Wananchi wapiga mawe gari ya Zimamoto, DC aingilia kati

Shinyanga. Novemba 19, 2025 saa 12 jioni nyumba yenye makazi ya watu na biashara iliyopo maeneo ya Mnara wa Voda, mkoani Shinyanga iliteketea kwa moto.

Wananchi walifanikiwa kuuzima moto huo wakidai gari la zimamoto lilichelewa kufika eneo la tukio na kuchukua hatua ya kulishambulia kwa mawe.

Wakizungumza Novemba 19, 2025 baadhi ya mashuhuda na waathirika wa ajali hiyo wameeleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kuondoa watu kwa silaha wakidai  hao ndio waliotoa msaada mkubwa katika kuokoa mali zilizokuwa ndani ya nyimba iliyokuwa inawaka moto.

“Watu hawa wamekuja baada ya mimi kupiga kelele kuomba msaada, wametoa msaada mkubwa katika kuokoa vitu pamoja na kuzimamoto, nimepigia zimamoto muda mrefu sana hawaonekani na ofisi ya ilipo sio mbali na hapa, ni hapo tu nyuma ya shule, kwa hiyo ni kosa wao kuja kuokoa hadi polisi waanze kuwapiga mabomu,” amesema Zainab Shaban.

“Moto ulianza saa 11 jioni, zimamoto tumewafuata ofisini kwao wanasema tunakuja! tunakuja! Tukaanza kuokoa chumba hadi chumba na baadhi ya vyumba vimeteketea, lakini tumeshangaa askari wanafika wanaanza kupiga watu mabomu wakati vitu hivi vyote vimeokolewa na watu, hapa kuna watoto, wenye presha na wazee vipi kama wangeumiza watu,” amehoji Said Ramadhan.

Mmoja wa ndugu wa familia iliyopata ajali, Baby Mohammed ameeleza kuwa alipigiwa simu akiwa kwake wakati anakuja alipita ofisi ya zimamoto kuomba msaada lakini   gari la zimamoto likawa haliwaki.

“Nyumba iliyoteketea moto ni ya baba mdogo, nilipigiwa simu nikiwa nyumba Ndala, nikiwa njia nakuja nikapita zimamoto kuomba msaada wa gari, wakasema linagoma kuwaka baadaye likawaka ndio wakaja, wakati nafika hapo nimekuta moto umepungua, nawashukuru wananchi kwa juhudi zao za uokoaji japo mzigo mkubwa umeteketea, hii nyumba ina vyumba vitano vya kuishi upande wa nyuma na mbele vyumba vitano vya biashara,” amedai Baby.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amewaonya vijana kutorudia tena kushambulia gari la zimamoto kwa sababu likiharibika hakutakuwa na msaada wa chombo za kuzimia moto, na bado litanunuliwa kwa kodi za wananchi itakuwa ni hasara.

“Familia iliyoathirika itapatiwa msaada na kilichotokea leo kisijirudie kuna watu wachache ambao wameanzisha na wengine wakafuta mkumbo, hapa katika wilaya yetu kuna gari moja tu la zimamoto tusichukue hatua mkononi bila ya kujua ni changamoto zipi zimetokea, na hapa katika eneo hilihili ni mara ya pili baada ya miezi michache tukio kama hili linatokea, nimetoa maagizo kwa kamati husika kufanya uchunguzi,” amesema Mtatiro.

Pia amesema, “Nawaambia kwa sababu ni kama vijana wenzangu kuna watu wamepanga kufanya maandamano Desemba 9, nawaombeni kuweni watulivu kama mlivyofanya kipindi kilichopita msifuate mkumbo, mkifuata mkumbo tutakaa nyumbani hakuna shughuli zitakazo endelea na wafanyabiashara tutapata hasara.

Aidha, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema askari watakuwa eneo la tukio kwa kulinda wananchi na mali zao hasa kwa mali ambazo zimeokolewa.

“Tuko hapa eneo la tukio kuweka ulinzi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zilizookolewa, lakini Jeshi la Zimamoto litafanya uchunguzi kujua chanzo cha ajali hiyo ya moto ni nini, pia tunapita kwa familia kujua na kufanya tathmini ya vitu gani vilivyoharibika na kwa kiasi gani,” amesema Magomi.