KOCHA Mkuu wa maafande wa Transit Camp, Shadrack Nsajigwa ameweka wazi anatamani kuona soka safi likichezwa katika Ligi ya Championship hali ambayo itawavutia watazamaji wengi kama ilivyo Ligi Kuu Bara tofauti na sasa timu nyingi zinacheza soka la nguvu nyingi.
Nsajigwa alijiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Namungo, akiwa na kazi kubwa ya kuipambania kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka daraja mwaka 2006, ikimaliza mkiani kwa pointi 20, ikishinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20. Kikosi hicho kilifunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 48.
Transit Camp msimu huu katika mechi tano ilizocheza katika Ligi ya Championship, imekusanya poingi nane, sawa na nafasi iliyopo, ikishinda mbili sawa na sare ilizotoka na kupoteza moja, huku ikifunga mabao saba na kufungwa matano.
Akizungumzia tofauti kati Ligi Kuu na Championship, beki huyo wa zamani wa Yanga, Tanzania Prisons na Taifa Stars, amesema timu nyingi za Championship zinacheza kwa kupiga na kwenda zikilenga matokeo zaidi ya soka safi kutokana na presha ya kupanda daraja.
Amesema zinawaza kupanda daraja na sio kucheza vizuri, kinachotangulizwa mbele ni matokeo baadae ndio ije kucheza, akiongeza kuwa kuna haja ya waalimu kufundisha uchezaji ili iweze kuwavutia watu wengi kuja kuangalia mpira katika mechi za ligi hiyo.
“Ushindani upo, lakini matumizi ya nguvu ni makubwa sana, watu wengi wanawaza kupanda tu, hawawazi kucheza vizuri, matokeo ndiyo yanatangulia badala ya uchezaji.
“Nafikiri kuna haja kubwa ya kufundisha soka linalochezeka ili kuvutia mashabiki wengi,” amesema Nsajigwa.
Akizungumzia mwenendo wa kikosi chake kuelekea safari ya kusaka nafasi ya kurejea Ligi Kuu, amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata ugenini dhidi ya TMA Stars ya Arusha umeongeza morali ndani ya timu, na kipaumbele kwa sasa ni kurekebisha makosa aliyoyaona ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika kila mechi.
