Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa imeanza kuandaa kanuni mahususi zitakazodhibiti wakopeshaji wa mitandaoni wanaotoa huduma zao bila kufuata taratibu, ikiwemo kutosajiliwa rasmi kama inavyotakiwa kisheria.
Hatua hii imekuja kufuatia malalamiko lukuki kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakitozwa riba kubwa kupita kiasi na hata kudhalilishwa hadharani kupitia simu au mitandao ya kijamii wanapochelewa kulipa mikopo yao.
Vitendo hivyo vimetajwa kuathiri utu na usalama wa watumiaji wa huduma hizo.
Wakati wa vikao vya Bunge la 12, wabunge kadhaa walilalamikia kwa ukali mwenendo huo wa wakopeshaji wa mitandaoni.
Afisa Sheria Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhan Myonga akitoa wasilisho lake katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.
Walisema kumekuwa na ongezeko la taarifa za wananchi kupigiwa simu na kutukanwa, au taarifa zao binafsi kusambazwa kwa ndugu, majirani na kwenye makundi ya mitandaoni kama njia ya kushinikizwa kulipa madeni.
Wabunge walishinikiza BoT na Serikali kuchukua hatua za haraka ili kulinda haki na usalama wa raia, wakisisitiza kuwa shughuli za mikopo lazima ziendeshwe kwa kufuata sheria na maadili ya kifedha.
Hatua ya BoT kuanza kuandaa kanuni hizi mpya inakuja pia siku chache baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa “Sema na BoT”, unaowawezesha wakopaji kuwasilisha taarifa au malalamiko kuhusu programu na taasisi za utoaji mikopo ya mtandaoni zinazokiuka taratibu.
Hayo yamesemwa jana na Ofisa Sheria Mwandamizi kutika Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Kifedha kutoka BoT, Ramadhan Myonga wakati akitoa mada katika mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari yanayofanyika jijini hapa.
Akizungumza katika mafunzo hayo Myonga amesema mara zote mtumiaji wa huduma za kifedha amekuwa akilindwa kwa taratibu, kanuni, miongozo na sera za fedha ili awe salama.
Amesema changamoto iliyopo ni soko la programu za mikopo mitandaoni linategemea sana majukwaa ya kampuni kama Google, ambayo inaweza kuruhusu programu kufanya kazi bila usimamizi wa BoT.
Hapo awali, BoT ilikubaliana na Google kwamba programu yoyote isipandishwe kwenye mtandao bila uwepo wa ruhusa kutoka BoT (letter of no objection) hata hivyo, baadhi ya programu bado zimekuwa zikipenya kupitia Google kinyume na makubaliano yaliyopo ya Google na BoT.
“Hata hii hatua ya kuanza kutoa barua ya kutokuwa na pingamizi la mtoa huduma kuendeaha shughuli zake haijaweza kumaliza tatizo, hivyo tuko katika hatua za ndani za maandalizi ili tuje na kanuni hizi ambazo zitakuwa suluhisho ya kudumu,” amesema.
Licha ya malalamiko mengi ya umma kuhusu uendeshaji usiozingatia kanuni za ukopeshaji unaofanywa na programu hizi, Myonga amesema kuwa BoT haina mamlaka juu ya taasisi ambazo hazijasajiliwa.
“Watumiaji wanapaswa kufuata taratibu za kisheria na kutoa taarifa wanapokutana na uendeshaji usiovutia. Ili kutambua taasisi zilizosajiliwa, tembelea tovuti yetu ambayo ni www.bot.go.tz,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa mifumo na taratibu za kisheria zinazolinda haki za watumiaji na kuhakikisha uwajibikaji wa watoa huduma za kifedha.
Hii ni pamoja utekelezaji wa Kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (za Ulinzi wa Wateja wa Huduma za Kifedha) za mwaka 2018, GN Na. 883 ya 2019.
Myonga pia alibainisha kuwa dawati la malalamiko la BoT, ambalo limepewa jukumu la kuhimiza uwazi na uadilifu katika sekta ya fedha, lilianza kufanya kazi Juni 5, 2024.
Vipaumbele vyake ni pamoja na kuhakikisha mbinu za masoko na uuzaji zinazokubalika, ukusanyaji wa madeni kwa maadili, uadilifu wa wafanyakazi, faragha ya taarifa, na utatuzi wa migogoro kwa ufanisi.
Pia, kupitia Sema na BoT wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko na ushahidi kwa njia ya kielekroniki wa ambao unapatikana katika tovuti ya Benki kuu ya Tanzania.
Mtu akiingia hapo ataona kiunganishi (link) na malalamiko yake yatapokelewa na kufanyiwa kazi. Kupitia mfumo huo pia mtu anaweza kujua kama kampuni aliyokopa imesajiliwa au la.
Haya yanasemwa wakati ambao Novemba 21, 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilitangaza kuzifungia kutoa mikopo programu tumizi (application) 69 baada ya kuzi
baini zinaendesha shughuli hiyo kidijitali bila kuwa na leseni wala idhini. Kupitia taarifa ya ufutaji programu hizo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alibainishwa kuwa majukwaa na programu hizo zimeshindwa kukidhi matakwa ya mwongozo kwa watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili kwa wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024, uliotolewa na Benki Kuu Agosti 27, 2024.
