Madiwani 72 wajitokeza CCM kuwania umeya, uenyekiti Kilimanjaro

Moshi. Jumla ya madiwani 72 kutoka Halmashauri sita za Wilaya na Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania nafasi za uenyekiti wa halmashauri, meya na makamu mwenyekiti.

Kwa mujibu wa ratiba, uchukiaji wa fomu na urejeshaji kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Meya, wenyeviti wa halmashauri ni siku mbili kuanzia leo Alhamisi, Novemba 20 hadi kesho Ijumaa saa 10:00 jioni. Kisha vikao ngazi ya wilaya, mikoa na Kamati Kuu vitafuata.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa makatibu wa CCM wa wilaya saba za kichama mkoani humo, madiwani 47 wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Wenyeviti wa Halmashauri na Umeya, huku wengine 25 wakichukua fomu za nafasi ya makamu mwenyekiti.

Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, amesema leo ambayo ni siku ya kwanza jumla ya madiwani 17 walijitokeza kuchukua fomu,kati yao, madiwani 11 waliomba nafasi ya Wenyeviti wa Halmashauri na madiwani sita waliomba nafasi ya makamu mwenyekiti, wakiwemo wanawake wawili.

Miongoni mwa walioomba nafasi ya uenyekiti katika Halmashauri ya Moshi ni pamoja na Dickson Tarimo (Makuyuni), John Meela (Njiapanda), Deogratius Mushi (Kibosho Magharibi), Innocent Shirima (Marangu Mashariki), Leonard Waziri (Arusha Chini) Kamili Mmbando (Kahe Mashariki), Filbert Shayo (Marangu Magharibi) Geofrey Mkunde (Kirua vunjo kusini) Omben Massawe (Mbokomu), Frank Foy (Kimochi) na Stephen Massawe (Kibosho Mashariki).

Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti waliojitokeza ni Samuel Shao (Mwika Kaskazini), Geofrey Mkunde (Kirua vunjo kusini), Bahati Mamboma (Kibosho Kati), Innocent Shirima (Marangu Mashariki), Doren Agustine na Asia Kimaryo(Viti Maalum).

Kwa upande wa Manispaa ya Moshi, Kaimu Katibu wa CCM, Catherine Sarwatt, amesema madiwani 11 wamechukua fomu kuomba nafasi ya Umeya, huku madiwani tisa wakichukua fomu za nafasi ya Naibu Meya.

Wilayani Siha, Katibu wa CCM, Andrew Gwaje amesema madiwani wawili wameomba nafasi ya Uenyekiti wa Halmashauri na wawili wengine nafasi ya makamu mwenyekiti, ambapo mwanamke ni mmoja.

Katika Wilaya ya Hai, Katibu Hamis Kura amesema madiwani sita wamejitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti, huku mmoja akichukua fomu ya makamu mwenyekiti.

Wilayani Rombo, Katibu Masoud Melimeli amesema madiwani watatu wameomba nafasi ya uenyekiti na wanne nafasi ya makamu mwenyekiti, miongoni mwao mwanamke mmoja.

Kwa Wilaya ya Mwanga, Katibu wake, Mwadawa Maulid amesema madiwani wanane wamechukua fomu kuwania uenyekiti wa halmashauri huku mmoja akichukua fomu ya makamu mwenyekiti.

Halmashauri ya Same imeripoti jumla ya madiwani sita walioomba nafasi ya mwenyekiti na wanne walioomba nafasi ya makamu mwenyekiti.