Wafanyabiashara watakaonunua parachichi mashambani kudhibitiwa Rungwe

Mbeya. Katika jitihada za   kudhibiti wanunuzi holela wa zao la Parachichi mashambani ,Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya,  imekuja na mkakati wa kuanza ujenzi wa mradi wa vituo saba vya kukusanyia  kabla ya kuingizwa sokoni.

Mradi unatekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana halmashauri hiyo, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).

Imeelezwa kati ya vituo saba,viwili vinajengwa Busokelo na vitano  Rungwe mkoani hapa kwa lengo la kuwezesha wakulima kuwa na sehemu moja ya kuuzia ili kudhibiti walanguzi wanao wafuata mashambani.

Akizungumza na Mwananchi  Digital  leo Jumatano Novemba 19, 2025,Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Rungwe, Adam Salum amesema ujio wa mradi utakuwa suluhisho kwa wakulima kuzalisha kwa tija na kuuza zao la parachichi kwa bei nzuri ya kujikwamua kiuchumi.

“Tayari mradi huo umeanza katika halmashauri mbili za Busokelo na Rungwe, lakini ukikamilika utakuwa chachu ya wakulima  kujiongezea mapato na kuchangia mapato ya halmashauri,” amesema.

Salum amesema  kwa kipindi  cha mwaka  2024/2025 ,uzalishaji  wa  parachichi  meongezeka kutoka wastani wa tani 25,866 mpaka 30,642, sawa na asilimia 64.7.

Amesema ongezeko hilo limetokana na mwitikia mkubwa wa wakulima kuwekeza kwenye kilimo  sambamba na elimu ya wataalamu katika kuandaa vitalu vya miche mpaka hatua ya uzalishaji.

“Mwitikio ni mkubwa licha ya hapo awali kuwepo kwa changamoto ya masoko makubwa ya nje, lakini Serikali inaendelea kuona namna bora ya kuwasaidia hususani ujenzi wa miundombinu ya kisasa yenye baridi na viwanda vidogo vya kuongeza thamani,”amesema.

Kuhusu kuchangia mapato ya halmashauri

Amesema kwa msimu uliopita zao hilo lilichangia mapato ya halmashauri zaidi ya Sh400 milioni ambazo zilielekezwa kwenye miradi mbalimbali  hususani ujenzi  wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Avocado.

“Parachichi ni zao kuu linalo changia mapato ambayo tunaelekeza kwenye miradi mbalimbali  ya maendeleo sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara  ili kurahisisha  usafirishaji kufikisha sokoni,” amesema.

Mkulima wa parachichi Kata ya Kiwira, Estrida Joel amesema endapo  Serikali ikaharakisha ujenzi wa vituo hivyo utakuwa mkombozi kwao kwani kuna kipindi mazao hufika kuharibika kwa kukosa masoko na hata ukipata tunauza bei rahisi.

“Yani kimsingi tumekuwa tukinyony’wa na wanunuzi kwa kujipangia bei wakifika  mashambani jambo ambalo tunalazimika kukubaliana nao kwani hakuna masoko ya uhakika na kuomba Serikali kuwatafutia masoko mbadala wakati ujenzi wa vituo ukiendelea,”amesema.