Kipa Singida Black Stars aibua gumzo Nigeria

Gwiji wa soka nchini Nigeria, Yakubu Aiyegbeni, ameibuka na kuhoji uamuzi wa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Eric Chelle, wa kumjumuisha kipa anayekipiga nchini Tanzania, Amas Obasogie, kwenye kikosi chake kilichoshindwa kufikia lengo la kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Nigeria ilishindwa mtihani huo, kwa kufungwa na DR Congo kwa mikwaju ya penalty 4-3, baada ya sare ya 1-1 kudumu kwa dakika 120, Jumapili, Novemba 16, 2025.

Chelle amekuwa akimuita Obasogie mara kwa mara kwenye kikosi chake, lakini kipa huyo wa Singida Black Stars SC, hajawahi kupata nafasi ya kukaa langoni akiwa na timu ya taifa, kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Akizungumza kwenye podikasti ya Home Turf, Yakubu amesema: “Kihistoria, makocha huwa wanajumuisha mchezaji mmoja au wawili wa nyumbani, kwangu mimi hilo silikatai, ni jambo jema kabisa, lakini kwa hili la Obasogie, sikubaliani nalo kabisa.

OBA 02

“Ninaamini ni vigumu kwa Chelle kututhibitishia, ni vipi alikuwa anamfuatilia Obasogie  katika Ligi Kuu ya Tanzania, na kuwaacha makipa wanaocheza Ligi Kuu ya Nigeria ambayo kila wiki ninaimani anaifuatilia akiwa hapa, sasa atuambie alikuwa anajigawa vipi kwa Nigeria na Tanzania, hadi kuamua kumchukua Obasogie mara zote hizo?

“Akisema hajavutiwa na makipa wa hapa, pia atueleze sababu kwa nini? Binafsi ninaamini kulikuwa na sababu ya kujaribu kwa wachezaji wengine, sio kuwa na mtu ambaye unamwita zaidi ya mara tano halafu humtumii, ni bora ungewachukua na wengine wakapata uzoefu basi,” amesema Yakubu.

OBA 01

Yakubu ametoa dukuduku lake, baada ya kujiridhisha kuwa Obasogie yupo kwenye nafasi ya chini katika mpangilio wa kocha Chelle, tofauti na wachezaji wengine ambao wamekuwa akiitwa kwenye kikosi cha Super Eagles.