Kusimama kwa shughuli na athari zake kwa wamachinga

Wajasiriamali wa mitaani katika miji mbalimbali nchini ni kundi muhimu la wafanyabiashara ndogondogo katika jamii zetu.

Mapema asubuhi utaona wamebeba bidhaa zao njiani, wakiuza maji ya chupa, nguo, matunda, juisi, korosho, na mengine, utawakuta pembezoni ya barabara au kandokando ya maeneo yenye shughuli nyingi mfano maduka, masoko, au vituo vya mabasi.

Kipato chao ni kile wanachopata kila siku; ni lazima watoe jitihada kila siku ili kula, kulipa gharama za familia na kupata mahitaji mengine ya msingi. Si biashara zinazotabirika. Hata mabadiliko madogo ya hali ya hewa, kama kunyesha mvua, yanaweza kufanya siku nzima biashara isifanyike. Muuzaji hawezi kutoka na bidhaa zake, wateja watakosekana, na kipato cha siku hiyo hupotea.

Kadhalika kwa wateja wao, si watu maalum, ni wapita njia, wanaokwenda na kurudi kazini, madereva, abiria wanaosubiri usafiri, na wengine. Sio wateja labda kama tulivyozoea amekuja kufanya manunuzi “kufungasha”, wote, wauzaji na wananunua katika biashara hizi hawana kituo maalum, wanapokutana popote, nipe maji, chukua pesa yako, biashara imeshafanyika.

Hali hii inawafanya kuwa ni kundi linaloathirika kwa haraka zaidi pale hali ya utulivu inapoyumba. Mfano kuwapo zuio fulani mathalan kutotembea kwa sababu za kiusalama, muda huohuo biashara za namna hiyo zishasimama, basi hata ikiwa muuzaji atasema afunike kombe, wacha nitoke!, wateja hawatokuwapo mitaani, hakuna waendao wala kurudi.

Vilevile, kwa kuwa ni biashara za kuhama, kuyumba kwa usafiri hata kwa siku chache kunawaathiri pakubwa. Chukulia mfano muuzaji wa mahindi ya kuchoma; kila siku anategemea usafiri wa daladala kubeba mzigo wake kwenda mjini, na jioni anarudi nyumbani.

Usafiri wa umma unaposita, hata kwa siku mbili, tayari kwake ni changamoto kubwa. Hawezi kwenda na kurudi; hana duka la kuhifadhia bidhaa, wala hawezi kutumia usafiri mbadala. Kuongeza gharama kwa kuchukua usafiri wa bajaji au taksi kwa kuwa ni hasara kwa biashara kama yake.

Hali kadhalika, aina nyingine za biashara wanazofanya wajasiriamali hawa ni vigumu kuhifadhi. Hali yoyote ya dharura haiwaruhusu kuifungia bidhaa ndani ya duka au nyumba na kusubiri mambo yakiwa sawa.

Chukulia mfano wa muuzaji wa ice cream: kila asubuhi anapita katika duka la wasambazaji kuchukua mzigo tayari kwa kutembeza mitaani. Dharura inapotokea, hata kwa siku moja tu, inamaanisha hana bidhaa ya kuuza, na athari zake zinampata papo hapo.

Suala ninalojaribu kueleza ni kwamba si kwamba hakuna biashara isiyoathirika wakati wa kusitishwa kwa shughuli za kawaida, bali kundi la wajasiriamali wa mitaani ndilo linaathirika haraka zaidi. Hali hii inatokana kwa kiasi kikubwa na aina ya biashara wanazofanya pamoja na mazingira wanayoyakabiliana nayo kwa ujumla.

Kwa upande wa mamlaka za kiserikali, zinaweza kusaidia kundi hili katika kipindi cha mpito kwa kuwapa nafuu fulani kwa muda maalumu. Mfano kwa wale wanaolipa ushuru kwenye maeneo yao, wanaweza kupewa ruhusa ya kulipa kwa njia rahisi au kwa punguzo kama njia ya kutambua changamoto waliokumbana nazo na kuwawezesha kurejea kwenye hali ya kawaida ya biashara.

Vilevile, makampuni yanayowahudumia wajasiriamali hawa yanaweza kuzingatia kuwapa nafuu katika huduma au bidhaa wanazochukua. Hii inaweza kujumuisha mikopo ya muda mfupi au punguzo la bei kama njia ya kusaidia wajasiriamali kufidia baadhi ya athari za muda mfupi walizokumbana nazo wakati shughuli ziliposimama. Zaidi ya hayo, taasisi za elimu na wakufunzi katika masuala ya fedha na ujasiriamali wana jukumu muhimu la kuwafikia wajasiriamali hawa.