifaa na vifurushi vya intaneti, ukosefu wa uelewa wa teknolojia vijijini na usalama wa taarifa mtandaoni.