Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuiimarisha Wizara ya Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana kwa kuteua viongozi wengine wawili.
Wizara hiyo mpya inayoongozwa na Waziri, Dk Joel Nanauka imeanzishwa mahususi kwa ajili ya kuimarisha sera, mipango na uratibu wa masuala ya vijana nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Novemba 20, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, walioteuliwa ni Jenifa Omolo ambaye sasa atakuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa ofisi hiyo. Awali, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.
Pia, Rais Samia amemteua Dk Kedmon Mapana kuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo. Awali, Dk Mapana alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), taasisi inayohusisha kwa karibu vijana kupitia sekta ya sanaa na ubunifu.
Dk Mapana aliteuliwa na Rais Samia kuwa katibu mtendaji wa Basata Julai 10, 2022 akichukua nafasi ya Godfrey Mngereza ambaye alifariki dunia Desemba 24, 2020 jijini Dodoma.
Dk Mapana pia aliwahi kuwa mhadhiri mkuu, Idara ya Sanaa Bunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika hotuba yake ya kulizindua Bunge 13, Novemba 14, 2025, Rais Samia alisema kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu nchini ni vijana, Serikali itaweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, viongozi hao wataapishwa kesho Ijumaa Novemba 21, 2025, Ikulu Chamwino, saa 8:00 mchana.
