Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameipa jukumu Tume huru ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, kusaka kiini cha tatizo hilo na kuja na mapendekezo yatakayoweka msingi wa maridhiano.
Wakati Rais Samia akitoa maelekezo hayo, baadhi ya wadau wameonyesha wasiwasi wao iwapo Tume hiyo itakuja na suluhisho la kudumu, ili kuzuia yaliyotokea yasijirudie huku wengine wakiihimiza kutafuta kwanza kiini cha vurugu hizo.
Maandamano yaliyozua vurugu siku ya uchaguzi, yalianzia Dar es Salaam na baadaye kuenea mikoa ya Arusha, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Kilimanjaro, Dodoma na Songwe.
Vurugu hizo zilisababisha taharuki na madhara katika miji mikubwa na kuzua hofu, usumbufu na kusimamisha shughuli za kila siku.
Aidha, watu ambao idadi yao haijafahamika walipoteza maisha kwenye vurugu hizo, huku mali za watu binafsi na za umma zikichomwa moto na baadhi ya watu walitumia fursa hiyo kufanya uporaji.
Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia, inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman huku ikiwa na wajumbe wengine saba ambao ni wabobevu katika masuala ya diplomasia, sheria, polisi na masuala ya utawala.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzinduliwa kwa Tume hiyo, leo Novemba 20, 2025, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema ameunda Tume hiyo kutokana na mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 2023, sura ya 32.
Amesema kutokana na kilichotokea kwenye uchaguzi, ameona kabla ya kuletewa Tume za nje, kuwe na Tume ya ndani ili ifanye kazi na zile za nje zitakapokuja, zitazungumza na Tume hii, ambayo tayari imeanza kazi.
“Kwa kifupi kilichotokea hakikutarajiwa kutokea ndani ya nchi yetu kwa sababu ya historia tuliyonayo ya usalama na utulivu wa kisiasa ndani ya nchi, hata kama kuna vipindi ambapo hatuna usalama wa kisiasa, haikufikia kiasi hiki tulichofikia,” amesema.
Amesema Tume hiyo ikikabidhiwa makabrasha ya kufanyia kazi, itapewa na hadidu za rejea za kwenda kuziangalia wakati wanafanya kazi yao, ikiwemo kutafuta kiini kilichosababisha kadhia ile.
“Vijana waliingizwa barabarani kudai haki, tunataka kujua ni haki gani ambazo vijana hawa wameikosa na kwa umoja wao waliingia barabarani kuidai haki hiyo. Purpose ya wale vijana kuingia ni haki gani ili tuweze kuzifanyia kazi na wapate haki hizo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameitaka Tume kwenda kuangalia matamshi ya vyama vya upinzani, hususani wale waliosema “lazima kiwake, hapakaliki, lazima aondoke, uchaguzi hautafanyika” na kubaini kilichowasukuma kufanya vile.
Ameongeza kuwa katika kufanya hivyo, waangalie uhusiano wa chama hicho (hakukitaja jina) na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili kubaini kama uhusiano huo ndiyo chanzo kwa yaliyotokea siku ya uchaguzi.
“Mbali na vyama vya siasa, tuangalie pia role (nafasi) za NGO’s zetu za ndani na nje. Tunaambiwa kwamba vijana wale walioingia kudai haki, walilipwa fedha kwanza ndipo wakaingia barabarani, je hizo fedha zilitoka wapi?” amehoji Rais Samia.
Ameongeza kuhoji kwamba hata kama kulikuwa na changamoto baina ya Tume ya Uchaguzi na vyama vya siasa au Msajili wa vyama vya siasa na vyama vya siasa au Serikali na vyama vya siasa, je, hakukuwa na njia nyingine nzuri zaidi za kutatua changamoto hizo hadi kuchoma nchi?
Vilevile, Rais Samia ameitaka Tume hiyo ya uchunguzi kwenda kuangalia, pia njia zilizotumika kukabiliana na vurugu zile siku ya uchaguzi hadi kusababisha vifo vya wananchi katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
“Ndiyo maana hapa ndani kuna Polisi mstaafu, Jeshi mstaafu, kwa hiyo twendeni tukaangalie njia zilizochukuliwa zilikuwaje,” amesema Rais Samia ambaye pia ni amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama.
Rais Samia amebainisha Tume hiyo itapewa hadidu za rejea pamoja na sekretarieti itakayowasaidia kutekeleza majukumu yake katika kipindi chote watakachofanya kazi huku akisema wataanza na miezi mitatu kwanza.
Amesema wakati anazindua kampeni zake za uchaguzi, aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano ili kuangalia changamoto za kisiasa nchini, lakini kwa lililotokea wakati wa uchaguzi, wameona waunde Tume hiyo kwanza ili ifanye kazi yake imalize.
“Mapendekezo yatakayotoka huku (Tume ya uchunguzi) ndiyo tutakayokwenda kuyafanyia kazi kwenye Tume ya Maridhiano. Kwa hiyo mapendekezo yenu ndiyo yatafanya ajenda za Tume ya Maridhiano,” amebainisha kiongozi huyo.
Amesisitiza kwamba ana matumaini makubwa na Tume hiyo, tofauti na vyama vingine vya upinzani, ambavyo amesikia vinaeleza kwamba havina imani nayo na vinapendekeza Tume itoke mashirika ya nje kama Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) au Umoja wa Afrika (AU).
“Mimi nina imani sana, kwa ubobevu na uzoefu wenu, nina imani sana na Tume hii na ni matumaini yangu kwamba mapendekezo yatatutoa tusogee mbele,” amesema Rais Samia.
Wakati Rais akiwa na Imani ya tume yake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Dk Ananilea Nkya yeye anaitazama kama Tume nyingine zilizopita, ambazo hufanya uchunguzi ilimradi tu ili ionekane kuna kitu kimefanyika, lakini haoni kama itatoa kitu ambacho kitalisaidia Taifa.
Amesema Tanzania imefika wakati watu wanauawa kwa sababu za kisiasa na hivyo haoni kama Tume hiyo itakuja na majibu kamili kuhusu mtanziko huo, anaodai umesababishwa na kupuuzwa kwa sauti za wananchi.
“Kwa nini watu waandamane siku ya uchaguzi? Tangu tumeanza mfumo wa vyama vingi, chaguzi zetu zilikuwaje? Tuliweka utaratibu wa haki ili kila mtu apate haki yake, lakini kumekuwa na malalamiko kila chaguzi, chanzo chake ni nini?
“Majibu ya hiyo Tume, sidhani kama yatatoa kitu ambacho kitatusaidia kama taifa. Ni kama kutupotezea ile point muhimu ya kwamba ‘watu wameuawa kwenye hayo maandamano’. Hatuwezi kuzuia vurugu kwa kupiga watu risasi,” amesema.
Dk Nkya ameongeza kuwa Tume hiyo imeundwa na Rais anayeongoza Serikali ambayo inanyooshewa kidole kwa kuua watu kwenye maandamano hayo, jambo ambalo linaondoa uhalali wake na imani kwa wananchi.
“Ukitaka Tume yoyote ifanye kazi vizuri katika jambo ambalo lina muktadha wa watawala na wananchi ambao ndiyo waathirika, Tume haiteuliwi na mtu mmoja. Mkuu wa nchi ndiye amiri jeshi mkuu, haachii nafasi hiyo wakati wa uchaguzi, anaendelea.
“Tume itakuwaje na impartiality (kutopendelea upande wowote) kama vyombo vyake ndiyo vimetekeleza mauaji hayo?” amehoji mwenyekiti huyo huku akiongeza kuwa Tume hiyo si suluhisho la mgogoro huo kwa kuwa kuna mgongano wa masilahi.
Kwa upande wake, mwanasheria mbobezi nchini, Dk Onesmo Kyauke amesema ni hatua nzuri ya kuunda Tume hiyo na ina watu wenye uzoefu wa kutosha katika masuala hayo hivyo ameitaka kwenda kuangalia kiini cha maandamano yale.
“Ukishughulikia source (kiini), kilichosababisha watu wakaenda barabarani, kama una damira ya dhati, ukishalijua hilo tatizo, itasaidia kutibu tatizo ili lisitokee tena,” amesema mwanasheria huyo.
Ameongeza kuwa maandamano hayo yametokea katika kipindi ambacho kuna udhibiti mkubwa wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari, jambo linaloonyesha kwamba kuna tatizo kubwa linahitaji kutatuliwa.
“Hizi vurugu na mauaji havikutokea huko nyuma wakati kulikuwa na uhuru mkubwa. Kwa hiyo, Tume iwe na umakini na iwe honest (wakweli) katika kutafuta chanzo na baada ya chanzo, tutatibu kile chanzo,” amesema mwanzuoni huyo.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka aliwaelezea wasifu wa wajumbe kwa ufupi akianza na Jaji Mkuu mstaafu, Othman kama mtu mashuhuri katika tasnia ya sheria, anayefahamika na kuheshimika kimataifa kutokana na uelewa wake wa masuala ya kisheria na siasa za kimataifa kwenye masuala ya utunzaji wa Amani.
Baadhi ya kazi ambazo Jaji Othman aliwahi kuzifanya mbali na Jaji Mkuu wa Tanzania (2010 – 2017), amewahi kushiriki kama mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa (UN) katika uchunguzi wa haki za binadamu Lebanon na Sudan.
Pia, amewahi kuwa mjumbe wa kupitia sheria iliyoanzisha Mahakama ya Kimtaifa ya Uhalifu (ICC), amewahi kuwa mjumbe wa tume huru ya wataalamu ya kutathmini utendaji na ufanisi wa ICC, amewahi kuwa mwendesha mashtaka katika kesi za uhalifu zilizotokea Timor Mashariki kabla ya kuwa mwenyekiti wa Tume ya Haki Jinai.
Mwingine ni Profesa Ibrahim Juma, mjumbe wa Tume ambaye alikuwa jaji mkuu wa Tanzania (2017 – 2025), aliwahi kuwa profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alisimamia mabadiliko na mifumo ya utendaji kazi wa mahakama ya Tanzania na kwa kutambua kazi hiyo, Rais alimtunukia nishani ya Muungano daraja la pili.
Mjumbe mwingine ni Balozi Ombeni Sefue, katibu mkuu kiongozi mstaafu na mwanadiplomasia mstaafu. Aliwahi kuwa katibu wa Baraza la Mawaziri, katibu wa Baraza la Usalama la Taifa na mkuu wa utumishi wa umma. Alisimamia kazi za Tume zilizoundwa na Rais wakati huo na alikuwa mjumbe Tume ya Haki jinai.
Mwingine ni Said Mwema, mjumbe wa Tume. Yeye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, akiwa IGP alisimamia maboresha makubwa ya jeshi hilo ikiwamo kuanzisha Polisi Jamii, amewahi kuwa mkuu wa kanda ndogo (Sub-Regional Bureau) ya Interpol, Nairobi, Kenya.
Luteni Jenerali Paul Meela, mjumbe wa Tume hiyo ambaye pia ni balozi na luteni jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini DRC. Akiwa Jenerali wa Jeshi, ameshiri katika misheni nyingi za kuleta amani.
Mjumbe mwingine ni Balozi David Kapya, mwanadiplomasia mwandamizi ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa katika utatuzi wa migogoro ya DRC, Sudan na Burundi.
Radhia Msuya ni mjumbe mwingine kwenye Tume hiyo. Yeye ni balozi na mwanadiplomasia mwandamizi, aliyehudumu katika mataifa mbalimbali na amewahi kutunukiwa nishani maalumu na Rais wa Ufaransa.
Mjumbe mwingine ni Dk Stergomena Tax. Ni kiongozi mwandamizi mstaafu mwenye uzoefu wa uongozi, diplomasia na utengamano wa kikanda. Amewahi kuwa katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), amehudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo uwaziri wa ulinzi.
Mjumbe wa tisa katika Tume hiyo ni George Madafa, ofisa mwandamizi wa Serikali mstaafu, amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.
Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Kusiluka amemhakikishia Rais Samia na Tume hiyo kwamba ofisi yake itaiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa malengo kusudiwa bila kikwazo chochote.
