Ekari 500,000 zatengwa Chunya uwekezaji kilimo cha umwagiliaji

Chunya. Ili kuongeza wigo wa  ukusanyaji wa mapato ya ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya  imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 500,000, kwa ajili ya ujenzi miundombinu ya kisasa ya  kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga.

Eneo hilo limetengwa katika Kijiji cha Sipa, Kata ya Kambikatoto  wilayani humo, kwa  lengo la kuongeza wigo wa fursa za uzalishaji  wa  mazao ya kimkakati  na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Novemba 21, 2025, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chunya, Tamim Kambona amesema licha ya kutenga eneo hilo kuna vijiji tayari walianza uzalishaji wa zao la mpunga cha kutegemea maji ya  msimu wa  mvua.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya,Tamim Kambona akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa  Novemba 21,2025,kuhusiana na mikakati yao kuwekeza kwenye sekta ya kilimo.Picha na Hawa Mathias

“Mikakati ya halmashauri ni kuongeza wigo mpaka katika sekta ya kilimo lakini mbali na kutenga eneo la  kilimo cha umwagiliaji kuna maeneo ambako wakulima wanaendelea kuzalisha kwa kutegemea msimu wa mvua pekee,” amesema.

Amesema mradi huo  umefikia hatua nzuri ambapo kwa sasa wanasubiri tathmini  ya wataalamu wa tume ya umwagiliaji  ili kuwezesha halmashauri kuanza  utekelezaji wa ujenzi  wa miundombinu.

“Mradi huo ukikamilika  utaongeza wigo mpana kwa wakulima kuongeza tija kubwa ya uzalishaji na kuweka ziada ya kuuza maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi,” amesema.

Mchango wa sekta ya kilimo

Kambona amesema asilimia 50 ya mapato ya halmashauri hutegemea sekta ya kilimo hususani  zao la tumbaku  licha ya kuwepo mazao mengine ya hususani ufuta, karanga, alizeti ,korosho na mahindi.

Amesema  kwa  mwaka fedha 2021,walifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh3.5 bilioni, sawa na asilimia 75,huku mwaka 2024/2025, yameongezeka na kufikia kiasi cha  Sh12 bilioni.

Kambona ametaja siri ya ongezeko la mapato ya  halmashauri  kuwa ni pamoja na kujenga  mahusiano mazuri na wadau wa sekta ya madini na kilimo kwa kuboresha mazingira rafiki  hususani uhakika wa masoko.

“Lakini pia  uwekezaji mkubwa wa Serikali ya awamu ya sita ikiwepo ujenzi wa masoko ya kisasa ya  madini ya dhahabu, upatikanaji wa pembejeo za kilimo na uwezeshaji  vyombo vya usafiri kwa maofisa ugani kupitia mapato ya ndani imeleta tija katika ufuatiliaji,” amesema.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo Mifugo na Uvuvi,Wilaya ya Chunya,Cuthbert Mwinuka akieleza hali ya uzalishaji  wa mazao mchanganyiko hususani tumbaku.Picha na Hawa Mathias.

Kwa upande wake Msimamizi wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na uvuvi, Cuthbert  Mwinuka amesema licha ya kuzalisha mazao mengi ya kimkakati ,lakini zao kuu ni  tumbaku ambalo huchangia asilimia kubwa ya mapato ya halmashauri.

Mwinuka amesema awali wakati kuna kampuni moja la ununuzi kwa mwaka 2019,tumbaku ilichangia pato la  Sh1.3 bilioni, mwaka 2022,  Sh3.1 bilioni ,lakini msimu wa kilimo 2024,2025, yaliongezeka Sh5.4 bilioni jambo ambalo linaleta tija kubwa katika kuchochea miradi ya maendeleo.

“Ongezeko  ni kutokana na wakulima kuhamasika kuzalisha kwa tija kufuatia mifumo mizuri ya  Serikali ya upatikanaji  wa mbolea na pembejeo za ruzuku ,elimu  ya kilimo bora na  kuzingatia  mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.

Katika hatua nyingine ,Mwinuka amesema katika kuongeza tija ya uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji wanahitaji  Sh700 milioni , kwa ajili ya  kufanya upembuzi katika skimu nne   lengo likiwa ni kusaidia wakulima kuzalisha mazao pasipo  kutotegemea msimu wa mvua pekee.

Mkulima wa tumbaku Emmanuel Lipson amesema licha ya zao hilo kuwa na mchango mkubwa wa pato la halmashauri  wanaomba uwekwe mfumo rasmi kwa makampuni  kuweka amana isiyo hamishika.

“Tunashauri Serikali kuja na mkakati wa kutunusuru wakulima kutolanguliwa maana kuna baadhi ya kampuni huchukua tumbaku na kuondoka bila kutulipa fedha jambo ambalo linazorotesha uzalishaji katika msimu husika,” amesema.