Tanzania matumaini kibao Kombe la Dunia Futsal

TIMU ya Taifa ya Tanzania ya Soka Wanawake ya Futsal, imewasili nchini Ufilipino huku ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Futsal yatakayoanza kesho Ijumaa Novemba 21, 2025.

Mashindano hayo yatakayofanyika nchini Ufilipino yakitarajiwa kufikia tamati Desemba 7, 2025, yanajumuisha timu 16, huku Tanzania ikipangwa kundi C na timu za Ureno, Japan na New Zealand.

Kundi A liko na wenyeji Ufilipino, Poland, Morocco na Argentina. Kundi B ni Hispania, Thailand, Colombia na Canada, huku kundi D likiwa na mabingwa wa zamani Brazil, Iran, Italia na Panama. 

Ratiba inaonyesha Tanzania itaanza kampeni hizo dhidi ya Ureno, Novemba 23, 2025, kisha dhidi ya New Zealand (Novemba 26, 2025) na kumaliza makundi Novemba 29, 2025 dhidi ya Japan, mechi zote zikipigwa Philsports Arena Pasig.

FUT 01

Kocha mkuu wa timu hiyo, Curtis Reid, amesema mabinti hao wako tayari kuchuana kwenye mashindano hayo ili kuhakikisha wanaweka rekodi nyingine kwa upande wa Kombe la Dunia.

“Tulikuwa na mechi mbili za kirafiki, zilitupa taswira ya timu yetu kuwa iko tayari kwa ajili ya kushindana na timu zingine, tunaamini tumepata uzoefu kidogo wa mchezo huu,” amesema Reid.

Mkuu wa Msafara, Zena Chande amesema licha ya ugumu wa kundi hilo, lakini ana imani Tanzania itafanya vizuri kutokana na ubora uliionyesha tangu kwenye hatua za kufuzu.

“Tuna kundi gumu lakini tuna imani ya kufanya vizuri na tumekuja huku kufanya vizuri, tumejiandaa tukiwa na imani kwamba tutaonyesha upinzani mkubwa kutokana na kikosi chetu,” amesema.

SAFARI YAO
Tanzania na Morocco ndio timu pekee kutoka Afrika kufuzu mashindano hayo, ikiwa mara ya kwanza kwa CAF kuanzisha mashindano hayo lakini kwa duniani hii ni mara ya pili baada ya kufanyika 2010 nchini Hispania ambako Brazil ilitwaa ubingwa huo.

Tanzania ilifuzu kucheza mashindano hayo baada ya kufika fainali ambayo ilipoteza dhidi ya Morocco kwa mabao 4-3, hivyo bingwa na aliyeshika nafasi ya pili wamefuzu moja kwa moja.

FUT 02

Fainali za Mataifa ya Afrika za Futsal ambazo zimetumika kuzipata timu hizo mbili, zilifanyika nchini Morocco kuanzia Aprili 22, 2025 hadi Aprili 30, 2025.

Kwa Afrika, hii ilikuwa mara ya kwanza mashindano ya Futsal kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) upande wa wanawake. Mataifa tisa yalishiriki ambapo Tanzania ilipangwa kundi C na Madagascar na Senegal, huku kundi B likiwa na Angola, Misri na Guinea, wakati Kundi A likiwa na wwenyeji wa mashindano hayo Morocco, Cameroon na Namibia.

Katika Bara la Ulaya, UEFA ilizindua mashindano ya kwanza ya Futsal kwa Wanawake Februari 2019, yakihusisha timu kutoka mataifa manne, Hispania, Ureno, Urusi na Ukraine.