Jamhuri yaweka wazi ushahidi itakaoutumia kesi ya Jatu

Dar es Salaam. Mashahidi 60 wanatarajiwa kuitwa na Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi wa Kampuni ya Jatu Public Limited Company (PLC), Peter Gesaya na wenzake, inayohusiana na ubadhirifu na utakatishaji fedha zaidi ya Sh3 bilioni.

Mbali ya idadi hiyo ya mashahidi vilevile Jamhuri inatarajia kuwasilisha jumla ya vielelezo 136, kati ya hivyo 104 zikiwa ni nyaraka na 32 vikiwa ni vitu halisi.

Idadi hiyo ya mashahidi hao pamoja na vielelezo imebainishwa na waendesha mashtaka leo Ijumaa, Novemba 21, 2025, wakati wa mwenendo kabidhi (committal proceedings).

Katika hatua hiyo waendesha mashtaka katika kesi hiyo wamewasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi hao pamoja na vielelezo hivyo.

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo hayo ya mashahidi na vielelezo hivyo na jopo la waendesha mashtaka watatu lililoongozwa na Wakili wa Serikali Roida Mwakamele kwa zamu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Goefrey Mhini, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, kesi hiyo  ilikokuwa ikisikilizwa katika hatua ya uchunguzi wa awali.

Mbali na Gasaya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 491356 ya mwaka 2023 ni Nicholaus Fuime, Esther Kiya, Habiba Magero, Mariam Mrutu, Mariam Kusaja, Lucy Izengo, na Jatu PLC.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 37, mashtaka matano kati yao yakiwahusu washtakiwa wote na mashtaka 32 yakiwahusu mshtakiwa wa kwanza, Gasaya na wa nane, Jatu PLC peke yao.

Mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni kuongoza genge la uhalifu,  matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia hasara mamlaka, huku mengine 33 yakiwa ni ya utakatishaji fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari Mosi, 2019 hadi Desemba, 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kuwa  waliandaa genge la kihalifu kwa nia ya kufanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh 3,149,172,167 (zaidi ya Sh3.1 bilioni) mali ya Jatu Savings and Credit Cooperative Society Limited.

Katika shtaka la pili, mshitakiwa wa kwanza (Gasaya) na wa pili (Fuime), wanadaiwa kuwa Februari 28, 2019 Dar es Salaam katika utekelezaji wa majukumu yao kama Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Jatu Saccos na Jatu PLC walitumia vibaya nafasi zao kwa kusaini makubaliano (MOU) kati ya Jatu PLC na Jatu Saccos.

Wanadaiwa kusaini mkataba huo kinyume na Kanuni za Vyama vya Ushirika za Mwaka 2015 na Vyama vya Akiba na Mikopo za Mwaka 2019 na kusababisha Jatu PLC  kupata faida isiyostahili yenye thamani ya zaidi ya Sh3.1 bilioni.

Shtaka la tatu liliwahusu washitakiwa sita, wa pili hadi wa saba.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es salaam wakiwa watia saini wa akaunti ya benki ya NMB ya Jatu Saccos bila uaminifu walitumia kwa maslahi yao binafsi zaidi ya Sh63 milioni mali waliyoaminiwa kwa nafasi zao.

Shtaka la nne, ambalo ni la kusababisha hasara linawahusu washtakiwa wote.

Wanadaiwa kuwa katika tarehe na eneo tajwa hapo juu washitakiwa wote kwa vitendo vyao vya makusudi walisababisha Jatu Saccos kupata hasara ya kifedha kwa  kujihusisha moja kwa moja katika miamala ya zaidi ya Sh bilioni 3.1 bilioni, wakijua kuwa fedha hizo ni matokeo ya kosa la msingi yaani ubadhilifu na matumizi mabaya ya mali.

Shtaka la tano ambalo ni la utakatishaji fedha linawahusu washtakiwa wote.

Wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kato ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2021 walijihusisha moja kwa moja katika miamala ya kifedha inayohusisha zaidi ya Sh3.1 bilioni, huku wakijua kuwa wakati wanajihusisha na miamala hiyo ilikiwa ni mazao ya kosa tangulizi la ubadhirifu.

Mashitaka 32 ya utakatishaji fedha kuanzia Shtaka la 6 mpaka la 37 yanamkabili mshitakiwa wa kwanza, Gasaya  na wa nane, Jatu PLC wakidaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya  Julai 1, 2017 hadi Februari 25, 2025.

Wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho walinunua mali mbalimbali zikiwemo magari, pikipiki, trekta na shamba.

Magari manne kati ya hayo aina ya Toyota IST, magari matatu aina ya Nissan X-Trail, Suzuki Carry ,Toyota Rav 4 moja, Toyota Alphard namba, Toyota Mark II, Toyota Noah, Toyota Land Cruiser Prado,Toyota Succeed, Toyota Townace Noah na  Toyota Fancargo.

Matrekta matanoni ya aina ya New Holland Model TT65 4WD, New Holland Model TT55-2WD, New Holland Model TD Straddle 80 4WD, New Holland Model AGR Tractor, mashine ya kuvunia aina ya Field King Combiner Harvester, malori mawili aina ya Mitsubishi Canter, na Toyota Toyoace.

Pia, kuna pikipiki sita, moja aina ya Sanlag Model SL125-5, nyingine tano aina ya Fekon na shamba moja lenye hati namba 288 LO Na. 184971 lenye ukubwa wa ekari 500 lililopo Matui, Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.

Washtakiwa hao, Gasaya na Jatu PLC wanadaiwa kujipatia mali hizo  zote kwa fedha zilizotokana na kosa la ubadhilifu na matumizi mabaya ya mali.

Mashahidi na maelezo yao ya ushahidi

Katika mashahidi hao wamo maofisa sheria kutoka Wakala wa usajili wa Kampuni (Brela) na mamlaka za usajili wa  vyama vya ushirika na taasisi za akiba na mikopo na na kutoka kitengo cha usajili wa vyombo vya moto cha Mamlaka ya Mapato (TRA).

Pia, wamo kwa wingi wanachama wa Jatu fani mbalimbali wakiwemo wastaafu kutoka taasisi za kifedha kama vile benki na askari polisi.

Pamoja na mambo mengine katika maelezo yao wameelezea usajili wa kampuni ya Jatu  PLC inayojihusisha uwekezaji katika kilimo cha mazao mbalimbali na Jatu Saccos na taratibu za uendeshaji, wanachama walivyojiunga.

Pia, wameeleza ahadi na mikakati waliyopewa, uwekezaji walioufanya, faida (walivyonufaika awali kabla ya baadaye kukwama, kwa kutokulipwa pesa zao ambazo wanazodai mpaka sasa.

Vilevile wameeleza uhamishaji wa fedha kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos kwenda kampuni ya Jatu PLC, huku wakibainisha taratibu zilizopaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mkataba wa makubaliano ya mkopo huo ambao hata hivyo wameeleza kuwa haujawahi kuwepo

Hata hivyo, kwa leo ni maelezo ya mashahidi 40 tu yaliyosomwa kati ya 60 na Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo mpaka Jumatatu Novemba 24, 2025, kuendelea kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi waliosalia pamoja na vielelezo, ambavyo pekee vina kurasa zaidi ya 4000.