Dk Mwigulu aanza na mkandarasi, aagiza akamatwe

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kukamatwa na kuzuiwa kwa hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala mkoani Singida.

Kauli hiyo ya Dk Nchemba, inatokana na kusuasua kwa mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Impresa Di Costruzioni Ing. E. Mantovani S.P.A kwa miaka miwili tangu 2016, lakini imechukua miaka minane na haujakamilika.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa leo, Ijumaa Novemba 21, 2025, imeeleza Dk Nchemba ameagiza hayo alipokagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida.

Amesema mkandarasi huyo aliaminiwa na kupewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa zaidi ya miaka minane tangu mwaka 2016.

Dk Nchemba ameeleza jitihada zimefanyika kuona mradi huo unaendelea, lakini mkandarasi amekuwa kikwazo cha utekelezwaji wake kwa kuwa ilitangazwa amefilisika.

“Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwa sababu ameicheleweshea mradi,” amesema Dk Nchemba.

Kutokana na hilo, amemwelekeza Kamishna wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala akamate hati yake ya kusafiria ili asitoke nje ya Tanzania hadi jambo hilo litakapoisha.

“Hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi anaifanyia nchi yetu, Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemwajiri, tunamlipa lakini anajiamulia kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe,” amesisitiza.

Ametumia tukio hilo, kuwasihi wakandarasi wa nje kufahamu kuwa, wanapokuja kufanya kazi nchini, watambue Tanzania imewaajiri na wasijione mabosi.

“Naelekeza wale washirika wetu katika mradi huu, ndani ya mwezi huu jambo hili liwe limekwisha watuambie wanaendelea au hawaendelei, na Kama hawataendelea Waziri wa Ujenzi uwapatie wakandarasi wadogo wamalizie kazi hii, hii nchi ni yetu na tuna wajibu wa kuilinda,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Nchemba ameiagiza Wizara ya Ujenzi ihakikishe inausimamia mradi huo ili ukamilike na itumie wakandarasi wazawa.

Katika ziara hiyo pia, amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kuwaelekeza wakandarasi wote kuhakikisha kila aliyepewa kazi apime kiwango cha kazi aliyofanya kama kinaendana na thamani ya fedha alizopokea.

“Haya ndiyo maelekezo ya Rais kwamba kila mradi, thamani ya fedha iendane na kazi ambayo imeshafanyika, sisi wasaidizi wake tutafuatilia maelekezo haya, hatutaruhusu watu wachezee nchi yetu,” amesema.

Ametoa wito kwa vijana nchini kuilinda Tanzania, ili iendelee kuwa na maendeleo.

“Mungu ametupa nchi nzuri, nchi hii si mali ya viongozi, nchi hii si mali ya vyama vya siasa, nchi hii ni yetu sote,” ameeleza.

Kwa upande wake, Ulega amesema mradi huo ni wa kielelezo na una faida nyingi zitakazolisaidia Taifa ikiwemo kuokoa fedha zinazowekwa kwenye barabara.

“Vilevile eneo hili litakuwa la kibiashara kwa sababu watu watapata nafasi ya kufanya biashara na wananchi kutengeneza uchumi wao, sisi wizara ya ujenzi tupo tayari kujenga ili mradi huu urejee” amesema Ulega.