Dodoma. Kama ingekuwa ni sherehe ya kawaida, basi kila mmoja angetamani vazi jeusi liendelee kuvaliwa, hasa walipofika watu wengi katika Viwanja vya Chinangali jijini
Hata hivyo, ulikuwa ni msiba. Wanasiasa, viongozi wa dini, wasanii na vyombo vya ulinzi walijaa katika viwanja hivyo ambako kulikuwa na msiba wa kuaga mwili wa Emmanuel Mathias, msanii na mchekeshaji maarufu, kabla ya kuelekea makaburini.
Watu wengi walilia, walihuzunika, lakini maneno ya wasanii Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji) na Sylvester Mujuni (Mpoki) yaliwatoa waombolezaji kwenye simanzi na kuwafanya watabasamu, ingawa walikuwa wakitoa ujumbe mzito.
Ni leo Alhamisi, Novemba 20, 2025, katika ibada ya maziko ya msanii na mchekeshaji huyo maarufu, MC Pilipili, ambayo imewakutanisha mamia ya watu maarufu, wasanii, viongozi wa dini na siasa.
MC Pilipili alifariki dunia siku ya Jumapili, Novemba 16, 2025. Taarifa za madaktari na Jeshi la Polisi zimethibitisha kuwa kifo chake kilitokana na kupigwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, juzi alitangaza kuwa kifo cha Pilipili hakikuwa cha kawaida na kinaonekana kilisababishwa na kupigwa.
Awali, kaka wa MC Pilipili, Mchungaji Christopher Mathias, alisema mwili wa mdogo wake ulikutwa na majeraha sehemu mbalimbali ikiwamo mgongoni na mabegani.
Akizungumza leo wakati wa kutoa shukrani, Mchungaji Christopher amesema kuwa kila jambo lililotokea kuhusiana na msiba huo wanalikabidhi kwa Mungu, na asingependa kuzungumza mambo mengi.
“Miaka mitatu iliyopita tulimpoteza mama yetu, na mimi nilijua kwa namna yoyote ningetangulia wao niwaache, sikutegemea kuwa mdogo wangu angeniacha, lakini ni mapenzi ya Mungu, asanteni sana Serikali, wananchi wa Dodoma, Watanzania na wasanii wenzake, Emmanuel aliwapenda Watanzania sana, niseme tu Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” amesema Mchungaji Christopher.
Leo baadhi ya wasanii walipewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi. Lucas Mhuvile (Joti) alishindwa kusema chochote; alianza kufuta machozi na ndipo akashushwa kutoka mimbarini.
Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji) amewataka wasanii kuishi wakimtazama Mungu na kujenga uhusiano mzuri Naye kwa kuwa hawajui nani anafuata.
Huku akiimba wimbo wa dini na baadaye wa Samba Mapangala, alimalizia kwa kumuonesha Joti na kusema, “Moja ya wanaonipasua kichwa ni hawa,” jambo lililowafanya waombolezaji kuanza kucheka.
Mchekeshaji Sylvester Mujuni ‘Mpoki’ amesema bado anashangazwa kuona Jeshi la Polisi halijasema kama watuhumiwa wameshakamatwa.
“Sitakiwa kuwaingilia lakini wakati tunazika leo nilitamani kuambiwa kuwa watuhumiwa wako jela maana kulikuwa na simu iliyompigia MC Pilipili na kumtaka wakutane, sasa siingilii kazi yao ila ukweli leo tungeambiwa wako ndani,” amesema Mpoki.
Hata hivyo, naye aliwakosoa wanasiasa na viongozi akiwataka wawe wepesi kupokea simu kwa kuwa wakati mwingine wanapigiwa kwa lengo la kupewa ushauri juu ya mambo muhimu.
Amesema baadhi ya waliokuwepo walifika hapo kwa sababu ya kazi za sanaa, jambo lililoibua shangwe na makofi.
Spika wa Bunge mstaafu, Dk Tulia Ackson amesema kifo cha MC Pilipili kimekuwa cha ghafla sana na kimezua maswali mengi.
Dk Tulia amewaomba Watanzania kuishi kwa kupendana na kusameheana, lakini akasisitiza haki na kuwaomba wote wenye nia njema kumuunga mkono mbunge wa Mtumba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika kutoa michango ili kufanikisha mpango wa kuwasomesha watoto wawili wa marehemu ambao amewaacha.
Hata hivyo, Mavunde amesema tangu walipopata msiba wameshikwa mkono na watu mbalimbali, lakini Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kusaidia shughuli zote zilizokuwa zikiendelea.
Mapema Mavunde alitangaza kuomba kuungwa mkono kwa ajili ya kuwasomesha watoto wa MC Pilipili ambao amewaacha ili kusudi ndoto zao zitimie.
Naibu Waziri wa Michezo, Hamisi Mwijuma (Mwana FA) amesema kifo ni ukumbusho, unaotaka kila mmoja aishi kwa kumuogopa Mungu kwa kuwa, kila aliyezaliwa lazima awe na uhakika wa kufa.
Mwana FA ameomba kila mmoja aishi vizuri duniani bila kumkanyaga mwingine kichwani kwa kuwa maisha ya mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake siyo nyingi nazo zimejaa tabu.
