Straika Mnigeria ampa Sowah maujanja

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Stand United, Mbeya City na Pamba, Abasirim Chidiebere amemsifu nyota wa Simba, Jonathan Sowah akiamini straika huyo atafanya vizuri kama atashikilia hapo alipoanzia.

Hata hivyo, Chidiebere alimtahadharisha Sowah raia wa Ghana, kuhakikisha kila nafasi anayoipata afunge mabao ili kuwa na makali na tishio katika ligi.

Chidiebere ambaye ni raia wa Nigeria, kwa sasa anaishi jijini Mwanza baada ya kustaafu soka na alikiri Sowah ni mshambuliaji hatari na tayari ameonyesha hilo tangu alipotua Ligi Kuu.

Sowah alitua Tanzania msimu uliopita akijiunga na Singida Black Stars kipindi cha usajili wa dirisha dogo na kufunga mabao 13 katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara.

SOW 01

Kiwango alichokionyesha, kimeifanya Simba kumsajili msimu huu na tayari ameanza kuteka hisia za mashabiki wa Msimbazi.

Akizungumza jijini Mwanza, Chidiebere amesema ili mshambuliaji huyo awe hatari anapaswa kufunga mabao na kutoa asisti walau katika kila nafasi mbili kati ya tatu anazopata.

“Unajua ukitaka kuwa straika mzuri unatakiwa ukipata nafasi hata tatu basi ufunge mbili au moja na hiyo nyingine utengeneze asisti kwa kila mechi,” amesema Chidiebere na kuongeza;

“Unatakiwa uonyeshe ubora wako. Sowah ni mchezaji mzuri, sina mashaka naye.”

Licha ya ushindani wa namba kwa washambuliaji Simba kati ya Sowah, Seleman Mwalimu na Steven Mukwala, mchezaji huyo amesema mastraika wote watatu ni wazuri, hivyo kocha ana kibarua cha kuwatumia wote kulingana na mbinu na aina ya mpinzani wanayekutana naye.

SOW 02

Amesema kilichofanywa na Sowah msimu uliopita akiwa na Singida BS licha ya kuingia dirisha dogo kimetosha kumwelezea ni mchezaji wa aina gani na namna gani alivyo tishio kwa wapinzani.

“Kama amepata nafasi ya kuwa kwenye timu kubwa kama Simba bila shaka ubora wake sioni kama ni mchezaji mbaya. Na kama mmeona ameshaanza kuingia kwenye mfumo wa timu taratibu,” amesema Chidiebere na kuongeza;

“Katika msimu wake wa kwanza tayari ameshaanza kuzoea mazingira kujua jinsi Simba wanavyocheza. Ni mchezaji mzuri.”