KIPA wa Mtibwa Sugar, Costantine Malimi amesimama langoni katika mechi nne kati ya tano ilizocheza timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akizitaja Yanga na Dodoma Jiji kuwa ni ngumu kuzisahau kwa jinsi zilivyomtoa jasho uwanjani.
Katika mechi hiyo Mtibwa ilicharazwa mabao 2-0 na Yanga, huku ilitoka suluhu mbele ya Dodoma Jiji mechi zote zikipigwa ugenini na Malimi amesema mechi iliyopigwa dhidi ya watetezi Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex ilikuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao wana wachezaji wakomavu ambao kila mmoja ana uwezo wa kuamua matokeo.
“Ukikutana na timu ambayo ina wachezaji wanane ndani ya uwanja ambao kila mmoja anaweza akaamua matokeo kwa uwezo binafsi lazima hiyo mechi inahitaji umakini wa hali ya juu, hicho ndicho nilichokiona dhidi ya Yanga,” amesema Malimi na kuongeza;
“Japo mshambuliaji wa timu hiyo Prince Dube yupo katika upepo wa kukosa mabao lakini ni hatari kwa kutengeneza nafasi. Laiti kama anaocheza nao mbele wakimsoma vizuri wanaweza wakawa wanafunga mabao mengi katika mechi moja.
“Dodoma Jiji ina wachezaji wazuri, mechi ilikuwa ngumu ilitumia ufundi zaidi ingawa hatukufungana, lakini ilitumika nguvu kubwa na akili hadi zinamalizika dakika 90 mchezaji unakuwa umechoka sana.”
Mbali na hilo, amesema msimu huu kwa upande wake anatamani uwe wa mafanikio ya kuonyesha uwezo wake na kuingia miongoni mwa makipa waliozisaidia timu zao kufanya vizuri.
“Japokuwa hatujaanza vizuri katika mechi tano tumeshinda moja, sare mbili na kufungwa kufungwa mbili, naamini makocha wanaendelea kufanyia kazi dhaifu ili mechi zinazokuja tuwe bora zaidi,” amesema Malimi.
Mtibwa iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Bara mwaka 1999 na 2000 ilishuka daraja msimu uliopita kabla ya kurejea msimu huu na kwa sasa inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi tano na itashuka uwanjani Jumatano ijayo kuvaana na KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
