Makada CCM katika vita mpya ya umeya, wenyeviti

Dar/Moshi. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikitoa saa 48 kwa makada wake wanaotaka kuwania umeya na wenyeviti wa halmashauri nchini kuchukua na kurejesha fomu, mvutano wa kuwania nafasi hizo umeshika kasi.

Dirsha la kuchukua na kurejesha fomu limefunguliwa kwa siku mbili kuanzia leo Alhamisi, Novemba 20, 2025 na litahimishwa kesho Ijumaa, saa 10 jioni, kisha itabaki hatua ya vikao vya chama kuteua wagombea.

Ukimya umetawala wakati wa uchukuaji na urejeshaji fomu hizo zinazotolewa katika ofisi za CCM Wilaya. Hakuna mbwembwe, wanaochukua wanakwenda kimyakimya. Maeneo mbalimbali nchini mchuano ni mkali na kila mmoja anatumia mbinu zake ili aibuke mgombea.

Baada ya dirisha kufungwa, vitafuata vikao vya kamati za siasa za wilaya na mikoa kuwajadili, kisha kupendekeza majina ya wale wanaoonekana wanafaa kwa kamati kuu ambayo itafanya uteuzi.

Taarifa ambazo Mwananchi linazo ni kwamba, baada ya kamati kuu kuteua majina ya wagombea wa umeya na wenyeviti wa halmashauri, yatapelekwa kamati za madiwani ya chama hicho ambazo zitamchagua mmoja.

Atakayechaguliwa na kamati hizo za madiwani kwa kila halmashauri, atakwenda kuchuana na wa vyama vingine kwa maeneo ambayo kuna madiwani wa upinzani.

Katika mbio hizo, mchuano umegawanyika makundi matatu, lile linalowaunga mkono waliokuwa mameya na wenyeviti wanaotaka kutetea nafasi zao na kundi jingine ni la wale waliokuwa naibu mameya na wenyeviti ambao sasa wanataka nafasi za juu.

Pia, kuna sura mpya zimechomoza kwenye udiwani ambao wamejitosa kuwania nafasi hizo. Katikati ya mbio hizo, CCM kimeonya siasa za kuchafuana na kwamba hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Onyo la CCM limetolewa na Katibu wa Oganizesheni wa chama hicho, Issa Gavu Ussi alipozungumza na Mwananchi leo, Novemba 20, 2025 kuhusu kinachoendelea ambapo amesema: “Chama chetu tunaruhusu demokrasia, lakini hakuna demokrasia inayotoa nafasi kumkashfu au kumbeza mtu.

“Tumetoa nafasi wachukue fomu, wasubiri utaratibu wa vikao, vikao wataamua viongozi wanaowataka. Sisi tunaamini tuna madiwani wenye sifa na wenye sifa za ziada watapewa nafasi.”

Katka maeneo mbalimbali, mvutano unaendelea na wengine wananyukana kwenye makundi ya kijamii ya WhatsApp kwa kila mmoja kumpigia chapuo yule anayeonekana anamuunga mkono.

Mkoani Kilimanjaro, hususan Moshi Mjini, mnyukano umekuwa mkubwa hadi chama hicho kimetoa onyo kwa wanachama wanaochochea malumbano hayo kwa kutaka utulivu na kufuata taratibu kuelekea mchakato wa kumpata mgombea atakayekalia kiti cha umeya.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amewataka wanachama kuacha kujihusisha na majadiliano yasiyo na tija kuhusu nani anafaa kuwa meya, akibainisha kuwa mchakato huo una taratibu maalumu.

“Madiwani wameshachaguliwa na bado hawajaapishwa, baada ya hapo ndipo utakuwapo mchakato wa kuchagua wenyeviti wa halmashauri, makamu wenyeviti, na kwenye manispaa tutatafuta mameya kwa kufuata taratibu.

“Uenyekiti wa halmashauri au umeya haulazimishwi, mwisho wa siku majina yatapendekezwa, utaratibu utatangazwa, watu watakwenda kuchukua fomu na watajadiliwa,” amesema Boisafi.

Boisafi amesema hakuna mwanachama au kiongozi anayeruhusiwa kujitokeza mitaani na kutangaza kumuunga mkono mtu fulani bila kufuata utaratibu wa chama.

“Asiwadanganye mtu kuwa anaweza kusimama mtaani na kusema anamtafuta au anamtaka fulani, hata mimi, kama mwenyekiti wa mkoa, sina uwezo wa kusema namtaka meya fulani kwa kuwa wanachaguliwa na madiwani wao,” amesema.

Boisafi amesema anaamini Mkoa wa Kilimanjaro utamaliza mchakato huo kwa utulivu na kwamba nafasi zote Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Meya na Naibu Meya zitapatikana kwa mujibu wa kanuni za chama.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame Haji, amesema pamoja na sababu nyingine, wanasiasa wengi huiona nafasi ya umeya kama ngazi muhimu ya kujijenga kisiasa na kuimarisha wasifu wao.

“Unajua, yule anayeanza chini hujenga uzoefu, mtandao na kutengeneza jina kwa wananchi. Hivyo, ikifika wakati wa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge, anakuwa na wasifu mzuri wa kujitangaza na kupanda ngazi zaidi,” amesema Profesa Mohamed.

Ameeleza kuanzia katika ngazi kama hiyo si jambo baya, kwani wapo wanaotumia nafasi hizo kujiimarisha kwa kufanya kazi bora ndani ya halmashauri, jambo linalowasaidia kupaa kutoka udiwani hadi kufikia ubunge.

“Ndiyo maana nafasi hizo hutazamwa kwa makini na madiwani, kila mmoja akitamani kuipata ili kuonesha uwezo wake. Wanaamini kwamba wakifanya vizuri katika nafasi hiyo, wanapata fursa tosha ya kujitangaza,” amesema.