Aliyemuua ndugu yake wakicheza ngoma ya kisukuma jela miaka miwili

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dodoma, imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela, Sandu Nkingwa baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya bila kukusudia ya ndugu yake, Adam Nkingwa.

Tukio hilo lilitokea Januari 3, 2024 katika Kijiji cha Mpugizi, Kata ya Mwaru, wilayani Ikungi mkoani Singida, wakati ndugu hao wawili wakicheza ngoma ya asili ya ‘Kisukuma’ ya kuchapana fimbo.

Ilidaiwa wakati wa kucheza, Sandu alimpiga Adam fimbo ya kichwani na kusababisha kuanguka chini ambapo licha ya kupewa dawa za kutuliza maumivu na kupelekwa hospitali, alifariki dunia.

Hukumu hiyo imetolewa Novemba  19, 2025 na Jaji Evaristo Longopa, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji namba 15168/2024 na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Longopa amesema baada ya Sangu kukiri kusababisha kifo bila kukududia ,Mahakama inamhukumu kifungo hicho cha miaka miwili jela baada ya kumpunguzia kutoka miaka minne ambayo ni adhabu ya chini ya kosa hilo la kuua bila kukusudia.

Kwa mujibu wa mashtaka, Sandu alishtakiwa kwa kosa la mauaji bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, ambapo kutokana na jeraha hilo Januari 4, 2024 Adam alifariki dunia.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo ambaye alithibitisha kuwa kifo hicho kilitokana na jeraha la kiwewe cha ubongo.

Baada ya Sandu kukamatwa, Januari 2, 2024 na kuhojiwa Polisi, alikiri kumuua ndugu yake bila kukusudia ambapo alifikishwa mahakamani kujibu kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Foibe Malecela, alieleza mahakama kuwa mshtakiwa hana rekodi za uhalifu ila aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kupunguza mila na desturi zinazoweza kusababisha kifo na kuwa marehemu alikuwa kijana mdogo hivyo kukatishwa uhai wake kinyume cha sheria kumesababisha taifa kupoteza nguvukazi.

Wakili huyo aliieleza mahakama kuwa kila mwanadamu amepewa haki ya kufurahia haki ya kuishi. Hivyo, mshtakiwa  alipaswa kuchukua hatua za tahadhari ili asimdhuru mwathirika wa tukio hilo ambaye alikuwa ndugu yake.

Wakili wa utetezi, Peter Ndimbo aliiomba mahakama kumpunguzia mteja wake adhabu kwa sababu alikuwa mkosaji wa kwanza, alikiri kosa tangu siku ya kwanza hivyo kuokoa muda na rasilimali za serikali.

Sababu nyingine ni kifo kilitokea katika uchezaji wa ngoma za kitamaduni na kuwa hakukuwa na nia hata kidogo ya kujeruhi au kuua na kwa kuwa mshtakiwa amekaa mahabusu zaidi ya mwaka mmoja amepata somo na ana mke na watoto chini ya miaka nane, ambao wanamtegemea.

Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili Jaji Longopa, amesema Mahakama imezingatia mazingira ya kosa lilivyofanyika na baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, suala kuu ka mtazamo wake ni kuzingatia hukumu inayofaa.

Jaji huyo amesema kutokana na mazingira ya mauaji hayo kuwa ilikuwa ni kucheza ngoma ya asili kwa kutumia fimbo na siyo kupigana, katika mazingira ya jambo hilo, Mahakama imeridhika kwamba mauaji hayo yalitokea bila kukusudiwa ingawa marehemu alipigwa kichwani.

Jaji Longopa amesema ni sheria kuwa kutokana na sababu fulani, kunaweza kusababisha kupunguzwa kwa adhabu baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukiri kuua bila kukusudia.

“Kwa kuzingatia mazingira hayo kwenye kumbukumbu, mahakama hii ina mwelekeo wa kuona kwamba mhalifu huyu anastahili kuhurumiwa na Mahakama.

Alichukua hatua zote zinazowezekana kuhakikisha kuwa mwathirika yuko salama kwa kutumia juhudi zote kuhakikisha usalama wa mwathiriwa,” amesema na kuongeza

“Ikiwemo kusimamia apate dawa za maumivu, kumpeleka hospitalini kuliashiria hakuwa na nia ya kutenda kosa hilo. Mahakama itampunguzia muda wa mwaka mmoja kutoka kifungo cha miaka minne kilichotarajiwa kwani ameonyesha kujuta, ushirikiano aliotoa,”

Jaji Longopa amesema pamoja na mazingira ya kosa yalivyotokea, Mahakama inapunguza muda wa mwaka mmoja aliokaa mahabusu hivyo kumpunguzia miaka miwili na kumhukumu kutumikia miaka miwili.