Tahadhari muhimu mauzo ya dhahabu yakizidi kupaa

Dar es Salaam. Dhahabu imeendelea kuwa moja ya chanzo kikubwa cha kuuingizia Tanzania fedha za kigeni baada ya mauzo yake kufikia Sh10.82 trilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2025, Ripoti ya Benki Kuu inaeleza (BoT).

Ripoti hiyo ya tathmini ya kila mwezi inaonyesha kuwa mauzo hayo ni ongezeko kutoka Sh7.97 trilioni iliyokuwapo kipindi kama hicho mwaka uliotangulia jambo ambalo lilichochewa na ongezeko la bei katika soko la dunia.

Kuongezeka kwa mauzo ya madini kumetajwa pia katika ripoti hii kuwa sababu ya ongezeko la mapato ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje.

Uuzaji wa bidhaa nje ya nchi ulifikia zaidi ya Sh24.707 trilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2025 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh20.09 trilioni kipindi kilichotangulia.

Ripoti hii inabainisha kuwa mbali na dhahabu bidhaa nyingine zilizochangia kukua kwa mapato haya ni bidhaa zilizotengenezwa viwandani, korosho, nafaka na tumbaku.

Mauzo ya nje ya bidhaa za asili pia yalipanda hadi kufikia Sh3.622 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.3 ikichochewa zaidi na ongezeko la mauzo ya korosho na tumbaku. Bidhaa hizo zilibebwa na ongezeko la bei yake sokoni na kiasi kilichouzwa.

Mauzo ya nje ya nafaka pia yaliongezeka hadi Sh831.534 bilioni kutoka Sh474.116 bilioni kutokana na ongezeko la mahitaji kutoka nchi jirani.

Katika hilo, Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo amesema dhahabu ni kama baraka kwa nchi wakati ambao bei yake imepanda katika soko la dunia.

“Inaweza kuwa na faida kubwa lakini inaweza kuwa na hasara kama tukijisahau na kuendelea kuiwekea mikakati wakati uchumi wetu hautakiwi kutegemea bidhaa moja, madini hayadumu milele ukiyachimba yanaisha bei yake kwenye soko la dunia inapanda na kushuka hivyo hauwezi kuyatumia kama kitu cha kujipiga kifua na kuweka mikakati yako kwenye madini,” amesema.

Alitoa angalizo kuwa bei ya dhahabu haitakuwa juu milele hivyo ni vyema kuboresha sekta nyingine kupitia madini huku akiwa hakubaliani na uanzishaji wa mfuko wa sekta ya madini kwani yana mwisho na bei yake inapanda na kushuka.

“Nchi zilizoendelea katika sekta yoyote ile hasa zile za uziduaji kama madini na mafuta wamekuwa wakizitumia kuboresha sekta nyingine zinazodumu ndiyo maana Dubai wanajua wana mafuta lakini wanajenga miundombinu, hospitali ili hata mafuta yakiisha hivyo vitu vitakuwapo,” amesema.

Amesema ni vyema kutumia madini kuboresha sekta nyingine kama kilimo, utalii, viwanda, elimu, afya, miundombinu vitu ambavyo ni vya kudumu kwani vitaendelea kuwapo milele.

Mchambuzi wa uchumi, Christopher Makombe amesema kuongezeka kwa bei ya dhahabu inamaanisha kuwa Tanzania hupata dola nyingi za Marekani kutokana na mauzo ya nje, jambo ambalo huimarisha ukuaji wa akiba ya fedha za kigeni na kusaidia kuleta uthabiti wa shilingi.

“Hii inaweza kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei linalosababishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hasa mafuta na mashine,” amesema.

Amesema kadiri bei zinavyopanda, kampuni za madini hupata faida kubwa zaidi, hali inayoongeza kiasi cha kodi kinacholipwa serikalini wakati ambao kupanda kwa bei kunavutia wawekezaji wapya katika uchimbaji, utafutaji na uchakataji wa madini.

“Tanzania inaweza kushuhudia upanuzi wa migodi iliyopo, utoaji wa leseni mpya za madini na kuvutia wawekezaji wa kimataifa. Hii itasaidia kuongezeka kwa upanuzi wa shughuli za madini ambazo zitaongeza mahitaji ya wafanyakazi pamoja na wazabuni wa huduma mbalimbali ikiwamo usafirishaji, chakula, uhandisi na huduma nyingine za usaidizi,” amesema.

Bei za juu za dhahabu pia zinaweza kuongeza kiwango cha mapato cha wachimbaji wadogo, hivyo kuboresha maisha ya kaya za vijijini na kupunguza umaskini hali itakayochochea kusisimka kwa sekta kama uchakataji wa dhahabu, benki, bima na usafirishaji. Hata hivyo, kutegemea sana mapato ya dhahabu kunaweza kuiathiri nchi endapo bei za kimataifa zitashuka hivyo uanuwai wa vyanzo vya uchumi ni muhimu kwa maendeleo endelevu.