Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam (AKH-D), imeandika historia mpya, baada ya kutunukiwa tuzo mbili katika Kongamano la 48 la Hospitali Duniani.
AKH-D imetunukiwa tuzo hiyo na Shirikisho la Kimataifa la Hospitali (IHF), ikiwa miongoni mwa taasisi chache kutoka Afrika Mashariki zilizofanikiwa kutambulika kwa ubora, uongozi thabiti na uwajibikaji wa kijamii.
Tuzo hizo zimetolewa mwanzoni mwa Novemba mwaka huu, Geneva nchini Uswisi wakati wa mkutano wa 48 wa hospitali duniani.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Novemba 21, 2025 na Mratibu wa Mawasiliano wa AKH-D, Geofrey Anael, inaeleza tuzo hizo zilikuwa zinashindaniwa na hospitali takrihan 700 kutoka mataifa 38.
“Aga Khan ilipata Tuzo ya Shaba ya Uongozi na Usimamizi kutokana na mafanikio makubwa ya Mradi wa Uimarishaji wa Udhibiti wa Saratani (TCCP), uliolenga kuongeza uwezo wa uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa ugonjwa huo nchini,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa ya IHF, inaeleza tuzo hiyo hutolewa kwa taasisi zinazoonyesha dira ya kimkakati, uamuzi wa kitaasisi wenye ushahidi na uwezo wa kuunganisha timu mbalimbali kukabiliana na changamoto tata za kisekta.
Ufanisi wa AKH-D katika kusimamia TCCP umetajwa kama mfano wa uongozi wa kisasa unaojikita katika matokeo na mabadiliko ya kimfumo.
Mbali na hiyo, hospitali hiyo pia imetunukiwa Tuzo ya Heshima kupitia Seddiqi Holding Excellence Award for Social and Environmental Responsibility, ikilenga uwajibikaji wa kijamii na kimazingira.
“Hii ni kutokana na mchango wake katika uwajibikaji wa kijamii, ikiwamo kambi za upasuaji za bure kwa wanawake na watoto walioathiriwa na ajali za moto na ukatili, sambamba na sera yake ya kuelekea kukomesha uzalishaji wa hewa ukaa,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika taarifa yake, Aga Khan, imesema kwa zaidi ya miaka 90, taasisi hiyo imekuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma nafuu, bora na za viwango vya kimataifa.
Imesema imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, teknolojia ya tiba na kujenga utamaduni wa huduma unaoweka mgonjwa mbele ya kila kitu, jambo lililochangia kuifanya kutambulika kimataifa.
Taarifa hizo inaeleza tuzo hizo mbili si tu zinaiinua AKH-D kimataifa, bali zinaonyesha namna Tanzania inavyopiga hatua katika kujenga mifumo endelevu ya afya, inayojikita kwenye ubora, usalama na ubunifu.
IHF iliyofanyika tangu mwaka 1929, inawakilisha zaidi ya hospitali 25,000 duniani na hutumika kama jukwaa la kujifunza, kujadiliana na kubuni mikakati ya kuboresha huduma za afya.
Kupitia tuzo hizo, IHF hutambua taasisi zinazobadilisha maisha ya jamii kupitia miradi yenye athari chanya.
Hospitali ya Aga Khan inayofanya kazi katika nchi tisa, ikiwemo Tanzania, Pakistan na Kenya, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aga Khan na taasisi nyingine za AKDN, inaendesha zaidi ya hospitali na vituo 940 duniani na kuhudumia watu milioni 14 kila mwaka.
