Benjamin Ratsim afanya yale yale ya Bayi

MWANARIADHA chipukizi Benjamin Ratsim amekuwa Mtanzania wa pili kuvunja rekodi ya dunia, baada ya kuweka alama mpya katika mbio za barabarani za Km 15 kwa wanariadha walio chini ya umri wa miaka 20.

Nyota huyo alifikia rekodi hiyo baada ya kutamba katika mbio za Zevenheuvenloop 15 Km huko Uholanzi zilizofanyika Novemba 16, akimaliza wa tatu kwa dakika 41:51 na kupiku muda wa dakika 42:00 uliowekwa 2017 na Mkenya Mathew Kimeli katika mbio za 15 Km du Puy-en-Velay zilizofanyika Ufaransa, wakati huo akiwa na umri wa miaka 19.

Kwa kuvunja rekodi hiyo, Benjamin amejiunga na orodha ndogo ya mabingwa waliowahi kuipeperusha Tanzania kimataifa, akifuata nyayo za gwiji Filbert Bayi ambaye 1974, alivunja rekodi ya dunia ya mita 1500 katika michezo ya Madola iliyofanyika New Zealand, akitimka kwa dakika 3:38 akiwa na umri wa miaka 20, rekodi ambayo imedumu hadi leo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye anatokea kambi ya Madunga iliyopo wilayani Babati, Manyara pia amevunja rekodi ya taifa ya km 15 kwa upande wa wanaume iliyokuwa inashikiliwa nyota Gabriel Geay aliyoiweka mwaka 2020 kupitia mbio za Boston za Marekani kwa muda wa 42:15.

Akiongea na Mwanaspoti amesema bado ana njaa ya kuweka rekodi nyingi zaidi, atajituma na kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania, huku akiongeza kuwa siri ya mafanikio ni usimamizi mzuri kutoka kwa mlezi wake Gabriel Geay.

“Kiu yangu kubwa kwa sasa ni kufanya vizuri katika mashindano ya dunia ya mbio za nyika ambazo zitafanyika nchini Marekani mwakani, naamini nitaenda kufanya kweli,” amesema Benjamin.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John, amesema kwa sasa wanasubiri tu uthibitisho wa Shirikisho la Riadha la Dunia, ili rekodi hiyo iweze kutambuliwa kwani kwa sasa bado hajatambuliwa (recognise).

“Zile mbio ni kubwa na zinatambuliwa matumaini yetu ni hivi karibuni, Benjamin atatambulika kama mwanariadha mwenye umri chini ya miaka 20 mwenye rekodi ya dunia,” amesema Rogath.